Tafakuri tano mwaka mmoja baada ya Lissu kushambuliwa

Sunday September 9 2018

 

By Luqman Maloto

Septemba 7, mwaka jana Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu alishambuliwa kwa kupigwa risasi nyingi, katika makazi yake Area D, Dodoma. Lissu alikuwa anarejea nyumbani mchana baada ya kutoka bungeni alipohudhuria kikao cha asubuhi.

Mungu alimnusuru Lissu dhidi ya kusudi la waliomshambulia. Yupo hai mpaka leo. Uhai wake ni kipimo cha wazi cha ukuu wa Mungu. Idadi ya risasi alizoshambuliwa na 16 zilizoingia mwilini, mpaka leo kuwa hai ni kudura za Mfalme wa mbingu na ardhi.

Ni mwaka mmoja umepita uliojaa maumivu na hasara. Maumivu kwa Lissu kwa sababu aliumizwa sana. Mwili wake ulivunjwavunjwa. Inaelezwa kwamba risasi zilitolewa tumboni, kiunoni, miguuni na mikononi. Shambulio hilo lilisababisha apoteze kiasi kikubwa cha damu na nyama nyingi.

Madaktari wa Hospitali ya Nairobi, Kenya, walimweleza Lissu kuwa aliongezewa damu zaidi ya robo tatu. Na hapa lazima kukiri kuwa fursa ya matibabu ya haraka na uhakika ni moja ya sababu ya uzima wake leo.

Maumivu ni makubwa kwa familia ya Lissu. Kwa mshituko baada ya shambulio. Nyakati za wasiwasi kipindi cha presha kubwa na hasa alipokuwa akihitaji uangalizi maalumu. Vilevile mapokeo mapya ya kumwona Lissu mgonjwa, aliyelala kitandani muda mrefu, akawa anatumia kiti cha magurudumu na sasa anatembea kwa msaada wa magongo.

Wananchi wa jimbo lake, Singida Mashariki, wanaumia kwa sababu umepita mwaka bila uwakilishi bungeni. Mbunge wao anapitia mapambano makali ya kurejea katika uzima wake. Ni sawa kusema kwamba tangu Septemba 7, mwaka jana, Singida Mashariki wanatawaliwa bila uwakilishi.

Lissu ni Mwanasheria Mkuu wa Chadema, vilevile Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni. Ni wakili, kipindi anashambuliwa alikuwa hana hata miezi sita tangu alipochaguliwa kuwa Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Machi 18, mwaka jana. Hiyo ilifanya TLS ikae zaidi ya miezi sita bila huduma ya Rais wake hadi walimpompata Rais mpya baadaye.

Lissu ni wakili wa kujitegemea. Amekuwa akitoa huduma za kisheria kwa taasisi na makundi ya watu wenye kuhitaji misaada ya kisheria. Hutengeneza kipato kupitia uwakili, na bila shaka alikuwa na kesi za wateja wake wengine akiwasaidia bila malipo. Makundi yote hayo yamekosa huduma yake, naye pia anakosa fedha.

Haiwezi kusahaulika kwamba Lissu alikuwa mchambuzi wa mstari wa mbele kuhusu masuala ya utawala na sheria. Alikuwa na kawaida ya kukutana na vyombo vya habari na kufanya uwasilishaji wa masuala mapya au kuchambua yaliyokuwa yakiendelea kwa kuainisha taarifa mahsusi. Huduma hii kwa Watanzania haipo kwa mwaka mmoja sasa.

Mke wa Lissu, Alicia Magabe pia ni wakili. Amekuwa akitengeneza fedha kupitia uwakili. Tangu Septemba 7, mwaka jana, amesimamisha kila shughuli ya kiuchumi na kukaa pembeni ya mume wake na kumuuguza. Hapo ni kugusa juujuu maumivu na hasara zilizosababishwa na shambulio dhidi ya Lissu, kuanzia kwake binafsi, familia, jimbo lake, Chadema, TLS, wateja wake wa kisheria, mkewe, vilevile Watanzania kwa jumla.

