Snura na Minu Mwaka huu ndoa lazima

Saturday January 19 2019

 

By Nasra Abdallah, Mwananchi [email protected]

Snuminu ndio kifupi cha majina ya wapendanao Snura na Minu Calypto. Ni wanamuziki wapenzi wanaofuatiliwa zaidi katika maisha ya uhusiano pengine kuliko kazi zao za sanaa kwa sasa.

Wimbo wao mpya Shoko walioshirikiana unafuatiliwa huku mashabiki wakisubiri kwa hamu kuona watakavyoinogesha video yake.

Snura Mushi aliyejipatia umaarufu kwa nyimbo zenye uchezaji wa kipekee, amekuwa kwenye uhusiano na Minu ambaye jina lake halisi ni Minhal Azad kwa zaidi ya mwaka mmoja.

Uhusiano wao unafuatiliwa kwa ukaribu na gumzo likiwa kigezo cha umri kwamba mwanamke amemzidi umri mwanamume.

Mwananchi ilifanya mahojiano nao kujua mapenzi yao yalipoanzia na nini matarajio yao katika muziki hasa kama ndoa inakaribia.

Walivyokutana

Minu anasema kwa mara ya kwanza alikutana na Snura katika studio ya mwanamuziki Christian Bela, maeneo ya Sinza ambako naye alifika mahali hapo kama msanii wake.

Anasema kwa muda mrefu amekuwa akifanya kazi za kumtungia nyimbo msanii huyo ambaye pia nafanya kazi bendi ya Malaika na kati ya alizomtungia ni pamoja na ‘Punguza Kidogo’ ‘Rudi’ aliyoimba na Joh Makini, ‘Niende Wapi’ huku nyimbo nyingine wakiwa wanasaidiana mawazo.

Wakati akiwa katika studio hiyo siku moja alimuona Snura akiwa amekwenda hapo kwa ajili ya kurekodi wimbo wa ‘Zungusha’.

Baada ya kumuona alipenda namna anavyofanya kazi na kutaka kumpa wimbo kwa kumuona inamfaa, ambapo anadai mpenzi wake wa zamani ndiye alimuunganisha naye kwa kumpa namba na kuanzia hapo wakawa wanawasiliana.

“Kama unavyojua mapenzi hayachagui pa kuchepua, na hivyo ndivyo ilivyokuwa kati yangu na Snura kwani kadri tulivyozidi kuwa naye tukajikuta na mapenzi yanaingia na Desemba mwaka juzi ndipo tulipoanza rasmi kuwa wapenzi,” anasema.

Matarajio katika mahusiano yao

Minu anasema matarajio yake kwa Snura ni kuwa mama wa watoto wake na angependa wa kwanza kumzalia awe wa kike ili amuite jina la mama yake Aisha.

Wakati kuhusu ndoa anasema Mungu akipenda mwaka huu atamuoa kwani ni mwanamke ambaye anampenda na siyo kwamba kaenda kwake kwa lengo la kupata umaarufu.

Anasema moja ya kitu kinachomvutia kwa Snura mbali na kujituma katika kutafuta maisha, ni pamoja na mashavu yake na ameshamueleza kuwa akijikondesha ahakikishe mashavu yanabaki.

Snura afunguka

Snura anasema anasikia furaha kufanya kazi na mpenzi wake huyo ambaye tayari wameachia wimbo wa Shoko.

Hata hivyo, anasema hafikiri kama ni mtu ambaye ameenda kumtumia ili atoke kimuziki kama ambavyo watu wamekuwa wakisema.

“Haya mambo ya kudanganywa katika mapenzi yapo kwa kila mtu, hivyo siwezi kulizungumzia sana labda yupo kwangu kwa ajili ya jambo fulani, isipokuwa mimi najipa imani kwamba yupo nami kimapenzi na kama ananidanganya itakuwa ni yeye,” anasema Snura.

Wakati kuhusu suala la umri anasema awali alikuwa hataki kusikia kuwa na mwanaume ambaye ni mdogo kiumri, kwani alidhani kuwa atakuwa msumbufu kwake na kuwa na akili za kitoto lakini ndio hivyo Mwenyezi Mungu baadaye kaja kumuonyesha kuwa mapenzi hayachagui umri.

Kuhusu Minu

Minu Calypto’ ambaye alizaliwa miaka ya 1990, anasema ilikuwa mwaka 2012 alipokwenda kutafuta maisha Jijini Dar es Salaam, akitokea Tanga.

Akiwa huko anasema alisomea mambo ya usanifu kurasa lakini kwa bahati mbaya hakupata kazi na mwaka 2014 kujikuta anaangukia katika kazi ya kubeba mizigo inayosambazwa katika supermarket za TSN.

Huko alifanya kazi kwa mwaka mmoja na miezi tisa na kuamua kuacha kwa sababu ambazo hakuwa tayari kuziweka wazi.

Anaeleza kuwa baada ya kupata mafao yake, aliamua kununua mashine za kutengeneza popcorn tatu na hivyo kujikusanyia hela.

Wakati huu alikuwa akipata muda wa kwenda kufanya kazi ya muziki kwa kuwa kwenye mashine aliweka watu.

Pia zilimsaidia kupata fedha ya kuingia studio na kutengeneza nyimbo ya kwanza ilikuwa ni Leo Hanitaki japokuwa haikufanya vizuri kwa kuwa hakuwa anawajua watu wa kuweza kumtangaza.

Mwaka 2016 alipata nafasi ya kurekodi studio za Wasafi wimbo ‘Bado Nachechema’ ambayo aliuachia mwaka jana.

Advertisement