Sumaye ana siri nzito kuhusu kurejea CCM

Waziri Mkuu aliyehudumia nchi kwa kipindi kirefu zaidi, Frederick Sumaye, amesema kurudi CCM ni ndoto. Amesema hakuna tatizo lolote kwa aliyerithi cheo chake mwaka 2005, Edward Lowassa, kurejea chama hicho kinachoongoza dola.

Sumaye na Lowassa wote walihamia Chadema kutoka CCM katika joto la Uchaguzi Mkuu 2015. Alianza Lowassa Julai 28, 2015 kisha bila kutarajiwa, Sumaye naye alihamia vuguvugu la mageuzi Agosti 22, 2015 bila kutaja chama alichojiunga nacho.

Kipindi ambacho vyama vya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Chadema, NCCR-Mageuzi, NLD na Cuf, vilitumia jukwaa moja la kisiasa, wakisimamisha mgombea mmoja wa urais, vilevile kushirikiana katika wabunge na madiwani, Lowassa akiwa ndiye mgombea urais, Sumaye akajiunga na Ukawa.

Safari ya Sumaye kurejea au kutorejea CCM inaundwa na siri nyuma ya uamuzi wake wa kuondoka CCM mwaka 2015 kujiunga na Ukawa kabla ya kuchukua kadi ya Chadema, kisha kuomba na kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa chama hicho Kanda ya Pwani.

Sumaye alikuwa na sababu gani ya kuhama CCM mwaka 2015? Jawabu la swali hilo ndilo lenye siri nzito kuhusu kile ambacho kinaweza kumrejesha CCM. Alipopanda jukwaa la Ukawa mwaka 2015, Sumaye alitoa sababu nyepesi mno kuwa alitaka kuwasaidia wapinzani kuongoza nchi baada ya kushinda uchaguzi. Akasema pia kwamba hakuwa akipewa uzito wa mawazo yake kwenye nchi na chama.

Mshangao ulikuwa mkubwa hata kwa viongozi CCM pale Sumaye alipogeuka meneja kampeni wa Lowassa na kuzunguka naye mikoani na wilayani kumwombea kura. Wakati Sumaye na Lowassa walikuwa na historia ya kutoiva chungu kimoja wakiwa CCM.

Historia hiyo ya kutoiva chungu kimoja ndiyo ambayo inaongeza simenti ya ujenzi wa siri nzito ya Sumaye alipoondoka CCM na kama iwapo atarejea. Mwenyewe husema amekuwa akishawishiwa sana kurejea CCM lakini hatafanya hivyo.

Ukitafakari kwa kina uamuzi wa Sumaye kuondoka CCM utabaini kuwa kuna kitu kikubwa kilimuondoa. Pengine siku kitu hicho kikipatiwa ufumbuzi ndipo naye atarejea. Na kwa vile hajawa tayari kukisema hadharani, vilevile wenye kujua wasivyotaka kumsemea, basi inabaki kuwa siri ndani yake.

Ni siri kwa sababu Sumaye kabla ya kuondoka CCM alipata kuahidi kuwa Lowassa angepitishwa kuwa mgombea urais wa chama hicho angehama. Japo Sumaye hakutaja jina la Lowassa moja kwa moja, lakini haikuwa ikihitaji kanuni ya kufungua mabano kumjua aliyemlenga.

Zaidi, baada ya Sumaye kuhama CCM, aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Jakaya Kikwete, katika kampeni za Uchaguzi Mkuu 2015, alisema hakuelewa sababu ya kiongozi huyo mstaafu kuhama. Alisema alijaribu kumsikiliza hakumwelewa. Akagusia kwamba ombi lake lilikuwa Lowassa asiwe mgombea urais, lakini baada ya ombi hilo kupita, akamfuata Lowassa Ukawa.

Nilifanya mahojiano na aliyepata kuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais, John Malecela, aliyesema kuwa Sumaye alimfuata mara nyingi na kumwambia kwamba Lowassa angepitishwa na chama kuwa mgombea urais angehama. Niliandika makala kuhusu mahojiano hayo.

Kwa mantiki hiyo hata baada ya Lowassa kurudi CCM si ishara kwa Sumaye kwamba naye yupo njiani. Baada ya Kikwete kupitishwa kuwa mgombea urais wa CCM mwaka 2005, Sumaye alitangaza kutogombea ubunge Hanang na kujiweka pembeni na siasa. Mwaka 2012 alijitokeza kuwania ujumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) CCM lakini akashindwa na mrithi wake wa ubunge Hanang, Mary Nagu.

Baada ya Sumaye kushindwa na Nagu, alipaza sauti kuhusu kuchezewa rafu. Mnyukano wa kuwania tiketi ya CCM ya kuwa mgombea urais mwaka 2015 ulitajwa kuhusika. Mwisho kabisa, lawama za Sumaye kuhusu rafu alizolalamikia, moja kwa moja Lowassa ndiye alitajwa kuwa mcheza.

Hata hivyo mpaka hapo Sumaye atakapoamua kusema wazi, hii ni siri inayoishi. Lowassa alihama kutafuta fursa ya kugombea urais. Sumaye alihama kwa sababu gani? Vinginevyo, Sumaye ni wa upinzani kwa muda mrefu ujao.