Sababu za wapenzi kutokuwa waaminifu kwenye ndoa-2

Muktasari:

  • Watoto wa familia nyingi wamebaki kuwa waathirika wa tatizo hili na bado hakuna dalili za tatizo hili kupungua.

Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na wimbi kubwa na malalamiko ya kila kukicha ya wanandoa wengi kutokuwa waaminifu. Wapo waliokabiliana na misuguano, mapigano na magomvi mengi kwa sababu ya jambo hili na wapo ambao tayari wameshaamua kutengana.

Watoto wa familia nyingi wamebaki kuwa waathirika wa tatizo hili na bado hakuna dalili za tatizo hili kupungua.

Kila mmoja akiulizwa anatoa sababu yake binafsi ya kwa nini ametoka au aliamua kutoka nje ya ndoa yake, sababu hizi zina mfanano na pia zipo baadhi zinazotofautiana.

Katika makala hii nimejaribu kuangalia baadhi ya sababu ambazo mara kwa mara zimeripotiwa na wanandoa wengi wanaokuja kutaka ushauri kwenye ofisi zetu.

Hii inafanya sababu hizi kuwa halisi na zitakazokupa msaada ukizielewa maana haziko kinadharia tu bali zimetokea katika maisha halisi ya ndoa za watu kama wewe.

Pamoja na yote haya ukweli unabaki kwamba matendo ya kukosa uaminifu kwenye ndoa au mahusiano yana athari mbaya na zinaweza kuambatana na maumivu makali na wahusika kuwa maadui badala ya wapenzi kama walivyokuwa awali.

Penzi kupoa au kufa

Penzi linapopoa au hata linapokufa hali huwa inaonyesha wazi kabisa. Kwenye kupoa mhusika anaweza kuanza kujihisi ndani ya moyo wake kutompenda mwenzake kama alivyokuwa akimpenda awali.

Inawezekana mwenzake hajagundua kuanzia mwanzoni kwamba penzi limepoa ila kama hali ya kupoa huku itaendelea lazima itagundulika. Baadhi ya vitu dhahiri vitakavyoweza kukufanya ufahamu kwamba penzi la mwenzako limepoa au kufa ni kwamba kuna mambo ambayo uliyazoea kuyaona yakifanywa kawaida hautayaona tena.

Kuna vitu vilikuwa vikifanywa pasipo kukumbushana sasa utalazimika kuviomba ili ufanyiwe, utaona kila kitu kinakuwa kigumu kumhusu mwenzako na hata uongeaji au kujibu kwake kunakuwa na walakini.

Kwenye tendo la ndoa nako mara nyingi ndiko kwenye kuonyesha taa nyekundu mapema, ule ushiriki, furaha na bashasha zilizokuwapo awali mkiwa kwenye tendo hauzioni tena, tendo la ndoa linafanywa kama jukumu la kawaida na mara nyingine hata hamu ya kushiriki haipo.

Hapa ndipo mmoja hukinai hiyo hali ya kulazimishana tendo la ndoa, au kupeana kwa masharti au kunyimwa au hata mmoja kupoteza hamasa ya kulifanya tendo hilo na mtu asiyekuwa na hisia naye.

Huo unakuwa mwanzo wa mmoja au wote kutoka nje. Penzi ni kama moto, ukiwashwa pasipo kuchochewa hupoa au hata kuzima kabisa. Wengi wanapoingia kwenye ndoa wanadhani mkishaoana basi mambo yanajiseti yenyewe tu, mapenzi yanajichanulia yenyewe tu, la hasha! Lazima kuwepo na jitihada za dhati za wanandoa kuhakikisha wanachochea penzi lao, kulilinda na kulipalilia ili liendelee kumea, kunawiri na kuzaa matunda.

Ushawishi wa marafiki

Wako watu wengi kwenye ushauri wa wanandoa na hata wale wasio wanandoa ambao wamekiri kuchepuka kwa sababu ya kushawishiwa na marafiki.

Ni lazima ukafahamu nguvu waliyonayo marafiki. Usipokuwa na hekima ya juu ya kuweza kuchagua nani wa kuwa naye rafiki na nani sio basi utajikuta unapelekeshwa kila upande hata kule usipopenda utapelekwa kwa sababu tu nguvu ya maamuzi haiko kwako tena bali iko kwa marafiki zako.

Yamkini unasema mimi ni rafiki tu sifanyi wanavyovifanya wao, mimi nasikiliza na kuchangia tu hoja zao, lakini ngoja nikwambie, taratibu utasikiliza, utaanza kuchangia na taratibu utavutika kuyafanya yale wanayoyafanya.

Hadithi ya kuchepuka kwao inaweza kuwa ya kawaida na kwako si ya kawaida lakini ukiendelea kukaa nao kidogo kidogo utaanza kuona kuchepuka si kitu cha kushangaza sana maana wengine nao wanafanya, na utaanza kidogo kidogo na mwisho utakuwa mtaalamu.

Wako waliofundishwa kiutaniutani leo hii ni wataalamu kuliko walimu wao. Jifunze kuwa na msimamo. Jifunze kuchagua marafiki wanaokujenga na si kukubomoa. Jifunze kufanya maamuzi binafsi yenye busara na yasiyokufungulia milango ya majuto. Kumbuka ukija kujuta hautokula majuto hayo na hao marafiki zako. Utayala mwenyewe na wanaokuhusu. Ni hasara na anguko kwako na familia yako na ndugu zako.

Ushawishi wa kilevi

Wako watu wanaojiamini na wanajihisi wenye uwezo wa kujizuia, lakini mara wakiwa katika ulevi wowote ule hushindwa kujizuia. Hili liko kwa wanawake na hata wanaume. Ulevi wowote hupunguza uwezo wa mtu Kufikiria ilivyo sahihi “rational thinking”.

Unaweza kukuta watu wameketi, wanaheshimiana lakini kadri wanavyoendelea kulewa wanaanza kushikana maungo na kila mmoja anaona ni sawa tu, heshima na nidhamu waliyokuwa nayo awali imeshapeperukia dirishani kwa sababu ya ushawishi wa ulevi.

Hali hii ina majuto sana maana mtu anajikuta kasha shiriki ngono na mtu mwingine, ama mtu anayemjua au hata asiyemjua pasipo utashi wake. Majuto yanakuwa makubwa zaidi maana mara nyingine hata usiri unakuwa haupo, heshima na nidhamu yako yote inaathirika.

Zipo baadhi ya pombe ambazo badala tu ya kukuondolea aibu, zinaweza kukulegeza mwili na viungo na kuongeza hamu ya ngono. Ndio maana watu wanaotumia vilevi wanashauriwa kuwa na wenza wao katika nyakati hizi ili walau kujizuia kuingia mitegoni.

Watu wengi tuliowahoji nyakati za ushauri wanakiri kwamba safari ya kuingia kwenye mahusiano ya kingono na watu wa nje ilisindikizwa zaidi na matumizi ya kilevi au vilevi na wengine wanaendelea kukiri kwamba ni ngumu kuchepuka bila kuwa na kilevi akilini.