Simba ilivyoendeleza ubabe kwa Yanga

Simba imeibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Yanga na kupeleka kilio katika upande wa mashabiki wanaotokea Mitaa ya Twiga na Jangwani.

Simba sasa imefikisha pointi 39 japo Yanga inaongoza kwa pointi zake 58.

Makala hii inaelezea namna ambavyo mchezo huo ulivyokuwa na kugusia pande zote mbili za timu hizo jinsi walivyocheza kwa dakika zote.

MAKAMBO ATULIZWA

Kwenye mechi hii kocha Mwinyi Zahera alimuamini mshambuliaji wake, Herieter Makambo, lakini kumchezesha yeye kama yeye kwa namna moja ama nyingine kuliifanya Yanga wasishambulie.

Mabeki wa Simba, Pascal Wawa na Juuko Murshid hawakuwa na kazi ngumu ya kuwazuia Yanga, kwa sababu mipira waliyokuwa wakipigiwa na kutua kwa Makambo hata akiituliza ilikuwa inapotea.

Tambwe ambaye alikuwa akisimama na Makambo, alipotea kabisa katika mchezo huo kiasi cha kocha Mwinyi Zahera kumtoa na nafasi yake kuingia Mrisho Ngassa.

Mabadiliko ya Mrisho Ngassa yalionekana kuwa na tija kwa sababu Ngassa alizidisha presha ktaika eneo la ushambuliaji lakini umakini kwa Makambo pamoja na ulinzi aliowekewa hakuweza kuifungia timu yake.

CHAMA, AJIB WAPOTEA

Wengi walitarajia kuona nyota wa vikosi hivyo vyote viwili wakitawala mchezo, lakini hali haikuwa hivyo.

Kiungo wa Simba, Clatous Chama ni miongoni mwa wachezaji ambao walikuwa wakisubiriwa kuonyesha ufundi wao, lakini walipotea.

Chama alikuwa chini ya ulinzi mkali wa Abdallah Shaibu ‘Ninja’ ambaye alikuwa akitembea nae bega kwa bega , hatua kwa hatua muda wote uwanjani.

Hata hivyo, kocha Patrick Aussems baada ya kuona hali hiyo, aliamua kumtoa dakika 45 na nafasi yake ilichukuliwa na Hassan Dilunga ambaye aliingia na kuongeza nguvu katika eneo hilo la kiungo.

Kwa upande wa Yanga, Ibrahim Ajib hakuweza kabisa kucheza soka la kuvutia kama ambavyo ilitarajiwa, mara kwa mara kocha Mwinyi Zahera alikuwa akionekana kumuelekeza lakini bado alikuwa haonyeshi kuelekea.

Zahera aliamua kumtoa na kumuingiza Mohammed Issa ‘Banka’ ambaye licha ya kuingia bado alishindwa kuonyesha makeke yake.

Hii ni kawaida kwa nyota wengi kushindwa kuonekana katika mechi kama hizi zilizojaa presha.

‘BOXER’ ANG’ARA

Beki huyu chipukizi kabisa katika kikosi cha Yanga, amezidi kuonyesha ukomavu katika eneo la Ulinzi baada ya kuweza kuzuia mashambulizi kadhaa katika mchezo huo.

Godfrey alikuwa akitumika kama mchezaji ambaye anapeleka mashambulizi katika lango la Simba, kwa upande huo aliweza kutimiza wajibu wake vizuri.

Kupanda kwake kwa spidi kulikuwa kunamfanya beki wa Simba, Mohammed Hussein ashindwe kabisa kupanda mbele kama alivyozoeleka kwasababu kama angekuwa anapanda angemfanya Paul kusababisha bao lolote kutokana na spidi yake aliyokuwa anaionyesha katika mchezo huo.

Emmanuel Okwi nae alikuwa katika wakati mgumu dhidi ya beki huyo kwasababu kila alipokuwa anapiga hatua basi dogo huyo alikuwa akifika na kumtuliza.

Mashabiki walijikuta wakifurahishwa na kiwango ambacho alikionyesha dogo huyo ndani ya dakika zote 90 alizokuwa amecheza.

