Tamu, chungu kwa Messi Barcelona

Monday February 18 2019

 

Lionel Messi alikosa penalti, lakini alifunga kwa mkwaju mwingine kama huo katika mchezo ambao Barcelona ilishinda bao 1-0 dhidi ya Real Valladolid.

Nahodha huyo wa zamani wa Argentina, amefikisha mabao 30 katika msimu 2018-2019.

Messi alikosa penalti baada ya kiungo nyota Phillip Coutinho kufanyiwa madhambi na mchezaji wa Real Valladolid Kiko Olivas.

Hata hivyo, mkwaju wa Messi ulipanguliwa na kipa Jordi Masip ambaye alicheza kwa ustadi mchezo huo ambao Barcelona ilikuwa nyumbani kwenye Uwanja wa Nou Camp.

Kipa huyo aliokoa michomo mingine ya Luis Suarez na Messi waliokuwa na kiu ya kufunga mabao.

Messi alisahihisha kosa lake kwa kufunga bao hilo dakika ya 43 na kuipa Barcelona pointi tatu.

Watani wao wa jadi Real Madrid wanashika nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi wakiwa ni pointi mbili nyuma ya Atletico Madrid.

Barcelona imejiweka katika nafasi nzuri ya kushinda mchezo wa leo itakapovaana na Lyon, kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Kocha wa Barcelona Ernesto Valverde alimpanga Kevin-Prince Boateng katika mchezo huo. Mchezaji huyo amejiunga na klabu hiyo katika usajili wa dirisha dogo mwezi uliopita ulioibua mjadala.

Katika mchezo huo, beki nguli Gerard Pique alicheza mechi yake ya 300 katika Ligi Kuu Hispania.

“Jambo bora zaidi ni kupata ushindi ingawa hatukucheza kwa kiwango bora,” alisema beki huyo wa kati.

Kipa wa Real Valladolid alisema walikuwa na nafasi ya kushinda kwa kuwa walikosa nafasi nyingi za kufunga baada ya kupenya ngome ya Barcelona.

Advertisement