Seif ahitimisha kesi 35 dhidi ya profesa Lipumba

Muktasari:

Wakati Maalim Seif na kambi yake wakihamia ACT- Wazalendo, nyuma wameacha utitiri wa mashauri hayo ambayo Maharagande amesema yote yanaondolewa.

Uamuzi wa mahakama kutambua nafasi ya Profesa Ibrahim Lipumba ndani ya CUF na hatimaye katibu mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad kutimkia ACT-Wazalendo, umehitimisha kesi zaidi ya 35 kortini.

Kwa takribani miaka miwili na nusu CUF imekuwa katika mgogoro mkubwa wa kiuongozi ulioambatana na kesi kedekede zilizokuwa zinasubiriwa kuamua hatima yake.

Uamuzi wa juzi wa kutambua mamlaka ya Msajili wa Vyama vya Siasa aliyemtambua Profesa Lipumba ndio umetoa mwelekeo wa kumaliza kesi hizo zinazofikia 35, kwa mujibu wa upande wa wadai (Seif) au 39 kwa mujibu wa Profesa Lipumba.

Aliyekuwa kaimu naibu mkurugenzi wa habari, uenezi na mahusiano ya kimataifa wa upande wa Seif, Mbalalah Maharagande alisema kesi za msingi zilikuwa tano, ikiwamo ya kuhoji mamlaka ya msajili kumtambua Lipumba iliyotolewa uamuzi juzi na maombi mengine madogo ndani ya kesi yapatayo 30.

Kesi hizo zilifunguliwa kutokana na mgogoro uliokikumba chama hicho Juni 5, 2016 baada ya Profesa Ibrahim Lipumba kutengua barua yake ya Agosti 5, 2015 ya kujiuzulu uenyekiti na kutangaza kurejea madarakani, ikiwa ni miezi 10 baadaye.

Wakati Maalim Seif na kambi yake wakihamia ACT- Wazalendo, nyuma wameacha utitiri wa mashauri hayo ambayo Maharagande amesema yote yanaondolewa.

Mashauri yaliyofunguliwa

Miongoni mwa mashauri hayo yaliyokuwa yameshafunguliwa na kambi ya Maalim ni kupinga uamuzi wa Msajili kumtambua Profesa Lipumba. Walianza na kesi ya kuomba kibali cha kufungua shauri na kukipata kibali hicho, ndipo wakafungua rasmi maombi ya kupinga uamuzi huo wa msajili.

Katika shauri hilo ambalo lilikuwa la msingi, upande wa Seif ulikuwa unapinga Msajili kumtambua Profesa Lipumba kama mwenyekiti halali, wakidai kuwa alishajiuzulu na tayari walishamfukuza uanachama na pia kwamba Msajili hana mamlaka ya kutoa uamuzi huo.

Mbali na hiyo pia yalikuwapo mashauri ya kupinga uamuzi wa Mamlaka ya Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) kutambua bodi ya wadhamini ya kambi ya Lipumba, kupinga uamuzi wa kuwavua ubunge wabunge wa wanane wa viti maalumu, kupinga utaoji wa ruzuku kwa kambi ya Lipumba na ile ya kuzia mkutano mkuu kufanyika.

Ndani ya kesi hizo kuliibuka maombi mengine ya mapitio na rufaa, kama kupitia uamuzi wa Jaji Sekieti Kihiyo kukataa kujiondoa katika kesi yao. Hadi uamuzi wa mapitio ulipotoka Jaji Kihiyo alikuwa ameshastaafu, hivyo shauri hilo lilirudishwa Mahakama Kuu na kupangiwa jaji mwingine.

Kesi ya wabunge

Katika kesi ya namba 143 ya mwaka 2017, wabunge wanane na madiwani wawili wote wa viti maalumu walikuwa wanapinga uamuzi wa kambi ya Profesa Lipumba kuwavua uanachama na hivyo kupoteza ubunge wao.

Walikuwa wakiiomba mahakama hiyo itamke kuwa uamuzi wa kuwavua uanachama ni batili kwa madai kuwa haukuzingatia kanuni za haki za msingi, kwani hawakupewa nafasi ya kusikilizwa, na tayari walikuwa wameshakata rufaa kwa Mkutano Mkuu wa chama hicho.

Pia, kulikuwapo maombi ya kuzuia Bunge kuwaapisha wabunge wateule wanane, ambao hata hivyo maombi

hayo yalitupiliwa mbali na mahakama baada ya kukubaliana na hoja ya pingamizi lililowekwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, hivyo waliapishwa na kuendelea na kazi.

