Sheria mpya na hatari ya kurudi chama kimoja cha siasa nchini

Msajili wa vyama vya siasa Jaji Francis  Mutungi

Muktasari:

Wiki iliyopita Muswada huo uliwasilishwa bungeni na kusomwa kwa mara ya kwanza; hata hivyo, wadau wamekosoa muswada huo wakisema kuwa unalenga kuua demokrasia na kurudisha nchi katika mfumo wa chama kimoja.

Wakati Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa ukiwa katika hatua ya kupokea maoni ya wananchi, wadau wa siasa na sheria wameshauri vyama hivyo kutumia muhimili wa mahakama kuipinga sheria itakayotokana na muswada huo.

Wiki iliyopita Muswada huo uliwasilishwa bungeni na kusomwa kwa mara ya kwanza; hata hivyo, wadau wamekosoa muswada huo wakisema kuwa unalenga kuua demokrasia na kurudisha nchi katika mfumo wa chama kimoja.

Awali, chama kikuu cha upinzani, Chadema, kilisema kuwa muswada huo unakosa sifa ya kuitwa wa marekebisho ya sheria na badala yake ulipaswa sheria mpya .

Chama hicho kilifafanua kuwa muswada huo umeleta marekebisho mengi ya zaidi ya vifungu 30, ambayo yanaua msingi wa kutungwa kwa Sheria ya vyama vya Siasa namba 5 ya mwaka 1992.

Pia, chama hicho kilisema Msajili wa Vyama vya Siasa amepewa nguvu kubwa sawa na kuwa mamlaka ya udhibiti.

Lakini swali ni je, nini hatima ya vyama hivyo baada ya muswada huo kupita na kuwa sheria?

Katibu mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji anasema hatima yao haitakuwa njema, na ndio maana wameamua kufanya mambo manne kukabiliana na muswada au sheria itakayotungwa.

Anayataja mambo hayo kuwa ni kupaza sauti kupitia wabunge wao pindi muswada huo utakaposomwa bungeni kwa mara ya pili na kujadiliwa.

“Wanaenda kufuta vyama vya upinzani, msajili amepewa nguvu kubwa, hatutakubali hilo litokee, badala yake tutahakikisha kila Mtanzania anajua ubaya wa sheria hii.”

Hata hivyo, Dk Mashinji anasema suala la wingi wa wabunge wa chama tawala si tatizo kwao na badala yake wanataka umma ujue ukweli.

“Wakati mwingine hata wabunge wa CCM wanapitisha kitu wasichokijua kwa kisingizio cha kutetea itikadi yao, madhara yake wanakuja kuyaona baada ya sheria husika kupita, vivyo hivyo kwa wananchi sasa tumejipanga kuwaonyesha mabaya yote ya sheria hiyo ili waelewe wanapitisha nini na wajue ipo siku zitawageuka,” alisema.

“Wingi wa kura za CCM hautuzuii kusema ukweli, mara nyingi ukweli unashinda hata kama unasemwa na watu wachache. Ukweli ni lazima uwekwe bayana,” alisema.

Jambo jingine watakalolifanya ni kupeleka mapendekezo yao kwa maandishi kwa msajili wa vyama vya siasa.

“Msajili ametuandikia tutoe maoni yetu, hatuwezi kupoteza fursa hiyo tutamuandikia ubaya wa sheria hiyo kifungu kwa kifungu, yapo yanayokiuka Katiba ya nchi, mfano; Muswada unampa mamlaka msajili hata kumfukuza mtu uanachama.”

Anasema chama cha siasa ni taasisi na inasajiliwa kwa mujibu wa sheria, hivyo kumpa mamlaka mtu mmoja kumfuta uanachama mwanachama ni kuvunja Katiba na badala yake angepewa mamlaka ya kulalamika kwa vyombo husika kama Kamati Kuu ya chama husika.

Mashinji anasema iwapo njia zote hizo zikishindikana watakwenda mahakamani kudai haki yao.

“Bunge siyo sehemu ya mwisho, bado tuna imani na mahakama zetu, tunaamini zitatafsiri sheria kwa kuzingatia haki,” anaongeza.

Anasema endapo njia zote zitalegalega watashtaki kwa mahakama ya wananchi ili waamue.

