Sababu za ugumba kwa wanaume

Muktasari:

  • Yako mambo yanayosababisha utengenezaji wa mbegu zisizo na ubora zinazokosa ufanisi wa kazi yake, mambo hayo ikiwamo kuzaliwa na korodani ambazo hazijashuka kutoka tumboni.

Zipo sababu mbambali zinazochangia ugumba kwa wanaume ikiwamo matatizo ya kuzaliwa nayo au kuyapata ukubwani ikiwamo magonjwa mbalimbali. Matatizo yafuatayo yamekuwa ndio mara kwa mara chanzo cha kujitokeza kwa tatizo la ugumba kwa wanaume. Utengenezwaji wa mbegu zilizo dhaifu

Yako mambo yanayosababisha utengenezaji wa mbegu zisizo na ubora zinazokosa ufanisi wa kazi yake, mambo hayo ikiwamo kuzaliwa na korodani ambazo hazijashuka kutoka tumboni.

Kwa kawaida kabla ya kuzaliwa kokwa za kiume huwa zipo ndani ya pango la tumbo na hutakiwa zishuke kuelekea sehemu za uzazi baada ya kuzaliwa, kushindwa kushuka na kuhifadhiwa katika korodani husababisha mbegu au kokwa kuharibika kutokana na joto kali la tumboni.

Kushuka na kuning’ia kwa korodani ni maumbile sahihi ya kibailogia yenye tija kiafya ambayo huwezesha kupata joto la wastani hivyo kutengenezwa mbegu zenye kiwango.

Matatizo kwenye mfumo wa chembe za urithi mwanadamu anaweza kurithi chembe za urithi zenye maelekezo ya kimwili yasiyo ya kwaida hivyo kujikuta akizalisha mbegu zisizo na ubora.

Maambukizi ya virusi hatari ikiwamo virusi vya mumps na maambukizi sugu ya magonjwa maeneo ya uzazi.

Ajali za bahati mbaya zinazotokea wakati wa upasuaji wa kurekebisha matatizo ya kiafya ikiwamo katika korodani au ngiri(hernia) na aina ya kizamani ya upasuaji wa tezi dume.

Kuwahi kuasiliwa na kufungwa kitanzi katika mrija kama njia za uzazi wa mpango.

Kuongezeka ukubwa wa mishipa inayorudisha damu mwilini kutoka katika kende/kokwa huweza kusababisha damu kwenda kwa kasi eneo hilo na kuongeza joto hivyo kuathiri ufanisi wa utengenezaji wa mbegu hizo ikiwamo wingi wake na maumbile.

Uwepo wa vizuizi katika utolewaji wa mbegu za kiume

Matatizo ya kujamiana ikiwamo wanaume kuwa na tatizo la kutoa mbegu haraka isivyo kawaida wakati wa tendo, tatizo la mbegu kuchepukia katika kibofu cha mkojo badala ya kupitia katika mrija wa wa mkojo.

Matatizo ya kimaumbile ikiwamo uwepo wa vizuizi katika kokwa, mirija na inayobeba mbegu.

Kuugua magonjwa ya zinaa mpaka kufikia madhara ya kuharibu mfumo mzima wa utengenezwaji wa mbegu za kiume.

Kukumbana na kemikali sumu mbalimbali

Zipo baadhi ya kemikali ambazo kama mwanaume zitamwingia mwilini au kukaa katika maeneo yenye kemikali hizo kwa muda mrefu zinaweza kumletea ugumba.

Kemikali hizo ikiwamo za madawa ya kilimo, rangi, mipira, mionzi na dawa za steriods. Unywaji pombe kupindukia ni tatizo ambalo limekuwa likizidi kuwa kubwa, hii ni kutokana na maendeleo ya kichumi watu wengi wamejiingiza katika unywaji wa pombe uliopindukia.

Matumizi ya madawa ya kulevya kama cocaine, bangi, hashishi, mihadarati yote hayo hupunguza idadi na kiwango cha shahawa .

Matumizi ya baadhi ya dawa za matibabu kama cimetidine, spironolactone na Nitrofurantoin.

Madhara ya saratani na matibabu yake ambayo yanahusisha mionzi na kemikali tiba za saratani nazo zinaweza kuathiri utengenezwaji wa mbegu za kiume.

Uondolewaji wa kokwa za kiume baada ya kupata saratani au uvimbe. Kupata ajali maeneo ya uzazi.