Shirikisho la Kikapu Tanzania, chukueni kikokotoleo

Monday October 1 2018

Ligi ya RBA ni kati ya michezo inayoleta

Ligi ya RBA ni kati ya michezo inayoleta amshaamsha ya kikapu Dar es Salaam. 

By Nicasius Agwanda

Usiku wa Agosti 27, 2018, kulikuwa na hafla fupi jijini New York iliyokuwa sehemu ya mikutano ya Umoja wa Mataifa na Marais kadhaa wa Afrika walikuwepo.

Chama cha soka cha mpira wa kikapu Marekani, (NBA) kikachukua fursa hiyo kuandaa mkutano ambao ulihudhuriwa na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, Paul Kagame wa Rwanda, Kamishna wa NBA, Adam Silver, Makamu wa Rais wa NBA na mkurugenzi mtendaji wa NBA Africa, Amadou Galo Fall pamoja na watendaji wengine wa NBA na viongozi wakubwa duniani.

Kwenye agenda kuu, ilikuwa kuanzishwa kwa Ligi Kuu ya kikapu Afrika itakayoitwa Pan African League itakayokuwa chini ya Utendaji wa NBA. Wenzetu wana macho makali, wana fikra pana na wana hisia za ajabu pengine hata wanapenda kutuzidi. Katika bara ambalo lina viwanja vichache, bara lenye uhaba wa miundombinu ya mchezo wa mpira wa kikapu, bara linalokosa viwanja vingi vya ndani bado NBA wanaweza kukaa na kujiuliza namna ya kuanzisha ligi hiyo kubwa.

NBA sio wajinga, wanaishi na kalamu, karatasi na kikotoleo kila siku kwa maana ya kwamba hesabu ni somo rafiki kwao. NBA wametizama kwenye ligi yao, kuna ongezeko kubwa la raia wa Afrika wenye maumbo rafiki kwa mchezo huo wanaoongezeka kila kukicha.

Wakaenda mbali zaidi, wakatizama vyuoni na kwenye shule kadhaa zinazoshiriki michuano ya mpira wa kikapu wakagundua namba kubwa ya raia wa Afrika wanaojaribu kuingia kwenye ligi yao. Ongezeko hili linakua kila kukicha na wala halitokoma kamwe.

Kwao hii ni fursa, wao wanatizama kwa jicho pana la kwamba tangu mara ya kwanza walipoamua kuanzisha NBA Africa kule Afrika Kusini, mara zote kumbi walizochagua zimekuwa zikiuza tiketi zote. Walipoamua kuanzisha mifumo ya kusaidia vijana waliopo mashuleni kupitia JR NBA, mwitikio wa shule nyingi ulikuwa mkubwa na hata walipoamua kuanzisha mpira wa kikapu bila mipaka (basketball without boarders) napo walipata wachezaji bora kama Lucah Mba Moute, Joel Embiid na wengine. Wapo makini wanalitizama bara letu kwa jicho la pekee na jicho la umakini wa biashara.

Mara ya kwanza kusikia neno Pan African NBA League ilikuwa Afrika Kusini kutoka kwenye mdomo wa Adam Silver ambaye ni kamishna wa NBA. Tukiwa kwenye kikao maalumu chenye watu takribani 10, Adam Silver aliuweka huu kama mpango wa muda mrefu akiuita mpango wa miaka kumi. Hata hivyo inawezekana ukawa mpango ambao ukawahi kukamilika haraka zaidi kama wiki tatu baadae wameshaanza kukaa vikao vyenye kusimamia ahadi hizi.

Upande wa pili, fursa kwetu tumezikalia tena kwa “siasa” isiyokuwa sawa. Machozi yananilenga kila nikitizama vijana wa timu ya Taifa ya wachezaji watatu watatu (3x3), ikikosa udhamini na pongezi kwa Karabani ambaye kwa nguvu na misuli yake ameamua kuibeba timu hii mgongoni kwa sababu ndani ya roho yake anaipenda basketball lakini pia anauona mwanga mbeleni.