Tuingie kwenye tafakari

Jambo la kwanza la kutafakari ni ujasiri wa waliomshambulia. Uthubutu na dhamira yao. Je, Tanzania imekuwa ya kuwindana kutoana roho? Bado inaumiza kichwa kuusaka ukweli. Je, lilikuwa jaribio la mauaji ya kisiasa? Nyumba ya Lissu imo ndani ya uzio wa nyumba za viongozi mbalimbali wakiwemo mawaziri na naibu spika. Usalama wao upoje?

Kitendo cha watu waliotaka kumuua Lissu kuingia ndani ya uzio wa nyumba za viongozi, kufanya shambulio na kuondoka salama, kinaweza kuwafanya wao waliohusika na waovu wengine kuona kuwa viongozi wa nchi wanafikika kwa urahisi, hivyo kupanga mambo mabaya dhidi yao.

Jambo la pili la kutafakari ni upelelezi. Je, polisi wameshafunga jalada la upelelezi kuhusu shambulio la Lissu au bado unaendelea? Mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini, aliuawa kwa kupigwa risasi alipokuwa kwenye daladala, Februari 16, miezi mitano na siku tisa kutoka shambulio la Lissu. Akwilina alijikuta ni mwathirika wa kuwa kwenye eneo lenye hatari bila kupanga. Daladala aliyokuwa amepanda, ilipita kwenye eneo ambalo polisi walikuwa wakiwatawanya viongozi na wafuasi wa Chadema, waliokuwa wanakwenda kwenye ofisi za Msimamizi wa Uchaguzi Wilaya ya Kinondoni.

Polisi walitoa taarifa kuwa jalada la upelelezi kuhusu tukio hilo lilifungwa kwa sababu ya ugumu wa kumpata aliyetenda tukio. Kama tukio la Akwilina ambalo lilitokea miezi mitano baadaye upelelezi wake umefungwa, vipi Lissu?

Mwaka mzima umepita. Lissu hajawahi kufuatwa Nairobi wala Ubelgiji kuhojiwa kuhusu tukio la shambulio dhidi yake. Polisi wanasema bado wanamsubiri?

Hili la kutomfikia na kumhoji kuhusu tukio lake la kushambuliwa kwa risasi linaibua tafakuri kuhusu namna ambavyo polisi wanalifanyia kazi tukio hilo.

Zipo sheria za kusimamia na kudhibiti maudhui mitandaoni, vilevile kuna Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari. Mitandaoni kuna watu huwatuhumu watu fulani kuhusika na shambulio la Lissu. Vipo pia vyombo vya habari ambavyo huingia ndani zaidi na kueleza mpaka namna mpango wa kumshambulia Lissu ulivyoandaliwa. Je, nini kimefanyika ili watu hao wasaidie upatikanaji wa majibu yanayosubiriwa kwa hamu?

Dereva wa Lissu amekuwa gumzo. Lissu anamtetea kuwa hahusiki. Amekuwa akieleza kwamba dereva huyo alihamishiwa Nairobi na sasa yupo Ubelgiji ili kumtafutia salama ya maisha yake. Kwamba baada ya mpango wa kumuua Lissu kukwama, waliotaka kutekeleza ubaya huo waliona wakimpata dereva watakuwa wamemaliza kila kitu.

Hisia za watu wa mitandao na maelezo ya Lissu ni kipimo kwamba dereva ana vitu vingi vya kuisaidia polisi katika upelelezi wa shambulio la Lissu. Mwaka mzima umepita pasipo dereva kuhojiwa chochote. Hili linachokoa tafakuri kuhusu utayari wa polisi kuchunguza suala la Lissu ndani ya muda mzuri na kupata majibu.

Tuendelee kutafakari

Jambo la tatu la kutafakari ni kukosekana kwa walinzi kwenye nyumba za viongozi. Lissu amekuwa akieleza kwamba nyumba za viongozi hulindwa saa 24, lakini mshangao ni kuwa siku hiyo hawakuwapo, hivyo kusababisha waliomshambulia waingie na waondoke eneo la tukio pasipo upinzani wowote baada ya kumshambulia.

