SIASA ZA KITAA: Siasa za njaa ni bora kuliko siasa za shibe

Muktasari:

  • Lowassa wa CCM na wa Chadema ni watu wawili tofauti. Yule wa CCM mbele ya wana Chadema, alikuwa fisadi aliyejilimbikizia mali nyingi za umma. Huyu wa sasa mbele ya wana Chadema katakaswa. Nywele nyeupe, roho nyeupe na njia nyeupe. Msafi kama vazi la kasisi.

Ndiyo, siasa inahitaji unafiki ili ufike unapotaka. Mwanasiasa bora ni yule anayejitoa ufahamu kidogo. Huko ndipo neno duniani wawiliwawili linamaanisha. Watu huweka kando elimu zao na kuazima akili mpya wanakojua wao ili kufanyia shughuli za kisiasa. Utadhani siasa ni jambo la kipuuzi.

Lowassa wa CCM na wa Chadema ni watu wawili tofauti. Yule wa CCM mbele ya wana Chadema, alikuwa fisadi aliyejilimbikizia mali nyingi za umma. Huyu wa sasa mbele ya wana Chadema katakaswa. Nywele nyeupe, roho nyeupe na njia nyeupe. Msafi kama vazi la kasisi.

Kikwete wa Ikulu tofauti na Msoga. Wa Ikulu alifuja fedha kwa safari, kujuana kwingi, dhaifu kwenye maamuzi. Alilea ufisadi. Baraza kubwa la mawaziri. Huyu wa Msoga mtu safi, muungwana, aliruhusu demokrasia. Safari zilikuwa na tija. Aliajiri watumishi kila mwaka, alikubali kukosolewa na kualika wapinzani Ikulu.

Ndivyo ilivyokuwa kwa Mzee Mkapa na Mzee Mwinyi. Hizi ni hulka za wanasiasa na mitazamo ya watu kwa viongozi wao. Wanasiasa wanapokula hubadilika kabisa kimtazamo. Na wananchi nao wanampenda zaidi mtu akistaafu kiasi cha kufanya ionekane ni watu wawili tofauti.

Profesa Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi. Amepelekwa eneo sahihi la uwaziri wa Sheria na Katiba. Tatizo Kabudi huyu ni tofauti na yule wa awali. Kabudi yule alibaki kwenye makabrasha ya Rasimu ya Katiba Mpya ya Warioba. Tena wana tofauti kubwa sana kimtazamo na Kabudi wa sasa.

Polepole huyu si yule kijana machachati kwenye Rasimu ya Katiba Mpya ya Warioba. Ni watu wawili tofauti sana. Wanafanana sura, rangi, umbile na sauti. Lakini anachotoa kinywani leo tofauti kabisa na alichotoa jana. Hapa ndipo maana ya duniani watu wawiliwawili inajitokeza wazi kupitia yeye.

Namkubali sana Polepole. Ni dogo timamu ukimsikiliza. Kosa lake ni kukubali ukuu wa wilaya na hatimaye kupewa uenezi wa chama. Wajanja zaidi yake walimpatia nafasi kumdhibiti na misimamo yake iliyokuwa tofauti na chama chake. Siasa ni sayansi na hesabu. Polepole ‘kwishnei’.

Magufuli unayemuona leo akiwa Ikulu ya Magogoni. Usitegemee kumuona katika mtazamo huu akiondoka pale Ikulu. Haijalishi unamtazamo gani juu yake hivi sasa. Pindi akistaafu kitazaliwa kiumbe kingine tofauti na huyu. Ndivyo ilivyo mitazamo yetu kukithamini zaidi kilichopita.