Tawfiq: Mbunge anayevalia njuga kope, kucha bandia

Muktasari:

  • Tawfiq ni mtoto wa aliyewahi kuwa katibu mkuu wa Tanu, Hassan Tawfiq, ambaye anatajwa kuwa miongoni mwa watu waliomsaidia Mwalimu Nyerere katika harakati za uhuru.

Dodoma. Mtoto wa nyoka ni nyoka. Huu ni msemo wa wahenga ambao unasadifu maisha katika nyanja zote, ikiwamo siasa.

Ingawa wapo wanasiasa walioingia katika siasa bila kuwa na historia ya kuzaliwa au kukulia ndani yake, wapo waliozaliwa na wanasiasa hata wakajikuta wamekuwa wanasiasa na wakati mwingine ndio wanaovuma zaidi.

Hili linajitokeza kwa mwanasiasa na mwanaharakati wa siku nyingi, Fatuma Hassan Tawfiq ambaye ndani ya Bunge la kumi na moja anajulikana kama ‘mama wa kope na kucha bandia’.

Huyu ni mbunge wa Viti Maalumu (CCM) kutoka Mkoa wa Dodoma. Ni mwalimu, mwanaharakati wa haki za wanawake. Katika awamu ya nne alikuwa mkuu wa wilaya.

Tawfiq ni mtoto wa aliyewahi kuwa katibu mkuu wa Tanu, Hassan Tawfiq, ambaye anatajwa kuwa miongoni mwa watu waliomsaidia Mwalimu Nyerere katika harakati za uhuru.

Maisha ya Fatuma

Katika simulizi yake inaonyesha Fatuma alikuwa mwanaharakati tangu akiwa binti mdogo shule ya msingi, lakini umaarufu wake ulipanda kadri siku zilivyosonga.

Akizungumzia maisha yake katika mahojiano na Mwananchi, Fatma anasisitiza kuwa amezaliwa katika familia ya wanasiasa na baba yake alikuwa mwanasiasa mpambanaji hata kabla ya uhuru.

Mimi ni mwalimu wa kusomea na kufundisha. Nimefundisha miaka mitatu kisha nikaenda Botswana ambako nilisoma ngazi ya diploma na niliporudi nikateuliwa kuwa ofisa elimu Dodoma Vijijini.

Baadaye mwalimu huyo alijiendeleza hadi shahada ya pili katika masuala ya jinsia (Masters in Gender) kisha akasomea mambo ya harakati za kisheria kwa wanyonge

Anasema kazi hiyo aliifanya kwa moyo na katika kuzunguka akakutana na matatizo makubwa ya wanawake wanaonyanyasika. Na uanaharakati ukaanzia hapo.

Ni kwa vipi aliacha utumishi wa serikali na kuwa mwanaharakati? Tawfiq anasema mateso ya wanawake vijijini, ukosefu wa haki zao na ukeketaji kwa watoto wa kike ndivyo vilimfanya aamue hivyo bila kujali mbele yake kungekuwa na nini

Alipoulizwa kama aliachana na shirika alilolianzisha kuhusu utetezi huo, anasema hawezi kuacha WOWAP (Women Wake Up), na kila siku yuko ofisini kuendeleza mapambano.

Anasema ubunge aliomba ili awe mtumishi wa watua na anajisikia faraja anapokutana na watu na kuzungumzia matatizo yao ambayo mengi anayamaliza au kutoa ushauri.

Mbunge huyo anasema uongozi kwake si suala jipya, alianza tangu akiwa shule ya msingi alikokuwa kiongozi kwenye makundi huku akiwa mwanachama wa chipukizi.

“Ndoto hiyo haikufa kwani kadiri siku zilivyopita nilikuwa natafuta uwakilishi,” anasema.

Tawfiq pia alikuwa miongoni mwa wanawake walioandika historia mwaka 1995 alipokwenda kwenye mkutano wa Beijing nchini ambako aliwawakilisha vijana wa kike Tanzania.

Mwaka 2005 na 2010 aliomba ubunge bila mafanikio na kuupata mwaka 2015. Pamoja na harakati zake anasema bado kuna safari ndefu kwa kuwa ukandamizwaji bado mkubwa.

“Utakumbuka nilipoingia kwa mara ya kwanza bungeni niliuliza lini sheria ya ndoa ya 1971 italetwa tuifanyie marekebisho lakini hadi leo ni danadana.

Nyingine ni sheria ya mirathi ya kimila ambayo inamnyima mwanamke haki ya kumiliki mali isiyohamishika kama ardhi na nyumba, lakini nitapambana humuhumu (bungeni) hadi kieleweke.

Akizungumzia tatizo lilipo, Tawfiq anasema hakuna utashi katika kurekebisha sheria.

“Bila ya kupepesa macho naona wenzetu wanaume hawajawa tayari sheria hizi zibadilike hivyo ipo kazi ya kufanya.

Anapokumbushwa jambo aliloliibua bungeni kuhusu kope na kucha za bandia, mbunge huyo anacheka na kusema “nilijua utauliza, hadi leo bado napambana nalo, haya ni mambo hayana faida kwetu zaidi ya hasara.”

Anasema kulikuwa na rafiki yake (jina linahifadhiwa) ambaye alikwenda kumweleza namna alivyopata madhara baada ya kuwekewa kope za bandia, jambo lililosababisha maumivu ya jicho na licha ya kutibiwa hadi leo amekuwa na uono hafifu

Kwa maelezo ya mbunge huyo madaktari walishamweleza kuhusu madhara ya kucha na kope bandia ndiyo maana akalipeleka bungeni.