TULONGE KILIMO : Namna ya kuzalisha viazi vitamu kibiashara

Saturday January 26 2019

 

By Elias Msuya

Viazi vitamu vimekuwa vikilimwa nchini kwa muda mrefu hasa katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Dodoma, Morogoro, Kagera, Arusha na Ruvuma.

Viazi huhifadhiwa kwa kukatwa vipande vidogo vidogo (michembe) ambavyo hukaushwa. Unga wake hutumika kutengenezea vitafunwa kama keki, maandazi kalimati na tambi. Vilevile unga huo hutengenezewa juisi, huku majani yake yakitumika kwa mboga (matembele).

Viazi vina thamani kubwa kwa lishe, licha ya kuwa na wanga kwa wingi na kambalishe, wataalamu wameviongezea virutubisho (fortification) ambavyo ni pamoja na vitamin, kalishiumu asilimia 25-50, potasiam asilimia 5-7, chuma, protini, kalori, fosforus asilimia 1.5-2.

Hata hivyo, kutokana na kutotumia na kutozingatiwa kwa kanuni za kilimo bora, uzalishaji wake uko chini kwa kuwa wakulima wengi hupata wastani wa mavuno kwa mkulima ni tani nane hadi 10 vikiwa vibichi. Wataalamu wa kilimo wanakadiria kupatikana kwa kati ya tani 20 hadi 35 za viazi vitamu katika eka moja kama kanuni za kilimo bora zitazingatiwa.

Namna ya kulima kibiashara

Wataalamu wanashauri mkulima achague eneo lenye ardhi tifutifu inayopitisha maji kwa urahisi, mvua za wastani na joto la kadri na hali ya unyevunyevu. Eneo hilo litakuwa na uoto uliostawi kwa wingi kutokana na rutuba na eneo lenye mwinuko wa ardhi. Hali hiyo husaidia viazi kustawi vizuri; uoto mwingi hufunika ardhi isikauke.

Eneo la kulima viazi litayarishwe kwa kufyeka na kung’oa visiki ili kuwezesha mizizi kupenya ardhini kwa urahisi. Eneo hilo halipaswi kuwa karibu na mwamba kwa kuwa litasababisha mizizi ya viazi ishindwe kupenya ardhini na kutoa viazi.

Ili kuongeza utifutifu wa ardhi, mkulima anashauriwa kulima matuta yatakayopandwa malando. Hata hivyo, utifuaji wa udongo haupaswi kuwa mkubwa kwenye udongo wa kichanga, kwa kuwa utakausha ardhi kwa urahisi.

Baada ya utayarishaji wa shamba kukamilika, mkulima anapaswa kuchagua mbegu ya kupanda. Inashauriwa kupanda malando yenye urefu wa kati ya sentimita 15 hadi 30. Mbegu hizo huwa na vifundo kati ya vitano hadi vinane na hivyo ndivyo ndivyo vyanzo vya machipukizi na mizizi.

Mbegu yenye vifundo vichache hukua kwa tabu na hata zikikua hazitakuwa na mazao mengi.

Mkulima aangalie mbegu ambazo hazijashambuliwa na wadudu ili kuepuka magonjwa. Ili kupata faida ya lishe ya viazi, mkulima anashauriwa kutumia mbegu zilizorutubishwa.

Advertisement