Je, watu waliomshambulia wanajua ratiba za walinzi kiasi kwamba walijua ni wakati gani rahisi kuingia na kumshambulia au ilitokea tu kama ajali? Swali hilo linavuta lingine kuhusu madai ya Lissu kwamba kamera za usalama kwenye nyumba za viongozi ziliondolewa baada ya shambulio.

Hili ni eneo ambalo polisi walitakiwa wawe wameshalifanyia kazi. Kama nyumba za viongozi zilifungwa kamera, maana yake zingesaidia kuwapata watu waliomshambulia Lissu. Na kama Lissu alitoa shutuma za uongo kuwa kulikuwa na kamera zikaondolewa, ilikuwa vizuri polisi waliweke sawa hilo kwa kulitolea ufafanuzi.

Tafakuri ya nne inahusu matibabu ya Lissu. Mpaka leo analalamika kuwa Bunge halijamhudumia matibabu. Hili lilikuwa ni suala la mazungumzo na lilipaswa kuwa limepatiwa ufumbuzi. Mwaka mzima, mbunge mwenye stahiki za kutibiwa na Bunge, anajitibu mwenyewe au kwa michango ya watu binafsi na chama chake. Hili linafikirisha.

Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisema utatatibu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), unaelekeza wagonjwa wote wenye kutibiwa nje ya nchi, wanapaswa kuwa wamepitia Hospitali ya Taifa, Muhimbili na kupewa rufaa. Na kwamba rufaa ya Muhimbili huelekeza moja kwa moja mgonjwa atibiwe Hospitali ya Apollo, India.

Lissu alishambuliwa kwa risasi Dodoma na kupewa matibabu ya awamu ya kwanza Hospitali ya Mkoa wa Dodoma. Alihamishiwa Hospitali ya Nairobi kwa matibabu ya awamu ya pili, kisha Ubelgiji. Ni kweli kwa mtiririko huo, na kwa maelezo aliyotoa Ndugai, ni wazi matibabu ya Lissu hayajafuata mfumo wa NHIF.

Lakini Lissu amekuwa akiitafsiri Sheria ya Uendeshaji wa Bunge ya mwaka 2008, kwamba sheria hiyo imesema kwa kifupi kwamba kila mbunge atakuwa na haki ya kutibiwa ndani au nje ya Tanzania kwa gharama ya Bunge. Hapa anamaanisha kuwa huo utaratibu wa NHIF haumo kwenye sheria hiyo.

Kwamba Bunge ndilo lina wajibu wa kisheria wa kutibu wabunge. Nalo limesajili wabunge NHIF ili mfuko huo ubebe gharama za matibabu ya wabunge. NHIF nao wameweka utaratibu wa kumhudumia mgonjwa anayetakiwa kupewa matibabu nje ya nchi. Hata hivyo, mwisho kabisa, mfumo wa NHIF siyo sheria ya Bunge.

Suala la Lissu lina mazingira yenye kutengeneza udharura. Familia na chama chake walihofia usalama wake, hivyo wakataka apelekwe Nairobi badala ya Muhimbili. Kiungwana menejimenti ya Bunge ilipaswa kutambua hili. Nani ndugu yake anaweza kupigwa risasi halafu asiingiwe na wasiwasi kuwa waliompiga wangeweza kumfuatilia ili kummalizia?

Ilitakiwa Bunge liketi na kuangalia namna ya kushirikiana na familia ya Lissu. Kujitenga kabisa na matibabu yake wakati ni mbunge, tena kiongozi ndani ya Bunge, hakuleti tafsiri nzuri.

Tafakuri ya tano ni ushirikiano baina ya wabunge. Utengano mkubwa umeonekana katika matatizo ya Lissu. Wabunge karibu wote wa CCM hawakwenda Nairobi kumjulia hali Lissu. Aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini (CCM), Lazaro Nyalandu, ndiye pekee alikwenda kwa uwazi, ila aliporejea alijivua uanachama wa CCM na kujiuzulu ubunge. Kuna nini hapa? Ubelgiji mbali, Nairobi je, au wabunge hawana nauli?

Advertisement