Simba SC ilipokumbusha kipigo cha USM El Harrach

Monday January 14 2019

 

Unaikumbuka Simba ya fainali ya Kombe la CAF 1993? Iliingia fainali lakini ikapoteza kwa mabao 2-0 ya Boli Zozo wa Stella Abidjan kwenye Uwanja wa Taifa mbele ya Rais Ali Hassan Mwinyi.

Simba iliingia fainali ile lakini humo ilimopita, ilikutana na timu moja ya Algeria, inaitwa USM El Harrach. Mchezo wa kwanza uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa Simba ilishinda mabao 3-0 na marudiano ikafungwa 2-0, Simba ikasonga mbele kwa mabao 3-2.

Kuonyesha kuwa Simba haitishiki na timu za Algeria, iliitoa ES Setif ya huko mwaka 2012, iliifunga mabao 2-0 mechi ya kwanza Kombe la Shirikisho kabla ya kufungwa 3-1 nchini Algeria na Simba kusonga mbele kwa faida ya bao la ugenini kwa matokeo kuwa 3-3.

Picha iliyopo, Simba hujipigia tu timu za Waarabu hasa Algeria kwani imewahi kuzitoa mara mbili na safari hii JS Soura ya huko imelala 3-0, Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mabao ya Meddie Kagere aliyefunga mawili na Emmanuel Okwi bao moja.

Matokeo hayo ya mwishoni mwa wiki yanaifanya Simba kuongoza Kundi D ikiwa na pointi tatu ikifuatiwa na Al Ahly ya Misri yenye pointi tatu baada ya kuishinda AS Vita ya DR Congo mabao 2-0 mjini Cairo.

Vita inashika nafasi ya tatu wakati JS Saoura iko nafasi ya nne.

Wakati AS Vita ikilala, ndugu zao wa TP Mazembe wameanza kwa kishindo Kundi C kwa kuwalaza Ismaili ya Misri mabao 2-0.

Mpambano mwingine wa Kundi B, mabingwa wa Zimbabwe, Platinum Stars ilitoka suluhu na Orlando Pirates katika mchezo uliokuwa mkali na kusisimua wakati mechi nyingine ya kundi hilo, Esperance ya Tunisia na Horoya AC ya Guinea zilitoka sare ya 1-1.

Ushindi wa Mazembe huko Lubumbashi ulipatikana licha ya kucheza pungufu baada ya kipa wao raia wa Ivory Coast, Sylvain Gbohouo kulimwa kadi nyekundu baada ya kumchezea vibaya Benson Chilongo na kipa wa akiba Aime Bakula alifanya kweli ikiwemo kuokoa penalti.

Ushindi wa Mazembe umeifanya timu hiyo kukwea kileleni ikifuatiwa na CS Constantine, iliyoifunga Club Africain bao 1-0 mechi ya Ijumaa.

Mechi zijazo za Ligi ya Mabingwa zimepangwa kucheza kati ya Januari 18 na 19. Kwa mechi za Kundi D, Simba itakwenda DR Congo kucheza na AS Vita iliyojeruhiwa na Al Ahly itakwenda Algiers, Algeria kuifuata JS Saoura iliyoadhibiwa na Simba.

Advertisement