Tufunge mjadala kuwaweka ndani watumishi

Muktasari:

Sheria ya Tawala za Mikoa ya mwaka 1997 (The Regional Administration Act) kwenye kifungu cha 15 (1) imeweka shar-ti muhimu kwa Mkuu wa Wilaya ikiwa atahitaji kutumia mamlaka ya kuamri-sha mtu akamatwe, kifungu hicho kinam-taka afanye hivyo pale tu ambapo atakuwa ameji-hakikishia kuwa kosa lililotendwa na mhusika athari yake huwa ni kukamatwa na kushtakiwa na tena sheria imeweka masharti ya namna ya kushtaki.Sheria hiyohiyo katika kifungu cha 15 (1) imeeleza kuwa ikiwa mkuu wa wila-ya atatumia mam-laka yaliyowekwa na kifungu husika kwa maana ya kutumia madaraka yake viba-ya, atakuwa ameten-da kosa na anaweza kushtakiwa kwa mujibu wa kifungu cha 96 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu (Penal Code).

Alhamisi Novemba Mosi 2018 katika ukumbi wa Nkrumah ulioko Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kulifanyika kongamano la kutathmini hali ya uchumi na siasa katika nchi yetu, hususani kwa kulenga kipindi cha miaka mitatu 2018 – 2018 ambayo serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli imehudumu.

Mjadala wa Nkrumah ulihudhuriwa na JPM mwenyewe, akiwa kama mshiriki maalumu. Mambo mengi muhimu yalizungumzwa na mengi yalitufundisha na kutuhabarisha juu ya kule ambako taifa letu limetoka, lipo na linakwenda. Kama nikisema nizungumzie masuala yote hayo nadhani ukurasa huu hautatosha, nimeonelea nichague jambo moja tu, mjadala wa kuwaweka ndani watumishi wa umma.

Ninatambua kwamba Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alilifafanua jambo hili vizuri, kwamba wakuu wa mikoa na wilaya hawatumwi na Rais kufanya hivyo, lakini akasisitiza kuwa ukiwasikiliza wahusika hao nyakati ambazo huwa wanalazimika kuchukua hatua hizo, unaweza kuamini kuwa kumbe walipaswa kuchukua hatua kali zaidi ya hizo za kuweka ndani mtumishi wa umma anayehusika.

Mtazamo wa JPM

Rais JPM alikuwa wazi zaidi, akaeleza kuwa yapo makosa ambayo anaowateua wanayafanya, aidha kutokana na ujana na kuchemka kwa damu au sababu nyingine. Akasisitiza na kuwaomba Watanzania wawasaidie wateule wake na wasiwatizame kwa jicho baya hata pale wanapoteleza kwani wanajifunza zaidi.

Kinachoonekana hapa ni kuwa, hata Rais mwenyewe anaonesha haungi mkono sana hii tabia ya kuwaweka watumishi wa umma mahabusu badala ya kuwachukulia hatua za kinidhamu zinazoendana na hadhi au taratibu zao za kazi.

Kutofurahishwa huko kwa Rais kunaweza kuwa dhahiri kupitia kwa kauli mbalimbali ambazo zimekuwa zikitolewa na mawaziri wake au watendaji wake wengine ambao wamo serikalini.

Walichosema mawaziri

Agosti 15 mwaka huu, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TamisemiI, Mussa Iyombe aliwaonya wakuu wa wilaya wateule dhidi ya tabia ya kuwaweka ndani watumishi wa umma. Iyombe aliwaeleza wakuu wapya wa wilaya kwamba wanalo jukumu la kutowachukulia hatua za kinidhamu watumishi wa Serikali kwa kukurupuka hasa kwa sababu watumishi hao wana mamlaka zao za nidhamu.

Iyombe alitoa maelekezo haya kwa sababu yamekuwako matukio ya wakuu wa wilaya au wakuu wa mikoa kuwakamata watumishi wa umma na kuwaweka ndani kwa kutumia mamlaka ya kisheria ambayo yanawapa uwezo wa kumwweka ndani mtu yeyote saa zisizozidi 48 wakiridhishwa kuwa mtu huyo anahatarisha amani.

