Tiketi ya Fainali za Kombe la Dunia kwa U-17 inaanzia hapa

Dar es Salaam. Fainali za Afrika kwa vijana chini ya miaka 17 ‘Afcon U17’ ambayo yatatimua vumbi nchini kuanzia Aprili 14 hadi 28 Aprili, ndiyo yatakayotoa wawakilishi wa Afrika kwenye Fainali za Kombe la Dunia kwa vijana nchini Brazil.

Timu ya taifa la Tanzania kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ ni miongoni mwa timu za mataifa manane ambayo yamejinoa vilivyo kupigania nafasi hiyo ya kwenda Brazil.

Kuna nafasi nne kwa bara la Afrika kutoa timu ambazo zitaungana na nyingine kutoka mabara mengine kucheza Fainali za Kombe la Dunia kuanzia Oktoba 5 hadi Oktoba 27.

Awali Peru walipewa uwenyeji wa fainali hizo lakini Februari ya mwaka huu walipokonywa kutokana na ubovu wa miundombinu uliopo kwenye taifa hilo.

Baadaye Machi, Brazil walipewa uwenyeji huo.

Katika harakati za Serengeti Boys kuwa miongoni mwa mataifa manne kutoka Afrika yakayoshiriki fainali hizo, wanahitajika kushindi michezo miwili ya Afcon U17.

Ushindi wa michezo hiyo miwili ni kwenye hatua yao ya makundi ambapo wamepangwa Kundi A na timu za vijana za mataifa mengine ambayo ni Nigeria, Angola na Uganda.

Katika michezo yao ya kundi hilo, Aprili 14 wataanza kibarua cha kupigania nafasi hiyo kwa kucheza na Nigeria Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Aprili 17 ni dhidi ya Uganda na Aprili 20 watamalizana na Angola.

Ushindi katika michezo hiyo miwili kati ya mitatu ya makundi utawafanya kutinga nusu fainali na kujikatia tiketi ya moja kwa moja kushiriki fainali za Brazil.

RAIS TFF ASISITIZA

Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia alisema vijana wa Serengeti Boys alikuwa nao bega kwa bega kwenye maandalizi yao ili wawe na nguvu ya kulipigania Taifa kwenye mashindano hayo.

“Tunaenda kuweka historia kwenye Soka la Tanzania, baada ya Simba kwenda robo, Taifa Stars kufuzu Afcon na sasa ni zamu ya Serengeti Boys kwenda Brazil, niliomba ili Mungu aniwezeshe ndani ya uongozi wangu niache alama nzuri ya mafanikio katika mchezo wa soka,” anasema Karia.