Serengeti Boys ina miaka 5 tu

Monday April 8 2019

 

By Imani Makongoro, Mwananchi [email protected],tz

Timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ inahesabu siku kabla ya kuanza harakati za kusaka ubingwa wa Fainali za Afrika kwa vijana (Afcon U17) Jumapili ijayo jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na Spoti Mikiki, Kocha wa Serengeti, Oscar Mirambo anasema jambo la msingi kwao ni kutwaa ubingwa lengo ikiwa ni kucheza Fainali za Kombe la Dunia baada ya kuwa mabingwa wa Afrika.

“Watoto kwa umri wao wamepata uzoefu wa kimataifa naweza kusema Serengeti Boys tuko tofauti msimu huu,” anasema Mirambo.

Anasema timu hiyo imekuwa ikishindana na wachezaji ambao wamewazidi umri ili kuwajenga zaidi katika maandalizi na wamefanikiwa.

Safari ya Serengeti Boys

Kocha huyo kijana alianza kuinoa Serengeti Boys mwaka 2014 wakati huo ikiwa ni timu ya umri chini ya miaka 13, akichukuliwa kutoka Sekondari ya Makongo ambako alikuwa kocha na mwalimu wa soka wa shule hiyo.

“Nilipokuwa Sekondari ya Makongo niliomba kwa mkuu wangu wa kazi, nibaki kuwa kocha tu na masuala ya kufundisha nipumzike, kwani lengo la Makongo lilikuwa kuirejesha shule katika fomu kimichezo.

“Nilikubaliwa na kweli mikakati ikatimia kupitia timu ya Makongo, Dar es Salaam ikawa bingwa katika soka kitaifa kwenye mashindano ya Umisseta kuanzia 2011 na hapo ndipo familia ya mpira ikaanza kumfuatilia na kumfahamu.

Anasema hakwenda TFF kuomba kazi alipigiwa simu na kuitwa na utawala ambao walimwambia ‘interest’ za kutaka awe kocha wa timu hiyo.

“Nilipokubali walizungumza na menejimenti ya shule na pale nikaanza kazi TFF.

“Ilikuwa kitu kikubwa kwangu, kutoka kuwa kocha wa shule hadi timu ya Taifa,” anasema kocha Mirambo.

Anasema, ilikuwa mwaka 2013 alikabidhiwa kwa vijana ambao wakati ule walikuwa katika Shule ya Alliance ambao walikuwa kwenye timu ya vijana chini ya miaka 13 (U-13).

“Hatua ni kubwa kwa sababu Serengeti Boys ni timu ambayo inasemwa vizuri katika soka la Tanzania, hiyo ni faraja kwangu na wanangu (timu),” nasema Mirambo.

M irambo anasema katika kipindi chote alichopewa kazi, amefanya jambo ambalo Watanzania wanajivunia kuwa ni timu pekee nchini ambayo katika msimu mmoja wamepata vikombe viwili.

Anasema kuwa pamoja na kucheza mechi mfululizo, imefanya vizuri katika mashindano mbalimbali. Timu hiyo ni bingwa wa Cecafa, michuano iliyofanyika Burundi mwaka jana.

Pia timu hiyo ilishiriki michuano ya Cecafa Afcon iliyofanyika Tanzania na kushika nafasi ya tatu ikifungwa mabao 3-1 na Uganda katika nusu fainali lakini ikailaza Rwanda kwa mikwaju ya penalti.

Serengeti hiyo ilialikwa michuano ya Cosafa U-17, iliyofanyika Botswana na kutwaa ubingwa kabla ya mwanzoni mwa mwezi uliopita kwenda Uturuki kushiriki michuano ya Uefa Assist na ilipoteza mechi mbili na kushinda moja.

Baada ya kurejea nchini, ilikwenda Rwanda kushiriki michuano maalumu ya vijana yakiundwa na timu tatu za Tanzania, Cameroon na Rwanda.

Iliifunga Cameroon 2-1 na kutok sare ya 3-3 na Rwanda na sasa inajiandaa na fainali za vijana.

Mirambo anasema kuwa mechi mbalimali zimeisaidia timu hiyo kuipa uzoefu na anaamini fainali za mwaka huu watafanya vizuri kwa kuwa wamejifunza mbinu kadhaa.

Advertisement