Malalamiko ya namna hii pia yamewahi kutolewa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu pamoja na Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo, wote wawili wakionya tabia ya watu wenye mamlaka katika mikoa na wilaya kuwakamata na kuwaweka ndani watendaji wa Serikali.

Waziri Jafo amelipigia sana kelele suala hili mwezi Septemba na Oktoba 2018 kwa nyakati tofauti.

Mfano wa Mtaka

Agosti 17, 2018, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka, wakati akifunga kikao cha madaktari wa mikoa na wilaya zote nchi nzima kilichofanyika mjini Dodoma, alishaajihisha mjadala huu wa kuwaweka ndani watumishi wa umma kwa kuonesha kushangazwa na tabia ya wakuu wa wilaya kuwaweka ndani watumishi wa umma.

Mtaka alisisitiza, “sisi viongozi tuwalinde watumishi wetu, mimi nilipoenda kuwa mkuu wa mkoa wa Simiyu niliwaambia wakuu wangu wa wilaya kuwa sitaki kusikia mtumishi wa umma anawekwa mahabusu...kwenye mkoa wangu hutaona upuuzi huo.”

Kauli hii ya Mtaka inasisitiza kukerwa na kuguswa na ukubwa wa tatizo hili ambalo sasa linageuka kuwa mjadala wa kitaifa hadi kutolewa maoni na Rais JPM akitaka wateuliwa wake waendelee kupewa muda na nafasi ya kujifunza kutokana na makosa yao na akiwaomba Watanzania wasiwahukumu.

Mamlaka yanatoka wapi?

Mamlaka ya mkuu wa mkoa na mkuu wa wilaya kuagiza kukamatwa kwa mtu na kuwekwa rumande yanapatikana kwenye vifungu vya 7 (mamlaka ya mkuu wa mkoa) na 15 (mamlaka ya mkuu wa wilaya) vya Sheria ya Tawala za Mikoa ya mwaka 1997. Vifungu hivyo vinafanana kila kitu isipokuwa kile cha 7 kinamtaja mkuu wa mkoa na kile cha 15 kinamtaja ‘mkuu wa wilaya’.

Swali muhimu la kujiuliza ni je, wakuu wa mikoa na wilaya, hata kama sheria inawapa mamlaka ya kumkamata mtu yeyote na kumweka ndani kwa saa 48 wanapaswa kufanya hivyo kiholela tu hata kwa nyakati ambazo walipaswa kufanya kinyume chake? Je, wakuu wa mikoa na wilaya wanapaswa kufanya hivyo hata kwa watumishi wa umma ambao wanaweza kuwajibishwa kwa mifumo tofauti kabisa ya uwajibikaji ambayo imeanishwa kwenye sheria na taratibu za ajira na kazi?

Sheria mbalimbali zimetungwa ili kuongoza namna mwananchi anavyopaswa kuhusiana na wenzake na Serikali au mamlaka zilizomo kwenye nchi yake, lakini sheria yoyote ile lazima itumiwe kwa busara kubwa inapata uhalali wake. Huwezi tu kufuata sheria inasema nini hata katika mazingira ambamo busara inapaswa kuchukua nafasi yake.

Mfano wa JPM na adhabu ya kunyonga

Sheria za nchi yetu zimeeleza wazi kuwa mahakama inaweza kumhukumu mtu yeyote kunyongwa hadi kufa, ikiwa mtu huyo atakutwa na hatia katika makosa makubwa ambayo adhabu yake ni kifo.

Makosa kama mauaji ya kukusudia ni mfano halisi wa yale ambayo yanaweza kumpa mtu adhabu ya kifo. Pamoja na kuwepo kwa sheria na utoaji wa adhabu ya kunyonga hadi kufa. JPM amewahi kusema hadharani kuwa hawezi kuidhinisha mtu yeyote yule kunyongwa.

Hii haina maana kwamba Rais anakiuka sheria. Sheria zilitungwa na wanadamu na zinatumiwa na wanadamu. Rais anaona kuwa kumyonga mtu labda ni kinyume na maadili, utu na utamaduni wa Kitanzania. Busara zinamwambia usiidhinishe watu wanyongwe. Mbona Rais anayo mamlaka ya kisheria ya kuidhinisha watu wanyongwe na hayatumii, kutoyatumia kunamfanya asiwe Rais mwenye mamlaka? Kunampunguzia nini?

Wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya wanalo jukumu kubwa la kutumia madaraka yao kwa busara za hali ya juu. Kila Mtanzania anajua kuwa wanayo mamlaka hayo na kwamba kutoyatumia ovyoovyo hakuwaondolei hadhi na ukuu wao kwenye wilaya na mikoa yao.

Tufunge mjadala huu

Mamlaka ya wakuu wa mikoa na wilaya ya kumweka mtu yeyote ndani yatumiwe kwa malengo ya utungaji wa sheria husika. Watumishi wa umma kwa sababu wao wana taratibu maalumu za kinidhamu, wataepuka kikombe hiki. Hawa wangelipaswa kufuata hatua zingine muhimu za kinidhamu ambazo zinaweza kuwa kubwa kuliko hii ya kuwekwa ndani, lakini zenye maadili na utaratibu wa ajira na kazi. Tuufunge mjadala huu kwa kuwakumbusha wakuu wa wilaya na mikoa kuzingatia hatua zote ambazo zimeelezwa kwenye sheria niliyoitaja pale juu.

Kwanza, “...Mkuu wa mkoa/wilaya aweza kukamata au kuagiza kukamatwa kwa mtu yeyote ambaye mbele yake anatenda kosa au alitenda kosa ambalo linamfanya mtu huyo kuweza kukamatwa na kushtakiwa.” Kwa vyovyote vile, kosa linalozungumziwa hapa linapaswa kuwa kosa la jinai.

Pili, “...kama mkuu wa mkoa au wilaya ana sababu za kuamini kuwa mtu yeyote aweza kuvunja amani au kuharibu utulivu uliopo au kufanya kitendo chochote ambacho kinaweza kuvunja amani au kuharibu utulivu na uvunjifu huo hauwezi kuzuiwa kwa njia yoyote nyingine isipokuwa kumsweka rumande mtu huyo, mkuu wa mkoa au wilaya aweza kuagiza kwa maneno au maandishi kukamatwa kwa mtu huyo”.

Tatu, “...Mtu aliyekamatwa kwa amri au maelekezo ya mkuu wa mkoa au wilaya anapaswa kufikishwa mahakamani ndani ya saa 48 kwa ajili ya kufunguliwa mashtaka ya jinai. Endapo hatafikishwa mahakamani kwa muda unaopaswa, na muda kuisha, anapaswa kuachiwa na hapaswi kukamatwa tena kwa amri ya mkuu wa mkoa au wilaya kwa namna ileile”

Nne, “...wakati wa kuagiza kukamatwa kwa mtu yeyote au muda mfupi baada ya kuagiza, mkuu wa mkoa au wilaya lazima aandike sababu za kukamata au kuagiza kukamatwa kwa mtu husika na kupeleka nakala kwa hakimu ambaye mbele yake aliyekamatwa atafikishwa kwa ajili ya kushtakiwa.”

Tano, “...Hakimu ambaye mbele yake aliyekamatwa atafikishwa kwa ajili ya kushtakiwa, aweza kumwachia huru aliyekamatwa, kumpa dhamana au kutoa agizo la kuachiwa aliyekamatwa.

Yeyote (mkuu wa mkoa au wilaya au ofisa wa polisi) ambaye ataagizwa na mahakama kumwachia aliyekamatwa na hatatii agizo hilo atashtakiwa kwa kuidharau mahakama chini ya kifungu 114 cha kanuni ya adhabu.”

Sita, “...Mkuu wa mkoa au wilaya yeyote au mtu yeyote ambaye atampelekea mkuu wa mkoa au wilaya kutumia vibaya mamlaka yake chini ya sheria ya tawala za mikoa (vifungu husika vya kukamatwa mtu) atatenda kosa la jinai na anaweza kushtakiwa chini ya kifungu cha 96 cha Kanuni ya adhabu, sura ya 16 ya Sheria za Tanzania.”

Julius Mtatiro ni mchambuzi wa mfuatiliaji wa utendaji wa Serikali barani Afrika; ni mtaalamu mshauri wa miradi, utawala na sera na ni mtafiti, mfasiri, na mwanasheria. Simu; +255787536759 (Whatsup, Meseji na Kupiga)/Barua Pepe; [email protected])