Taarifa ya mwenendo wa uchumi wa Bara la Afrika 2018 itufikirishe

Mkurugenzi wa Benki ya Dunia kwa nchi za Tanzania, Burundi, Malawi na Somalia, Bella Bird akizungumza jana jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Ripoti ya 9 ya hali ya uchumi nchini. Picha ya Maktaba

Muktasari:

  • Mara kwa mara, Benki ya Dunia hutoa ripoti ya mwenendo wa uchumi. Hii huwa kwa dunia, bara au nchi moja moja. Kwenye ripoti ya mwenendo huo mwaka huu, ripoti inaonyesha ipo haja ya kuimarisha baadhi ya maeneo ili uchumi wa Afrika kwa ujumla ikiwmao Tanzania uwe shirikishi.

Oktoba 3, Benki ya Dunia ilizindua taarifa yake ya mwaka kuhusu mwenendo wa uchumi wa Afrika mjini Washington, Marekani. Uzinduzi huo ripoti hiyo ulifuatiliwa na kujadiliwa sehemu mbalimbali duniani ikiwamo Tanzania.

Kati ya waliochangia mjadala huo kutoka Tanzania ni mwandishi wa makala haya na baadhi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe kampasi ya Dar es Salaam.

Taarifa ya benki hiyo inaonyesha ukuaji wa uchumi Afrika, kusini mwa Jangwa la Sahara umepanda kwa asilimia 0.4 mpaka asilimia 2.7 mwaka 2018 kutoka asilimia 2.3 mwaka jana.

Huu ni ukuaji mdogo usio mzuri sana kwa bara hili kiujumla. Tanzania ina ukuaji mkubwa ukilinganisha na uliotajwa katika taarifa hii. Tanzania imefikia ukuaji wa hadi asilimia 7 kwa mwaka.

Benki ya Dunia imezungumzia ukuaji wa tarakimu tuu. Kama ilivyo kwingineko duniani, suala la msingi sio ukuaji kwa tarakimu tuu. Muhimu ni ukuaji unaowagusa wananchi kwa kupunguza umasikini, unaozalisha ajira na kipato, unaojali na kuheshimu mazingira na utawala bora.

Kufufuka kwa uchumi

Kufufuka kwa uchumi wa Afrika kutoka katika mdororo wa mwaka 2014 bado ni wa kasi ndogo kuliko ilivyotegemwea. Baada ya kufufuka, uchumi wa bara sasa umeongeza kasi ya kukua kwa asilimia 0.4 chini ya maoteo na matarajio yaliyofanyika Aprili 2018.

Hii inasababishwa na hali ya uchumi isiyoridhisha ya mataifa matatu makubwa zaidi Afrika ambayo ni Nigeria, Angola na Afrika Kusini. Benki ya Dunia inaonya kuwa barabara ya kuelekea ufufukaji kamili wa uchumi wa Afrika ni mbaya na ina milima mingi na mikubwa.

Bei ya mafuta itazisaidia nchi za Afrika zinazozalisha na kuuza nishati hiyo. Lakini, bei hiyo ambayo imefika Dola 100 kwa pipa itaumiza nchi zinazonunua mafuta kama vile Tanzania.

Kufufuka kwa uchumi kutategemea, pamoja na mambo mengine, hali ya hewa kwa nchi zinazotegemea kilimo.

Nje ya Afrika

Kama ilivyo kwa sehemu nyingine duniani, mwenendo wa uchumi wa Afrika na Tanzania kimahsusi hutegemea mazingira ya ndani na nje pia. Hii ni kwa sababu ya utandawazi. Hakuna nchi inayojitegemea kwa kila kitu.

Nchi hufanya biashara, huwekeza, hutoa na kupokea misaada na fedha kutoka kwa wananchi wake wanaoishi na kufanyakazi ughaibuni (diaspora).

Hivyo, yanayotokea nje ya Afrika yanaathiri mwenendo wa uchumi wa bara hili na Tanzania pia. Kati ya mambo hayo hatarishi ni vita vya kibiashara duniani.

Vita vya kibiashara

Vita vya kibiashara ni hali ya nchi moja kuwa na mgogoro unaosababisha kutumia mbinu za biashara ya kimataifa kuiadhibu nyingine. Sababu za ugomvi zinaweza kuwa za kibiashara na kiuchumi. Sababu zisizo za kibiashara huweza kuchangia mgogoro baina ya Taifa moja na jingine.

Nchi husika hutumia mbinu kadhaa kudhoofisha biashara ya kimataifa ya nchi nyingine. Mbinu hizi ni pamoja na kuongeza kiwango cha ushuru wa forodha ili kuzuia kiwango cha bidhaa kuingia kwenye mipaka yake.

Mbinu nyingine si za ushuru wa forodha. Hizi ni pamoja na kupunguza au kuzuia kabisa kiasi cha bidhaa zinazotoka nchi husika kuingia katika nchi inayoanzisha vita hii.

Vita vya kibiashara vimeonekana sana kati ya Marekani na China, Marekani na Uturuki na, Marekani na Irani tukitaja mifano michache. Vita hivi huathiri mwenendo wa uchumi wa dunia pia.

Kwa sababu uchumi wa dunia umefungamana kwa kiasi kikubwa, vita hivi vinaweza kuathiri uchumi wa Afrika na Tanzania pia. Inaweza kupunguza uhitaji wa bidhaa na huduma kutoka Afrika na kwa hiyo kutoka Tanzania.

Inaweza kupunguza uwekezaji na misaada kutoka kwingineko duniani kuja Afrika na kupunguza fedha zinazotumwa nyumbani na Waafrika walio ughaibuni. Yote haya si mema kiuchumi.

Madeni

Bara la Afrika lina madeni mengi na makubwa kutoka sehemu mbalimbali duniani. Japokuwa katika siku za karibuni deni linalozungumziwa zaidi ni lile la China, nchi za Afrika zina madeni kutoka sehemu kadhaa duniani ikiwamo Ulaya, Amerika na kwingineko barani Asia ukiacha China.

Changamoto kubwa ya madeni ya Afrika ni ulipaji wake. Afrika imekuwa na hamu kubwa ya madeni kwa kiasi kikubwa kwa ajili ya miundombinu. Hii sio dhambi kama madeni haya yametumika vizuri. Changamoto ni pale yanapotumika vibaya na mikopo ya muda mfupi inapogharamia uwekezaji wa muda mrefu.

Pia, ni changamoto pale sarafu za Afrika zinapopoteza thamani ukilinganisha na za nchi zinazozidai nchi za Afrika. Mwenendo wa uchumi wa Afrika na Tanzania utakuwa bora kama kodi zitakusanywa zaidi kuiwezesha kupunguza kukopa.

Ufanisi wa nguvu kazi

Taarifa ya Benki ya Dunia inaonyesha ufanisi wa nguvu kazi Afrika ni mdogo. Kati ya sababu za hali hiyo ni kutokutumia vizuri rasilimali watu. Maana yake ni kuwa katika baadhi ya nchi za Afrika nguvu kazi inatumiwa mahali ambapo sio sahihi hivyo kupunguza ufanisi.

Kiuchumi, inalipa zaidi na kuleta ufanisi mkubwa kama rasilimali watu itatumiwa kwenye maeneo yanayohitaji utaalamu, ujuzi na uzoefu wa rasilimali husika kuliko ikifanyika vinginevyo.

Ili kuboresha uchumi wa Afrika na Tanzania, ni muhimu nguvu kazi ikatumiwa unapotakiwa zaidi.