Toolboksi inayowaunganisha vijana na fursa za ufundi

Wewe ni kijana mbunifu na una ujuzi wa kutengeneza kazi za mikono, lakini umekosa sehemu sahihi ya kuonyesha uwezo wako ili kujipatia kipato cha kuendesha maisha?

Usihofu teknolojia ndiyo ‘mpango mzima’ katika zama hizi za matumizi ya simu na kompyuta, kwa sababu inakuletea suluhisho na kukufungulia fursa mbalimbali mkononi mwako.

Wabunifu wamebuni tovuti maalumu ya toolboksi ambayo ni nyenzo muhimu kuwaunganisha vijana wa rika tofauti wenye ujuzi na stadi za maisha kama useremala, ufundi ujenzi, magari, vifaa vya umeme, utunzaji wa bustani, nyumba na fursa mbalimbali za ufundi zilizopo katika jamii.

Tovuti hiyo, iliyobuniwa na kuendeshwa na kampuni ya teknolojia ya Toolboksi Limited ya Tanzania, ni jukwaa linalowasaidia vijana waliojiajiri kuwafikia watu na taasisi zenye uhitaji wa kutengenezewa au kukarabatiwa kifaa au kitu chochote cha ofisini au nyumbani kinachosaidia shughuli nyingine zifanyike.

Kupitia toolboksi, wewe kijana unayeishi jijini Dar es Salaam hutohangaika tena kuweka matangazo au kuzunguka mitaani kutafuta wateja, kwa sababu teknolojia hiyo inakuunganisha moja kwa moja na mteja wako popote alipo.

Mwanzilishi wa tovuti hiyo, Julius Mbungo anasema tovuti hiyo pia inawasaidia watu na taasisi mbalimbali zinazohitaji mafundi wenye ujuzi tofauti kuwafanyia kazi za mikono katika maeneo yao ambapo inaondoa pengo la taarifa muhimu za ufundi katika jamii, kuharakisha shughuli za maendeleo na kuokoa muda ambao mteja na fundi wangekutana.

“Tumeamua kuja kutatua tatizo la ukosefu wa ajira na umasikini, kwa sababu kuna maelfu ya watoa huduma hususan mafundi stadi, wanawake kwa wanaume ambao wana ujuzi na wako tayari kufanya kazi lakini hawapati nafasi,” anasema.

Mbungo anabainisha kuwa maeneo ambayo yamekuwa na uhitaji mkubwa wa ufundi ni pamoja ufundi wa mabomba ya maji, umeme, useremala, uashi, ufungaji wa madishi ya visimbuzi. Maeneo mengine ni utengenezaji wa viyoyozi, kompyuta,samani na usafi wa nyumba.

Ukitazama kwa ukaribu utagundua kuwa maeneo hayo yanagusa moja kwa moja maisha ya binadamu katika nyanja za usalama wa afya na mazingira yanayomzunguka, ambayo yana mchango mkubwa wa kuharibu au kuendeleza maisha ya binadamu.

Tayari toolboksi inafanya kazi na mashirika na taasisi zinazowajibika moja kwa moja katika kuendeleza ujuzi na ufundi stadi kama Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), taasisi ya Digital Opportunity Trust (DOT) na kampuni ya ujenzi ya JINGU.

Vijana wanaounganishwa katika jukwaa hilo wanapatiwa mafunzo zaidi, ili kuimarisha stadi zao na jinsi ya kuwahudumia wateja ili kukidhi mahitaji wakati wakitoa huduma za ufundi.

Kwa mteja anayetaka huduma ataingia kwenye mtandao huo na kuchagua huduma inayoitaka na kuweka oda. Baada ya hapo utapokea barua pepe, ujumbe mfupi wa maneno (SMS) au kupigiwa simu kulingana na njia uliyotuma maombi. Mafundi wa toolboksi watafika nyumbani au ofisini kwako kwa kutumia anuani ya makazi kufanya tathmini ya ukubwa wa kazi na kufanya makubaliano ya bei. Baada ya makubaliano kazi itafanyika kwa uangalifu mkubwa kulingana na mahitaji ya mteja.

Kazi ikikamilika malipo yatafanyika hapo hapo baada ya kujaza fomu maalumu, ili kuthibitisha kama kazi imefanyika vizuri.

Watumiaji wa huduma za kifedha kupitia simu watasubiri kidogo wakati tovuti hiyo itakapokamilisha mfumo wa malipo kwa njia ya mtandao

Toolboksi inawafikia vijana wote hadi wale wasiotumia intaneti ambapo wanaweza kupiga simu au kutuma ujumbe mfupi wa maneno, ili kuunganishwa katika orodha ya mafundi ambao wameidhinishwa kufanya shughuli hizo katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam.

Mpaka sasa jukwaa hilo la mtandaoni limeshasajili vijana rasmi 350 na 500 wasio rasmi wa Dar es Salaam wenye ujuzi na kuwaunganisha na wateja waliopo katika maeneo mbalimbali ili kujipatia kipato cha kuendesha maisha.

Hata hivyo, huduma hii haipatikani kwa mikoani kwa sasa, jambo linalofanya mafundi wa maeneo hayo kukosa fursa ambazo wenzao wa Dar es Salaam wanazipata.

Siku zijazo, Mbungo anasema wamepanga kuwafikia vijana wa mikoa ya Mbeya, Arusha na Dodoma, ikiwa ni hatua ya kuongeza wigo wa huduma na kushiriki katika mikakati ya wadau wa maendeleo kuwaondolea vijana umasikini na kuwaunganisha na fursa zilizopo katika jamii.

Makala haya kwa hisani ya tovuti ya www.nukta.co.tz