“Tupo kwa ajili ya wananchi, tutazunguka kuwaeleza mapungufu ya sheria hiyo na wao watafanya maamuzi.”

Watetezi wa haki nchini

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga anasema muswada huo umewastua sana kutokana na elimu ya uraia kupelekwa katika ofisi ya msajili wa vyama vya siasa.

“Hii sheria ina mkanganyiko, inasema ili sisi tufanye kazi yatupasa kujisajili katika ofisi za Tume lakini pia tujisajili kwa msajili; sasa hatuelewi nani mwenye mamlaka zaidi ya mwenzie na je, ukishajisajili kwa msajili wa vyama ndiyo umemaliza au,’ alihoji Henga.

Henga anasema sheria hiyo imempa majukumu makubwa mno msajili wa vyama kwani sasa anasimamia, anachunguza na zaidi amepewa kinga, jambo ambalo ni hatari kwa mustakabali wa demokrasia nchini.

“Sasa mambo yote yamewekwa katika chombo kimoja jambo ambalo ni hatari sana na si afya, sheria inatoa faini na kufunga mpaka miaka 20, hiyo ni sawa na kuua vyama na kusema visiwepo kabisa na hivyo kurudi katika mfumo wa chama kimoja,” alisisitiza.

Anasema hata suala la msajili kupewa mamlaka ya kumfukuza mwanachama kama kiongozi wa chama halina mantiki kwa kuwa ni sawa na kusema yeye ndiyo atakuwa kiranja mkuu wa vyama vyote kwa kuwa baadhi ya vyama ni lazima kiongozi awe mwanachama wa chama husika.

Alisema hata kipengele cha chama kuzuiwa kuwa wanaharakati nacho hakina maana kwakuwa lengo la vyama vya siasa ni watu au kikundi cha watu fulani chenye malengo yanayofanana wanaopigania kitu fulani, hivyo huwezi kutofautisha.

Kwa mujibu wa Henga taasisi yake imeamua kuupitia muswada huo kifungu kwa kifungu na hatua zaidi zitachukuliwa ikiwamo ya kwenda mahakamani kuupinga.

Hoja za mwanasheria

Wakili wa kujitegemea, Peter Mshikilwa anaunga mkono hoja ya Dk Mashinji na kusema kwa vyovyote vile hakuna miujiza itakayosababisha muswada huo usipite kwa kuwa wabunge wengi ni wa chama tawala.

Mshikilwa anasema bado vyama vya siasa vina nafasi ya kwenda mahakamani na kupinga vipengele ambavyo wanaona haviwapi haki.

“Haki ya watu kuwa na uhuru wa kujiunga katika vyama vingi ipo kikatiba kwa hiyo wasiogope waende mahakamani kudai haki hiyo.

Kwa mujibu wa wakili Mshikilwa, vyama hivyo vina wigo mpana wa kudai haki hiyo katika Mahakama ya Haki za Binadamu iliyo jijini Arusha.

Hata hivyo, wakili huyo anasema pamoja na haki hizo itawabidi wasubiri mpaka muswada huo utakapopita na kusainiwa kuwa sheria.

“Kwa wenzetu Kenya wanaweza kwenda mahakamani kupinga hatua za awali za muswada wowote mfano tumeshuhudia hivi karibuni wabunge walipinga muswada wa sheria ya kodi ya petroli lakini hapa kwetu hilo haliwezekani; Mahakama haiwezi kuingilia Bunge,” anasisitiza.

Mkurugenzi wa itifaki, mawasiliano na mambo ya nje wa Chadema, John Mrema anasema mbali na muswada kumpa mamlaka makubwa msajili kuwa Mdhibiti wa vyama vya Siasa, umejaa adhabu za kijinai na unafanya shughuli za vyama kuwa jinai wakati ni haki ya kikatiba.

Mrema anasema sheria hiyo ikipita itakuwa kandamizi kwa kuwa inatoa mamlaka kwa msajili wa vyama vya siasa kuingilia mfumo wa uchaguzi wa ndani ya chama, jambo linalokiuka haki ya vyama.

Vilevile, Mrema anawatahadharisha wanachama wa CCM wasibweteke kwa kudhani kwamba muswada huo utawakandamiza wapinzani pekee, badala yake nao wajitayarishe.