Tamu, chungu miaka mitatu ya Mashinji kuongoza Chadema

Muktasari:

  • Daktari huyo wa binadamu zamani kabla hajawa mwanasiasa, anasema kwa sasa Chadema ipo katika vijiji, vitongoji, halmashauri na mikoa yote tofauti na awali ilipokiwa katika maeneo machache huku ikikosekana katika baadhi ya kanda.

Ni matukio ya sura mbili katika miaka mitatu ya uongozi wa Dk Vincenti Mashinji. Yapo mafanikio katikati ya hali ngumu.

Katika mahojiano maalumu na Mwananchi Dk Mashinji ambaye ametimiza miaka mitatu tangu ateuliwe kushika wadhifa huo Machi 12, 2016, anasema, “najivunia mambo niliyoyafanya ndani ya chama, najisikia faraja kuona sasa tuna taasisi ambayo ipo imara. CCM walijaribu kutubomoa lakini kwa mfumo uliopo tumevuka katika hali hiyo.”

Daktari huyo wa binadamu zamani kabla hajawa mwanasiasa, anasema kwa sasa Chadema ipo katika vijiji, vitongoji, halmashauri na mikoa yote tofauti na awali ilipokiwa katika maeneo machache huku ikikosekana katika baadhi ya kanda.

Anasema kwa sasa chama chake kinakamilisha mpango wa chama wenye kubainisha mikakati yao kwa kipindi fulani na mambo wanayotarajia kufikia.

Katikati ya mafanikio hayo, ana jingine la kusema:

“...Nimekuwa na wakati mgumu katika uongozi wangu.”

Akiwa katibu wa nne wa Chadema tangu kilipoasisiwa, Dk Mashinji alitanguliwa Bob Makani, Dk Walid Kabourou na Dk Willibrod Slaa.

Lakini, hutu ni mtendaji wa juu wa chama hicho ambaye amekutana na changamoto nyingi katika utawala wake tofauti na waliomtangulia.

Dk Mashinji aliyechukua nafasi iliyoachwa na Dk Slaa, jina lake halikuwa miongoni mwa majina yaliyotabiriwa kushika nafasi hiyo.

Majina yaliyotabiriwa na wengi kushika uongozi huo ni Salum Mwalimu, Frederick Sumaye, Benson Kigaila, John Mnyika, Dk Marcus Albanie na Profesa Mwesiga Baregu.

Akizungumzia utendaji wake, anakiri ni mtendaji aliyekutana na wakati mgumu kwa kushindwa kufanya siasa za majukwaani baada ya kuzuiwa.

Dk Mashinji aliyezaliwa mkoani Mara mwaka 1973, anasema uongozi wake umekutana na changamoto nyingi, mbali na siasa za jukwaani kuzuia hata zile za ndani zinazoelezwa ziko huru wameshindwa kuzifanya kwa kuzuiwa na polisi.

Anasema uongozi wake badala ya kueneza siasa majukwaani umejikuta ukilazimika kufanya siasa za chinichini, lakini kubwa zaidi ni kukamatwa kwa viongozi wengi na kulazimika kutumia muda mwingi kwenye kesi.

Makatibu wakuu waliomtangulia walikuwa na fursa ya kufanya siasa za majukwaani, hakukuwa na kizuizi cha Serikali hata kamatakamata ya wanasiasa wa upinzani haikuwa kubwa kama ilivyo sasa, anaeleza. Anasema kamatakamata ya wapinzani inamfanya alazimike kutumia muda mwingi ofisini, lakini pia anatimiza miaka mitatu ofisini wakati mwenyekiti wake Freeman Mbowe akiwa mahabusu tangu Novemba 23, 2018.

Pia, kiongozi huyo kwenye uongozi wake ameshuhudia wimbi la madiwani, wabunge na aliyekuwa mgombea urais wao Edward Lowassa wakitangaza kukihama chama hicho na kurudi kwenye chama chao cha zamani CCM.

Hata hivyo, anasema pamoja na changamoto hizo pia ameweza kukieneza chama hadi ngazi ya chini vijijini na mijini kwenye maeneo mengi nchini, tofauti na ilivyokuwa mwanzo.

Chadema haijafa

Akizungumzia minong’ono kwamba chama hicho sasa kimekufa katibu huyo anasema Chadema haiwezi kufa kwa sababu ni dynamic (kinabadilika kulingana na mazingira) kutoka na waasisi wake walivyokianzisha.

“Mzee Bob Makani na Mtei hawakuwa na interest ya kundi kubwa la watu kwa sababu linataka tu mabadiliko, tubadilishe tuweke rais mwingine kwa hiyo wale watu wanatafuta tu urais, lakini hawa walikuwa na ajenda ya kiuchumi na unakuwa taratibu.

Anasema Chadema imepita katika vipindi vitatu ambavyo ni kwanza ilijikita katika kutengeneza miongozo ambayo ina-washape (inawajenga) wanachama wake.

“Baadaye kilitengeneza mfumo wa kufanya maamuzi iliyokuwa shirikishi, lakini mwisho ni kufanya rebrand kila baada ya muda fulani, mfano mwaka 2004 wakati tunaenda kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2005 tulikuwa na bendera imepauka tukaamua kuibadili na ndiyo tukaja na hizi rangi na kuja na logo mpya.

“Tukagundua kwamba centrality (uongozi wa juu kuamua kila jambo) ya chama kadri kinavyokuwa hakikisaidii chama ila inakidhoofisha kwa hiyo tuka dicentralitize (kutoa madaraka katika kanda) tukaanzisha kanda tukabakisha madaraka kidogo tu makao makuu na mengi ya operesheni yakaenda kwenye kanda.

