Safari kutoka mwanafunzi bora kidato cha nne hadi kuwa nguli wa hesabu

Muktasari:

Aliwahi kuwa mwanafunzi bora kitaifa kidato cha nne mwaka 1988. Sasa Ni mhadhiri wa hesabu Chuo Kikuu cha Aga Khan

Kila swali aliloulizwa alitabasamu kwanza kabla ya kujibu.

Tabasamu lake linamtofautisha na walimu wengi wa Hisabati, ambao wanafunzi huwa wanatafsiri ukali kwenye sura zao kwa kutotabasamu hasa wanapofundisha.

Japo ni mhadhiri wa chuo kikuu, hataki ajulikane kwa jina la mhadhiri, daktari au profesa. Ukitaka kumfurahisha mwite ‘mwalimu’

Tofauti na wengi, hafichi hisia zake kwamba yeye anapenda zaidi kuitwa ‘mwalimu’ badala ya mhadhiri’. Ndiyo maana hata umuonapo hukosi kumaizi haiba ya ualimu aliyonayo.

Huyu ndiye mwalimu Veronica Sarungi ambaye mwaka 1988 alikuwa msichana aliyeongoza kitaifa katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne akitokea Shule ya Sekondari Zanaki ya jijini Dar es Salaam.

Ndoto yake ni kuwa mwalimu wa walimu na sasa anaitekeleza vilivyo ndoto hiyo akiwa mwalimu katika Chuo Kikuu cha Aga Khan cha jijini Dar es Salaam.

“Napenda sana ualimu, natamani kuona watoto wote wanajua hesabu na ili kutimiza ndoto yangu niliamua kufundisha walimu ili wakawafundishe wanafunzi vizuri,” anasema na kuongeza:

“Sisomi nipate cheti, nasoma ili nitimize ndoto yangu ya kuwasaidia watu. Unajua hata mara ya kwanza nilipomaliza shule nilijitafakari nikagundua napenda kusaidia watu wapende hesabu. Mwanzoni nilidhani ningefundisha watoto wadogo ila nikaanza kufundisha walimu.”

Ni kwa sababu hii anasema mwaka 1997 aliporejea nchini kutoka masomoni, hakuona jambo jingine la kufanya zaidi ya kubobea kwenye ualimu.

Afanya utafiti wanafunzi kufeli hesabu

Kilio cha wanafunzi kufeli somo la Hisabati kila siku kilimfanya atafakari namna anavyoweza kusaidia kukinyamazisha.

Alianza kufanya utafiti wa somo hilo ambalo yeye anaamini ni kati ya masomo rahisi.

Anasema alichukua wanafunzi wa darasa la nne waliofeli Hisabati, akawafundisha kwa muda.

Baadaye anasema robo tatu ya wanafunzi hao walifaulu na hapo ndipo alipogundua kuwa wanafunzi hawafundishwi ipasavyo. Huo ukawa mwanzo wa kuamua kufundisha walimu na hatimaye kusomea shahada ya uzamili ya ufundishaji walimu akijikita katika hesabu.

“Nilijiuliza kweli hawajui? Ilibidi niwafundishe nikitumia mbinu za michezo na kuwashirikisha wanafunzi wenyewe ninapo wafundisha. Walifaulu vizuri kwa hiyo nikaona natakiwa kuwa mwalimu ili nisaidie kuwaandaa walimu nikiwafundisha mbinu za kufundisha hesabu,” anaeleza.

Unapomuuliza, kama somo la Hisabati ni gumu. Jibu la Veronica ambaye hupenda kuchanganya Kiswahili na Kiingereza katika mazungumzo litakuwa: ‘no, no, no’

Ukimtaka afafanue atakueleza hivi: ‘’Hesabu sio ngumu hata kidogo, ni fani rahisi kuielewa ila ugumu unakuja pale mtu asipojua kanuni. Hesabu ni kama kujenga nyumba lazima uanze hapa, uje hatua ya pili ukikosea tu basi.”

Kinara wa masomo

Haishangazi kuona sasa Veronica anafundisha somo ambalo kwa wengi wanaamini ni gumu tena kwa ngazi ya elimu ya juu.

Uwezo wake darasani ulianza kuonekana tangu akiwa darasa la kwanza na ilikuwa kawaida kwake kuwa mtu wa kwanza.

Anasema tangu mdogo alijua anapenda kusoma hesabu hivyo, alipofika kidato cha tano baada ya kupata ufaulu wa daraja la kwanza kwa alama saba, akaamua kujikita kwenye masomo ya Hisabati, Fizikia na Kemia.

“Unajua wakati nimefaulu hata dhana ya mwanafunzi bora haikuwa kama sasa unaamka na kuona magazeti yameandika, wakati ule ulipewa taarifa tu. Nakumbuka niliitwa kwenye hafla kupongezwa,” anasimulia Veronica.

Ndoto yake maishani

Veronica ambaye ni dada wa mwanaharakati Maria Sarungi ana ndoto moja maishani, nayo ni: ‘’Nataka ifike sehemu watoto wajue hesabu.’’

Ni kwa sababu ya wito huu alionao kwa watoto na jamii kwa jumla, Veronica anayependa kuimba nyimbo za dini, ameamua kusahau habari za kuwa na familia yake.

“Ndoto yangu ni kuona walimu na wadau wa elimu wanafanya kazi pamoja ili kumsaidia mwalimu na kuwezesha watoto wajifunze,” anafafanua.

Anavyoitazama sekta ya elimu nchini

Huku akikuna kichwa, Veronica anasema Tanzania imepiga hatua katika elimu lakini bado yapo maeneo ya kuboreshwa na Serikali na walimu wenyewe kujiongeza kama wadau muhimu.

“Mwalimu darasani anaweza kumkaribisha mwalimu mwenzake awafundishe watoto. Mwalimu akimkaribisha mwingine naye atapata nafasi ya kujifunza na watoto hawataona somo kama linawachosha,” anasema.

Kwa upande wa Serikali, anasisitiza suala la mafunzo kazini. Anashauri kuwapo kwa mfumo wa kumuendeleza mwalimu na kumfanya awe na ari ya kufundisha.