Ukitizama upande wa pili unaweza kuwapongeza Sprite Bball Kings kwa kujaribu kuleta mpira wa kikapu kwenye picha kubwa. Tatizo pekee lililopo mpaka sasa ni usimamizi ambao umeendelea kukosekana kwa miaka mingi. Sielewi muunganiko uliopo kati ya shirikisho la mpira wa kikapu Tanzania (TBF), wanachama wake na namna inavyojihusisha na wachezaji pia.

Zilichezwa fainali za kimataifa kwa vijana na hakukuwa na udhamini na bakuli la michango lilionekana likitembea katika dakika za mwisho, hali unayojiuliza kuna wasimamizi wa mchezo huu au viongozi?

Inawezekana kabisa kukawa na uchache wa usimamizi au kutokuelewana kwa viongozi baina yao. Wakati nahisi pengine kulikuwa na kuteleza, nikaona ombi la michango kwa ajili ya fainali za Basketball Zone 5, michuano ya kimataifa kwa timu za Afrika Mashariki na Kati zinazofanyika Tanzania.

Imetolewa namba ya kuchangia zikiwa zimebaki siku zisizozidi saba. Namba ya nini? Ili achangiwe nani wakati mashindano yameanza? Ili iweje? Nani afaidike? Ni aibu kuelezea hili kwa sababu mambo yanaendeshwa katika namna ambayo unaweza kuhisi watu walishitukizwa wiki mbili kuandaa mashindano haya wakati yalikuwepo kwenye kalenda ya mwaka mzima.

Inasikitisha kwa sababu siamini tena katika wanaosema mchezo wa mpira wa kikapu hauna wadau kwa sababu viwanja vinajaa kwa michezo iliyopangiliwa na kufanyiwa promosheni vyema.

Nikitizama Rais wa shirikisho akiwa msemaji, nawaza nafasi za viongozi wengine pia na ndio ninapopata shaka la utendaji wa shirikisho kwa ujumla. Kuna siku kaka yangu mwenye uchungu na mchezo huu Rueben Ndege, ‘Ncha Kali’ aliwahi kuniuliza nia yangu ya msingi katika kutoa nafasi ya watendaji hawa kuomba michango katika siku ya mwisho ya maandalizi kabla ya michezo ya vijana kupitia kipindi cha redio “Sports Xtra.” Itoshe kusema tu kuwa nilikosea na nakiri kuwa nilikuwa sehemu ya kuendeleza uzembe unaowekwa kwenye kusimamia mchezo huu pendwa.

Shirikisho limejaa uzembe, haliendi na wakati na halifahamu kwa ujumla wake namna ya kuweka misingi inayoweza kujisimamia bila hata kutaja majina ya viongozi. Ni lini wachezaji wataanza kulipwa vyema, vilabu kujitegemea kimapato, ligi kuwa na picha nzuri inayoweza kudhaminiwa ni maswali ya msingi ambayo wanatakiwa kuanza kuyafikiria kabla ya kuwaza propaganda za kuleta kwenye uchaguzi ujao wa viongozi.

Bahati nzuri viongozi wote nawafahamu, na ninahisi mambo hayapo sawa kati yao na hawashirikiani inavyopasa kuwa. Naomba muungane, mshirikiane na tuendeleze mchezo huu. Kama NBA wanawaza kuanzisha ligi kwenye bara ambalo wanafahamu fika michezo yao haitizamwi kwa kiwango kikubwa kutokana na changamoto ya muda, inakuwaje sisi tushindwe kushika kikokotoleo na kupiga hesabu zenye kutuonyesha maendeleo yanayoweza kuja?

TBF shikeni kikokotoleo, tazameni wakati ujao, sikilizeni vilio vya wanaopenda mchezo huu, chukueni kalamu na karatasi na muandike maoni, kisha kuweni wabunifu katika kusimamia mambo. Baada ya miaka mitano NBA wataanzisha ligi yao Afrika, na mtaenda kuhudhuria na kutueleza mambo mazuri yanakuja wakati Watanzania hawanufaiki. Umefika wakati wa nyie kuungana na kutumia kikokotoleo vyema kupata hesabu tunazohitaji hili kupiga hatua. Acheni ujanja.

Advertisement