TULONGE KILIMO : Uzalishaji bora wa zao la muhogo- 3

Muktasari:

Kwanza kuna wadudu wanaoitwa vidung’ata ambao huonekana kufunikwa na vitu laini vyeupe na majani huonekana kujikusanya nchani.

Tunaendelea na sehemu ya tatu ya uzalishaji wa muhogo. Wiki iliyopita tuliona baadhi ya magonjwa yanayolisumbua zao hilo, leo tutaona wadudu hatarishi kwa muhogo.

Kwanza kuna wadudu wanaoitwa vidung’ata ambao huonekana kufunikwa na vitu laini vyeupe na majani huonekana kujikusanya nchani.

Madhara yake ni kuharibu majani na shina la muhogo kiasi cha kuudhoofisha mmea.

Mdudu mwingine ni tandabui wa kijani ambaye husababisha kupotea kwa majani kuanzia nchani (candle stick).

Mwingine ni inzi mweupe. Huyu hufyonza majimaji ya mimea ya muhogo. Hawaishii hapo bali pia hueneza magonjwa ya virusi vya ugonjwa wa batobato.

Mdudu mwingine ni panzi kunuka ambao mara nyingi hujitokeza wakati wa kiangazi au wakati wa uhaba wa mvua. Hushambulia majani ya mmea na kuufanya ushindwe kuzalisha chakula.

Mkulima anashauriwa kuhakikisha idadi yao haiongezeki kwa kuharibu mazalia yao. Mashamba yanatakiwa kutayarishwa mapema ili kuharibu maeneo wanayotagia mayai.

Mwingine ni mdudu gamba (cassava scale) ambaye hushambulia shina la muhogo na kufyonza majimaji hadi mmea na kuufanya uwe dhaifu.

Wataalamu wanashauri kuongeza rutuba katika zao la muhogo kwani zao hilo hufyonza rutuba nyingi toka ardhini.

Hata hivyo, inategemea rutuba iliyopo kwenye ardhi. Kama ni shamba jipya basi litakuwa na rutuba, lakini kama limelimwa kwa muda mrefu, ni lazima kutumia mbolea ama za viwandani au mboji.

Watalaamu wanatahadharisha matumizi ya mbolea kwani unaweza kustawisha majani na shina badala ya mizizi.

Inashauriwa kutumika pale tu rutuba ya shamba inapokuwa chini sana.

Dalili za upungufu wa rutuba ni kukosekana kwa virutubisho kama vile nitrojeni ambapo mimea hudumaa na kubadilika rangi na kuwa ya njano kwenye majani yaliyokomaa hatimaye hupukutika.

Vilevile mimea inaweza kukosa fosiforasi ambapo ncha za majani huonekana kama zimeungua, hufuatiwa na majani yaliyokomaa kubadilika rangi na kuwa zambarau na kudumaa. Hata hivyo, muhogo unahitaji kiasi kidogo cha fosforas kwa mahitaji ya kunenepesha mizizi.

Kirutubisho kingine ni potasiam ambayo huhitajika kwa kiasi kikubwa katika muhogo. Ikipungua mmea hudumaa.