Thamani ya amani Zanzibar sawa na shilingi iliyopotea

Muktasari:

  • Watu walitembea hata usiku wa manne bila wasiwasi na ilikuwa kawaida kumwona mwana mama aliyejipamba kwa dhahabu, anatembea usiku kwenda au kurudi harusini peke yake na kwa raha zake bila ya wasiwasi.

Kwa miaka mingi mpaka siku za hivi karibu Zanzibar ilisifika kila pembe ya dunia kuwa ni visiwa vya amani na wizi wa kutumia silaha au mauaji yalikuwa si mambo ya kawaida hapa.

Watu walitembea hata usiku wa manne bila wasiwasi na ilikuwa kawaida kumwona mwana mama aliyejipamba kwa dhahabu, anatembea usiku kwenda au kurudi harusini peke yake na kwa raha zake bila ya wasiwasi.

Lakini leo hali hiyo ndio ile inayoitwa “Akher zamani”, yaani hali iliyopotea na kutoweka na kama kishada kilichokwenda arijojo.

Hali hii ya visiwa hivi vya Unguja na Pemba kuwa shwari na vya amani, vilipelekea watu wake kujivunia na kuwa na msemo wa “Zanzibar ni njema atakaye aje”.

Wakati nikiwa mdogo ilikuwa inapita miaka mitano hadi sita bila ya kusikia mtu kuuawa au hata kujeruhiwa vibaya kwa mapanga.

Nakumbuka kama mara mbili hivi, wakati nikiwa ninasoma shule ya msingi katika miaka ya 1950 yalitokea matuko mawili ya mauaji mjini Unguja.

Katika tukio moja nilishuhudia maiti ya mwanamke mwenye umri wa makamo ilifunikwa kanga katika jaa la taka (jalala) eneo la Gongoni, mjini Unguja ambapo ilitupwa.

Tukio hili lilishtua watu kila pembe ya Zanzibar na kila sehemu kulikuwa hapana mazungumzo kwa watu wa kila rika isipokuwa habari za yale mauaji ya yule mwana mama.

Siku ile baadhi ya maduka yalifungwa kama kuomboleza kifo kile na katika misikiti palifanyika sala maalumu ya kumuombea rehema yule maiti na kumuomba Mola aiepushe Zanzibar na matukio ya kijahili kama ya mauaji.

Katika nyuma za baadhi ya wawakilishi wa serikali mitaani, wanaojulikana kama masheha, bendera nyekundu ya Zanzibar iliyokuwa ikitumika wakati ule zilipepea nusu mlingoti.

Siku zimepita, miezi imehesabika na miaka kukatika. Ni nusu karne sasa tokea kuwepo mauaji yale na ninachokiona ni hali kuwa imebadilika sana.

Kwa kweli hali ninayoiona sasa sio tu inasikitisha bali ni ya kutisha na kuelekea mtu kuuliza nini kilichoisibu Zanzibar na visiwa hivi viliosifika kwa amani vinaelekea wapi?

Ni kweli idadi ya watu wa Zanzibar imeongezeka sana, kutoka laki tatu (300,000) wakati ule na sasa kukaribia milioni 1.5.

Lakini pia tukumbuke kuwa wakati ule idadi ya askari polisi wa Visiwani na wale wa kujitolea ilikuwa kama 700 tu.

Wakati ule Zanzibar haikuwa na jeshi na vikosi vingine vya ulinzi ukiachia askari wachache wa Zimamoto na Magereza (sio zaidi ya 100).

Idadi ya Wazanzibari

Hivi sasa idadi ya watu wanaohusika moja kwa moja na ulinzi ni zaidi ya mara 10 ya idadi ya hapo zamani na vipo vikosi vya ulinzi ambavyo ukivihesabu utakaribia kumaliza vidole ya mikono miwili. Hii ni pamoja na mamia ya vijana wanaojulikana kama polisi shirikishi (polisi jamii).

Lakini, siku hizi kila baada ya siku chache unasikia habari za mauaji mijini na vijijini na wengi wa wanaouawa kikatili ni wanawake.

Matukio ya hivi karibuni ya wanawake wawili kuuawa, mmoja alikutwa katika eneo la Tunguu, kusini Unguja na mwingine katika Kijiji cha Ndagaa, katikati ya Kisiwa cha Unguja.

Polisi wameeleza kwamba baadhi ya watu wamekamatwa na wanahojiwa kwa kushikiliwa kuhusika na mauaji haya. Tunasubiri maelezo zaidi juu ya uchunguzi unaofanywa na Jeshi la Polisi na kuona nini kitafuatia juu ya mauaji haya ya kinyama.

Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa) kimetoa tamko kulaani mauaji haya ya wanawake yanaoendelea na kuvitaka vyombo vya ulinzi kuchukua hatua za kuidhibiti hali hii mbaya inayokuwa kwa kasi Visiwani.

Tamwa imeelezea masikitiko yake kuwa vitendo wa kikatili vya kijinsia vimekuwa vikiongezeka na kwa bahati mbaya hakuna uwazi wa kueleza chanzo cha hali hii na njia gani zinatumika kuwalinda wanawake na uovu huu.

Polisi, jamii wafanye nini?

Ni vizuri kwa polisi kufanya juhudi zaidi za kuwasaka wanaohusia na ukatili huu na kuchukua hatua kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi.

Lakini, jamii nayo isikwepe wajibu wake kwa sababu hawa wauaji ni watu wanaoishi nao mitaani na vijijini. Upo umuhimu kwa kila mtu Visiwani kujiona ana wajibu wa kusaidia kupambana na uhalifu kwa kuwafichua watu ambao nyendo zao zinatia shaka.

Pia, vitendo vya ubakaji na kunajisi watoto navyo vinahitaji kumulikwa na vikosi vya ulinzi kwa kushirikiana na wananchi kuwafichua wote wanaohusika na uhalifu huu.

Wazanzibari lazima waamue kwamba wanaweza kutofautiana kwa kabila, imani za dini, mapenzi ya kisiasa na mambo mengine lakini si kwa suala la amani ya visiwa vyao.

Uhalifu, kama mauaji na vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji wa aina moja au nyengine hauchagui.

Ni Wazanzibari wenyewe ndio wenye uamuzi wa wapi visiwa hivi vielekee… kwenye amani au kuwa na huu mtihani wa kupoteza maisha yao mikononi mwa watu wachache walioamua kuwa majahili na kuua watu kwa sababu wanazozielewa wenyewe.

Tushirikiane kufichua wahalifu na kulinda amani ya Zanzibar na watu wake. Vinginevyo kila mmoja atakuja kujuta kwa nini aliipuuza hali iliyopo sasa.

Thamani ya amani, kama ya shilingi, huwezi kuijua mpaka pale itakapokutoka mkononi na kuwa huna kitu mfukoni. Tusikubali kuipoteza amani iliopo hivi saa ala hapo baadaye.