HOJA ZA KARUGENDO: Siasa na uaminifu: Tunahitaji mifumo la sivyo ngoma nzito

Watanzania wengi wamekulia katika mazingira ya udanganyifu, rushwa na uzembe. Katika awamu zilizopita, hasa ya tatu na nne, tabia hizi zilijioyesha wazi na kufumbiwa macho. Awamu ya tano inakazana kupambana na ugonjwa huu, lakini hakuna mfumo wa kurekebisha kasoro hizi.

Watu wachache wanafanya kazi kwa uaminifu na kwa bidii kubwa, lakini asilimia kubwa ni udanganyifu, rushwa na uzembe. Ni kutaka miujiza isiyowezekana watu hawa kuibuka na uaminifu. Mitihani inanunuliwa, vyeti vinanunuliwa na watu wanapata mafanikio ya haraka maishani (wanajenga majumba, wananunua magari, wanakuwa viongozi wa juu serikalini, wanakuwa na viwanda, pesa hadi mabilioni) bila kusoma wala cheti na wakati mwingine bila hata kumaliza sekondari.

Hata hivyo, uaminifu ni neno pana na linazua maswali kuliko majibu. Mtu mwenye uchokozi anaweza kutoa maoni kwamba hata majambazi wana uaminifu mkubwa miongoni mwao.

Jambazi akikamatwa, anakubali kuteswa na wakati mwingine kupoteza maisha bila kuwataja wengine. Huu ni uaminifu wa kiwango cha juu.

Mtu anayechota pesa za serikali ili kuwasomesha watoto wake, jamaa zake na kuleta maendeleo katika wilaya yake, anakuwa anakoswa uaminifu serikalini, lakini ni mwaminifu kwa familia yake na kabila lake. Au mtu akichota pesa za serikali kuendeleza chama chake cha siasa, anakuwa anakosa uaminifu katika serikali, lakini ni mwaminifu katika chama.

Uaminifu unahitaji malengo, kipimo na uwajibikaji. Ni lazima mtu ajiulize ni kwa nini anatakiwa kuwa mwaminifu, na kwa nani? Kwa familia yake, kwa kabila lake, kwa dini yake au kwa taifa lake, na je ni kipimo gani kitatumika kuupima uaminifu wake.

Ni lazima uwepo mfumo wa kumsaidia mtu kutekeleza malengo, kukumbushwa malengo na kupimwa mara kwa mara. Mtu akiachwa peke yake ni lazima atangulize uaminifu unaolenga kumletea manufaa binafsi.

Hivyo ni muhimu kuwa na mfumo na wawezeshaji wa kuelekeza na kusisitiza umuhimu wa uaminifu. Na la msingi hapa ni uaminifu kwa taifa, uaminifu kwa uhai na uaminifu kwa ubinadamu. Na hili si suala la kufanyia siasa, ni la kufa na kupona kwa taifa lolote ili liweze kustawi.

Mtu, akipora pesa za serikali, akajenga hekalu watu wanamshangilia. Anaonekana kama shujaa. Mazingira kama haya hayawezi kujenga uaminifu. Wazee waliofanya kazi enzi za Mwalimu Nyerere, wengi wao, maisha yao si mazuri sana. Hawakupora, na wengi wao hawakuweza kujenga mahekalu. Tunawacheka. Utasikia Waswahili wa mjini wakisema “Walijisahau”.

Hali ilivyo sasa hivi, mtu anaweza kujiuliza uaminifu maana yake nini? Na je, ni kwa nini mtu awe mwaminifu? Anaogopa nini? Anawajibika kwa nani? Kipimo cha uaminifu wake nini? Je uaminifu ni wa wote au kuna baadhi ambao lazima wawe waaminifu, ni wa maskini tu au na matajiri?Tunahitaji msingi imara wa uaminifu; kwenye familia zetu, kwenye jamii zinazotuzunguka, kwenye taasisi zetu, kwenye taifa. Hili likishindikana, ni wajibu wetu sote kuwaondoa wanasiasa wasiofanya hivyo na kutafuta kitu kingine cha kutuongoza kuelekea kuimarisha uaminifu wetu kwa taifa letu.