VIUNGO WAKITIFUA

Katika mechi hii eneo la kiungo ndio lilikuwa likivutia zaidi kutokana na kwamba timu zote mbili zilikuwa zimejaza viungo ili waweze kucheza kwa ustadi wa hali ya juu.

Katika kikosi cha Yanga walianza viungo Feisal Salum, Abdallah Shaibu na Papy Tshishimbi, huku Simba walianza James Kotei, Jonas Mkude na Clatous Chama.

Viungo wa Simba walitawala mpira kwa dakika 45 huku Yanga wakikaba zaidi, lakini beki Abdallah Shaibu alionekana kukaba zaidi na kuwafanya viungo hao wapunguze spidi katika kushambulia.

Timu zote mbili ziliamua kufanya mabadiliko katika eneo hilo la kiungo, ambapo Simba aliingia Dilunga akichukua nafasi ya Chama, wakati kwa Upande wa Yanga aliingia Mo Banka akichukua nafasi ya Ibrahim Ajib.

Mabadiliko hayo yalionekana kuwa na tija zaidi kwa upande wa Simba baada ya Dilunga kusambaza zaidi mipira katika eneo hilo la katikati ya uwanja.

ZANA MTAJI SIMBA

Licha ya mashabiki kuwa na shaka kwa beki Zana Coulibaly, katika mchezo huu ni kama nyota wa mchezo kutokana na aina ya soka alilokuwa anacheza.

Zana alikuwa akitumika kupeleka mashambulizi kwa upande wa Simba, huku spidi yake ikionekana kabisa kumnyima usingizi Gadiel Michael kupanda na kupiga krosi kama ambavyo amezoeleka.

Kadri siku zikiwa zinaenda mbele, beki huyu asiyeishiwa vituko ameonekana kuuzoea mfumo wa Simba, hivyo kama akipewa muda zaidi anaweza kuja kuwa msaada kikosini.

YANGA WALIKOSEA HAPA

Kitendo cha Mwinyi Zahera kumuanzisha Herieter Makambo katika eneo la ushambuliaji, kuliwanyima ushindi wa mapema Yanga ambao walikuwa wanashambulia kwa kushtukiza.

Yanga walianza kutumia zaidi mipira ya krosi katika kushambulia, hata hivyo umakini wa Pascal Wawa na Juuko Murshid kulimtuliza Makambo ambaye alionekana kutaka kufurukuta.

Hata hivyo Makambo alionyesha ukomavu kwasababu licha ya kwamba alikuwa amesimamishwa yeye pekee katika eneo la ushambuliaji, bado alitumia nguvu zaidi katika kupenya lakini haikuwa na maana kutokana na kupambana na watu wawili.

KABWILI AWEKA REKODI

Baada ya kipa Beno Kakolanya kugoma kurejea katika kikosi hiko, moja kwa moja Yanga walielekezea nguvu zao zote kwa kipa Ramadhan Kabwili.

Kweli na ikawa hivyo dogo huyo kupewa nafasi ya kuonyesha katika mchezo huo, ikiwa ndio kwanza mara yake ya kwanza kucheza pambano hilo.

Tayari ameshaweka rekodi ya kupata nafasi ya kucheza mechi hiyo kubwa na kufungwa, kwani huu ndio mchezo wake wa kwanza mkubwa kucheza akiwa na kikosi hiko cha Yanga.

KOTEI KAZI KAZI

Katika nafasi ya ukabaji wa kikosi cha Simba hivi sasa kuna muhimili mkubwa katika kuhakikisha viungo wa wapinzani hawawezi kabisa kucheza.

Nyuma yao kuna jina moja tu la Mghana, James Kotei ambaye amekuwa na msaada mkubwa katika kuhakikisha anakaba na sio kuwa na kazi nyingine yoyote .

Kotei ni kama ana mapafu ya mbwa kutokana na uwezo wake wa kukaba na kuzunguka muda wote ambao anakuwa yupo uwanjani na hali hiyo imewafanya viungo wa timu pinzani kushindwa kabisa kucheza.

Simba bado wanamuhitaji zaidi Kotei kwa msimu ujao, hivyo watakuwa na kazi ya ziada kuhangaika na kuhakikisha mchezaji huyo anabaki.