Lakini, baadaye Mahakama Kuu ilitoa amri ya zuio kwa CUF kujadili wala kuchukua hatua zozote dhidi ya uanachama wa wabunge waliotimuwa.

Uhalali wa bodi

Kesi hiyo namba namba 13 ya mwaka 2017 ilifunguliwa na Mbunge wa Malindi Zanzibar dhidi ya Rita akipinga wajumbe wa bodi ya kambi ya Lipumba.

Katika maombi hayo Jaji Benhajj katika uamuzi wake alitengua uteuzi wa wajumbe hao akisema kuwa haukufuata matakwa ya kisheria kwa kutokuwepo muhtasari wa kikao halali kilichopendekeza majina yao, na ambacho kinatakwa kusimamiwa na mamalaka halali ya Kiserikali.

Pia, alisema hata wajumbe waliokuwa wamependekezwa na kambi ya Maalim Seif hawakuwa na sifa kwani nao hawakuwa wametimiza matakwa hayohayo ya kisheria.

Msajili kuhusu ruzuku

Maombi namba 21 ya mwaka 2017, CUF Maalim walikuwa wakiomba kibali cha kumshtaki Msajili wa vyama kwa kitendo chake cha kutoa ruzuku ya chama kwa kambi ya Profesa Lipumba na kesi nyingine tofauti ya maombi zuio la ruzuku. Katika maombi hayo namba 28/2017, CUF Maalim walikuwa wakiomba zuio la muda dhidi ya msajili wa vyama kutoa ruzuku hadi shauri la namba 21/17 kupinga uamuzi wa msajili kutoa ruzuku kwa Lipumba litakapoamuriwa.

Zuio la muda la kutoa ruzuku

Katika maombi hayo namba 34 ya mwaka 2017, bodi ya CUF-Maalim ilikuwa ikiomba mahakama imzuie Msajili asiendelee kutoa ruzuku kwa Lipumba hadi kesi wanayokusudia kuifungua dhidi yake itakapoamuriwa. Pia, kulikuwa na maombi mengine kadhaa yahusuyo ruzuku ikidaiwa kuwa ilikuwa inaendelea kutolewa kinyemela.

Zuio la mkutano mkuu

Kulikuwa pia na mesi ya maombi ya kuzia mkutano mkuu yaliyofunguliwa na viongozi wawili kambi ya Maalim wakiomba mahakama itoe amri ya zuio dhidi ya kambi ya Profesa Lipumba kutokuandaa wala kuitisha mkutano mkuu kwa jina la CUF na walifanikiwa kupata zuio hilo.

Hata hiyo, mkutano huo uliitishwa hivi karibuni na kufanya maamuzi kadhaa, ikiwamo uchjaguzi mwenyekiti, Baraza Kuu na imeelezwa na Lipumba baadaye kuwa uliazimia kumtimua Seif uanachama.

Kinga kwa wabunge

Maombi hayo namba 21/17 yaliyofunguliwa na Abdallah Mtolea na wabunge wenzake 18 wa kambi Maalim Seif, mahakama iwape kinga ili wasijadiliwe na kuchukuliwa hatua yoyote na kambi ya Profesa Lipumba.

Hata hivyo, kabla ya kesi hiyo kuisha Mtolea alihamia CCM na kuchaguliwa tena kuwa mbungea.

Kupinga uongozi wa kina Sakaya

Ilifunguliwa pia kesi katika mahakama ya Kisutu dhidi naibu katibu mkuu, Magdalena Sakaya na viongozi wengine walioteuliwa na Profesa Lipumba katika nafasi za ukurugenzi wa idara mbalimbali.

Walikuwa wakiiomba mahakama iamue kuwa wadaiwa hao si viongozi halali wa chama hicho na itoe zuio la kudumu dhidi ya wadaiwa hao wasijihusishe na kazi zozote za chama hicho. Hata hivyo, maombi hayo yalitupiliwa mbali.

Mashauri ya kambi ya Lipumba

Kambi ya Lipumba ilikuwa imefungua mashauri mawili tu ambayo ni maombi ya kambi ya Lipumba ya kutaka kuunganishwa kwenye maombi ya bodi (Maalim) kuhusu kibali cha kumshtaki Msajili, wakidai kuwa na maslahi katika suala hilo.

Maombi mengine yaliitaka mahakama itoe zuio dhidi ya wanachama wote kambi ya Maalim wasiende katika ofisi za chama hicho Buguruni kwa lengo la kufanya usafi, kama walivyokuwa wamepanga awali.