Dk Mashinji anasema baada ya kuingia ofisini cha kwanza ilikuwa ni kuhakikisha mfumo huo unafanya kazi na viongozi wanabaki kusimamia sera na kutoa miongozo.

“Ndiyo maana kwa sasa migogoro ndani ya chama imepungua sana siyo kama zamani kwa sababu chama sasa kimerudi katika mfumo wa utawala ambao unatumika na Serikali lengo ikiwa ni kufanya maandalizi ya kwenda kuchukua dola.

“Kwa hiyo ukisema Chadema inakufa siyo si sahihi bali imebadili mtazamo wake, kwamba awali tulikuwa na siasa za hamasa na kuwahiana, ‘umesema asubuhi, jioni lazima nikujibu’, lakini sasa tunaweza kufanya siasa hizo lakini na mimi nikawa na mambo yangu nayafanya mwenyewe.

Dk Mashinji anasema mfumo huo umesaidia kuongeza wafuasi wengi nchi nzima, kufanya uchaguzi ndani ya chama, tunawaandikisha watu katika daftari la uchaguzi na tunazindua sera ya chama.

Hata hivyo, anaeleza hofu akisema, “Siasa za nchi za Afrika ni chafu, unapoenda kulala ukawa salama unashukuru sana” na analo la kushukuru, kwamba ni watu wanaomkosoa kuliko wanaomsifia.

Uchaguzi Mkuu wa 2020

Anasema chama chao kinatambua uchaguzi wa 2020 ni mkubwa kwa sababu wanapigania kuchukua Bunge, halmashauri na ikulu kwa wakati mmoja tofauti na chaguzi za marudio.

Dk Mashinji amesema ushindi unawezekana kwa sababu mazingira yatakuwa tofauti na chaguzi ndogo.

“Tunaenda kupigania dola, mwaka 2025 tulikuwa na excitement (hamasa) kubwa ya kisiasa hata hivyo ni somo kubwa sana kwetu, endapo tutaenda namna vile ‘tutapigwa’ tu.

“Hao polisi unayoona wakifanya katika uchaguzi mdogo wanajua Rais ni John Magufuli, lakini katika Uchaguzi Mkuu wanajua yoyote anaweza kushinda kutokana na jinsi mtakavyokuwa mmeonyesha jamii mnaweza kuongoza nchi kwa kiasi gani, kwa hiyo ile kupendelea upande mmoja inapungua.

“Pia, wananchi wataenda kuchagua mtu wanayemtaka, kutakuwa na waangalizi wa kimataifa lakini pia wagombea watakuwa na passion (shauku) ya ushindi,” anasisitiza Mashinji na kuongeza kuwa hakuna jeshi linaloweza kushinda wananchi.

Makatibu wakuu waliotangulia
Wasifu wa Dk Mashinji

Dk Mashinji ni daktari bingwa wa magonjwa ya binadamu, msomi mwenye shahada moja ya udaktari (MD), shahada  tatu tofauti za uzamili (Mastersdegree) na shahada moja ya uzamivu ya uongozi (PhD).
Dk Mashinji ni mtafiti wa kujitegemea, mwenye karama ya uongozi na asiyeogopa chochote katika kuitetea nchi, wananchi na haki zao.
Wakati wanateuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Chadema mwaka 2013 alikuwa na umri wa miaka 43.
Bob Makani
Bob Makani  ni Katibu Mkuu wa kwanza wa Chadema aliyezaliwa mwaka 1936 katika Hospitali ya Kolandoto, Shinyanga.
Alisoma Chuo Kikuu cha Makerere kilichopo nchini Uganda na alifuzu shahada ya kwanza ya uchumi (BA Economics).
Mwaka 1961 alikwenda Chuo Kikuu cha Liverpool kilichopo nchini Uingereza na 1965 alitunukiwa shahada ya sheria (LLB).
Mwaka 1992 mfumo wa vyama vingi vya siasa ulipokubaliwa Bob Makani na Edwin Mtei walikuwa mstari wa mbele katika kuunda chama cha siasa.
Kikao cha mkutano mkuu wa kwanza wa Chadema Desemba 1991, ndipo Bob Makani akachaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Kwanza wa chama hicho. Kazi ya kwanza Bob Makani ilikuwa ni kueneza chama kipya nchini.
Dk Amani Walid Kabourou
Dk Amani Walid Kabourou ni Katibu Mkuu wa pili wa Chadema ambaye alizaliwa Mei 23, 1949. Dk Kabourou alikuwa mbunge wa Kigoma Mjini kwa tiketi ya Chadema kwa mara ya kwanza mwaka 1995 alichaguliwa tena kwenye uchaguzi wa 2000-2005 na mwaka 2006 aliamua kurejea CCM ambako alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Kigoma.
Dk Willbrod Slaa
Dk Willbrod Slaa alizaliwa Oktoba 29, 1948 katika kijiji cha Kwermusi, wilaya ya Mbulu.
Alikuwa katibu mkuu wa Chadema wa tatu na alijiuzulu nafasi ya ukatibu mkuu na uanachama wa Chadema mwaka 2015 baada ya ujio wa waziri mkuu mstaafu Edward Lowassa ambaye alipewa nafasi ya kugombea urais mwaka huo.
Dk Slaa alikuwa mgombea wa urais wa chama hicho katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.
Kabla ya kugombea urais mwaka 2010 alikuwa mbunge wa Karatu miaka 1995-2010; baada ya kugombea Urais akawa si mbunge tena.