Sekondari ya Bwiru yaonyesha mfano elimu ya ufundi

Muktasari:

  • Ukiondoa elimu ya darasani, wahitimu wengi hawana stadi za maisha ambazo pengine zingewasaidia kukabiliana na changamoto za kimaisha

Ukosefu wa ajira rasmi unawatesa wahitimu katika madaraja mbalimbali ya elimu nchini.

Ukiondoa elimu ya darasani, wahitimu wengi hawana stadi za maisha ambazo pengine zingewasaidia kukabiliana na changamoto za kimaisha.

Wadau wa elimu wanasema dawa ya tatizo hili ni kusisitiza mafunzo ya ufundi. Hiki ndicho kinachofanyika sasa katika Shule ya Wasichana Bwiru iliyopo jijini Mwanza. Kama hatua ya shule hiyo kuandaa wahitimu kitaaluma lakini wenye maarifa yanayoweza kuwasaidia kujiajiri, uongozi umeanzisha kiwanda kidogo cha ushonaji wa nguo.

‘Bwiru Industrial Initiative’

Msimamizi wa idara ya sanaa shuleni hapo, mwalimu Khadija Abeit anasema kiwanda hicho ni matunda ya mpango wanaouita Kiingereza kwa jina la Bwiru Industrial Initiative yaani mpango wa kutoa stadi za ufundi kwa wahitimu

“Kiwanda chetu kinahudumia wanafunzi zaidi ya 800 wa kidato cha tano na sita, hivyo basi dalili za awali zinaashiria kwamba tunaendelea vizuri,” anasema.

Anasema kiwanda hicho kimejikita katika ushonaji wa magauni, sketi, hijabu. Walianza na wataalamu kutoka nje, lakini sasa wanajivunia kuwapo kwa wanafunzi mafundi ambao nao wanaotoa mafunzo kwa wenzao.

Tofauti na masoko ya kawaida ambapo gauni ama sketi hufika Sh 10,000, mavazi hayo kwa Bwiru yanauzwa kwa Sh 3000

“Sokoni, sketi moja inauzwa Shs10, 000. Hii ni tofauti na bei zetu hapa shuleni japo muundo au muonekano wa nguo ni ule ule, ‘’ anasema.

Doreen James ni mmoja kati ya mafundi wa nguo shuleni hapo anayesema bidhaa wanazozitengeneza wanauza kwa wanafunzi wenzao na hata walimu.

“Tunashona sketi na mavazi mengine ya shuleni. Aidha, tunafuma, kuremba na kutengeneza bangili, skafu na vitu vyote vya urembo,” anaeleza.

Doreen anasema mpango huo umekuwa na manufaa makubwa kwa kuwa wapo baadhi ya wanafunzi wasiojiweza katika masomo ya kawaida darasani, lakini sasa wanafanya vizuri katika ufundi huo.

“Kwetu sisi, hii ni fursa kubwa sana ambayo kamwe hatuwezi kuipuuza. Wengi wametoka kupitia fani zisizukuwa rasmi na hivyo nasi tunapambana,” anasisitiza Doreen.

Mkuu wa Shule, Mekitilda Shija, anaeleza kuwa mradi huo umekuwa ni nguzo muhimu katika kuwajengea wanafunzi uwezo wa ziada.

“Niliposikia kwa mara ya kwanza kwamba wanafunzi wana mpango wa kuanzisha kiwanda, nilisikitika sana kwa kuwa nilifahamu kwamba haiwezekana kutokana na mazingira yenyewe. Leo hii natabasamu kwa kuona kwamba sare na baadhi ya bidhaa tunazo hapahapa shuleni,” anasema Mwalimu Shija na kusifu juhudi za shirika lisilokuwa la serikali la Kivulini lililojitolea zaidi ya vyerehani 15.

Mkurugenzi wa Kivulini Yassin Ali, anasema lengo lao ni kuona watoto wanapata maarifa ya kuwasaidia kufikia ndoto zao na pia kuwawezesha kujiajiri.

“Ni dhahiri kwamba tukiwawezesha watoto wetu kwa vitendo, wataenda mbali na kufanya vitu ambavyo ni vikubwa. Huo ni uwekezaji,” anaeleza.

Changamoto

Moja ya changamoto wanazokumbana nazo katika mpango huo ni ukosefu wa jengo maalumu kwa ajili ya shughuli za sanaa kwa jumla.

“Hatuna sehemu au jengo la kufanyia hizi shughuli za sanaa, imebidi kuvamia jengo ambalo ni ukumbi wa mikutano. Tukiwa na mikutano inatulazimu kuhamisha baadhi ya bidhaa zetu na kusimamisha kazi kwa muda,” anasema Mwalimu Shija na kutaja changamoto nyingine kuwa ni pamoja na uhaba wa vitendea kazi ukilinganisha na idadi ya wanafunzi.

Mbunge aokoa jahazi

Shukrani kwa Naibu Waziri wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula ambaye pia ni mmbunge wa Ilemela, kwa msaada wa matofali yanayotarajiwa kujenga jengo maalumu la shughuli za sanaa shuleni hapo