Serikali Kenya kuwazimia simu wasiosajili upya

Serikali ya Kenya imetishia kuzima laini za simu za wananchi wake ambao hawatakuwa wamejisajili kwa mpango wa kidigitali baada ya kumalizika kwa muda uliotengewa.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano nchini humo (CA), Francis Wangusi amesema ifikapo Mei 8, Wakenya ambao hawatakuwa wamejisajili kwa mfumo huo mpya hawataweza kutumia simu za mkononi.

Mpango huo unaoendelea nchini Kenya unafanana na ule unaoandaliwa hapa nchini kuanzia Mei 1, ambapo simu zote zitasajiliwa upya kwa kutumia alama za vidole na namba ya kitambulisho cha Taifa.

Endapo Kenya itachukua hatua hiyo, ina maana mtu hataweza kufikia huduma za kupiga na kupokea simu, kuwasiliana kwa mtandao wa WhatsApp, kutuma na kupokea pesa na kutoa pesa kutoka benki kwa simu, kwa mujibu wa Gazeti la Taifa Leo.

“Tutauliza kampuni za kutoa huduma za mawasiliano ya simu za mkononi kuzima laini (SIM cards) za wale ambao hawatakuwa wamepata Huduma Namba pale muda wa usajili utakapoisha,” Wangusi akasema.

Akaongeza: “Na wale ambao hawatakuwa na laini za simu hawataweza kununua laini mpya ikiwa hawana Huduma Namba.”

Hata hivyo, katika taarifa kwa vyombo vya habari, Mkuu wa Wafanyakazi wa Ikulu, Nzoika Waita alifafanua kuwa Wakenya hawatashurutishwa kujisajili simu kwa Huduma Namba.

Waita alisema hakuna amri yoyote imetolewa na Serikali kuwaadhibu wale wasiojisajili. Badala yake, watahamasishwa kuhusu umuhimu wa kuwa na usajili huo.

Shughuli ya usajili kwa Huduma Namba iliyoanza Aprili 2 na inaendelea kwa siku 45 ilizinduliwa na Rais Uhuru Kenyatta katika Kaunti ya Machakos.