Tuitazame China idadi ya wabunge, urefu wa vikao na ufanisi wake

Muktasari:

Kutokana na nafasi ya China katika uchumi wa dunia, mkutano wa Bunge la Umma la China huwa unafuatiliwa sana duniani. Hii ni kutokana na kuwa mambo yanayojadiliwa na maamuzi yanayofanywa, yana athari za moja kwa moja kwa biashara, uwekezaji, usalama na hali ya uchumi duniani.

Hivi karibuni ulifanyika mkutano wa Bunge la Umma la China jijini Beijing baada ya kufanyika kwa siku 11.

Mkutano huo uliwakutanisha wajumbe zaidi ya 2,900 kutoka maeneo mbalimbali ya nchi na sekta mbalimbali. Pamoja na mambo mengine, kubwa walilofanya katika mkutano huo ni kujadili ripoti ya serikali iliyohusisha maelezo ya kazi ilizofanya katika mwaka uliopita, kujadili na kupitisha mipango ya kazi kwa mwaka huu na kufanya marekebisho ya sheria.

Kutokana na nafasi ya China katika uchumi wa dunia, mkutano wa Bunge la Umma la China huwa unafuatiliwa sana duniani. Hii ni kutokana na kuwa mambo yanayojadiliwa na maamuzi yanayofanywa, yana athari za moja kwa moja kwa biashara, uwekezaji, usalama na hali ya uchumi duniani.

Kwa Afrika, kuna mambo kadhaa yaliyojadiliwa na Bunge hilo, yanayohusiana moja kwa moja na maslahi ya nchi zetu, kama vile kodi ya uagizaji wa bidhaa na kufunguliwa kwa sekta nyingi za uwekezaji, ambazo hapo awali zilikuwa ni kwa wenyeji tu. Lakini, vilevile fursa zaidi zimetangazwa kupitia pendekezo la “Ukanda mmoja, njia moja” (BRI).

Lakini, mbali na mambo hayo makubwa, kuna mengine ambayo kwa Wachina yanaweza kuonekana ni madogomadogo, ambayo huenda hata wao wenyewe wasiyafuatilie. Lakini, mimi binafsi nimekuwa nikiyafuatilia na naamini yanaweza kuwa somo lenye manufaa kwa nchi zetu.

Kwanza ni uwakilishi. Tumekuwa na imani ya muda mrefu kuwa wenye elimu na uwezo kifedha ndio wanaweza au wanastahili kuwa wabunge au wawakilishi. Ndiyo maana mara nyingi tunasikia wabunge maprofesa, wahandisi na matajiri, na kulifanya Bunge kuwa kama “klabu” ya watu wa namna hiyo.

Naomba nisieleweke vibaya kuwa hawa watu hawafai au hawastahili kuwakilisha wananchi. Tumeona wakiwakilisha wananchi kwa ufanisi, lakini pia ni bora tukifahamu kuwa kuna kundi kubwa zaidi la watu ambao hawatoki katika klabu hiyo ambao sauti zao hazisikiki moja kwa moja. Kwenye Bunge la China, kati ya wabunge hao wachache kuna uwakilishi mpana kiasi kwamba maslahi ya watu wengi yanakuwa na sauti ya moja kwa moja bungeni.

Lakini, zaidi ya hapo kuna chombo kingine kinachoitwa Baraza la Mashauriano ya Kisiasa, hiki ni chombo ambacho kinawakutanisha wajumbe kutoka sekta mbalimbali, wanaokaa na Chama cha Kikomunisti cha China (CCP) na kutoa mapendekezo mbalimbali kutoka kwenye maeneo wanayofanyia kazi.

Pili, ni ufanisi wa uwakilishi na gharama za kuendesha Bunge. Licha ya eneo kubwa la nchi na idadi kubwa ya watu, Bunge la umma la China hukaa kwa muda wa siku 10 tu. Na katika siku hizo kumi, ripoti ya serikali kuhusu utendaji wa mwaka uliopita na mipango ya mwaka unaokuja, na hata miswada ya sheria na maagizo kwa serikali, vinajadiliwa kwa kina na kwa ufanisi mkubwa.

Hali hii inabana sana matumizi ya fedha na kutotoa fursa ya kujadili baadhi ya mambo yasiyo na tija kwa wananchi na taifa. Inawezekana kuwa hii ni kutokana na mfumo wa kisiasa wa hapa China, ambao serikali imefungamana sana na chama tawala.Inawezekana baadhi ya watu wakasema haya hayawezi kufanyika kwenye nchi yetu kwa kuwa tuna mfumo tofauti wa siasa. Lakini, katika siasa hakuna lisilowezekana.

Tatu ni nidhamu. Tukiangalia nidhamu ya wabunge ndani ya bunge ni ya hali ya juu. Mijadala inaendeshwa kwa kiasi kwamba kuna utulivu na nidhamu ya hali ya juu. Moja ya sababu ni kuwa muda wa bunge ni mfupi sana, hakuna nafasi ya kupiga porojo. Kila dakika ya kikao ina maana, na kila kinachojadiliwa ni maswala (issues) na si vijambo. Nidhamu hii inafanya bunge liwe tulivu na kusiwe na haja ya spika kuanza kusema “order, order, order”.

Tukiangalia mambo haya matatu, tunaweza kuona kuwa ukubwa wa nchi, au hata idadi ya watu, havimaanishi kuwa ni lazima bunge liwe na idadi kubwa ya wabunge, au kuwe na vikao vya muda mrefu. Nikijaribu kuangalia bunge la China naona kuwa katika muda wa siku 10, wabunge wa China ambao ni chini ya elfu tatu, wanaowakilisha watu bilioni 1.4, wanajadili maswala yote ya msingi, kupitisha sheria, na kufanya maamuzi na kutoa maagizo kwa serikali. Mbali na hilo, wanapokuja Bungeni hapa Beijing, tunaona wanatumia mabasi ya “Coaster” kwenda na kutoka bungeni, hii pia ni moja ya njia za kupunguza gharama.

Isieleweke vibaya kuwa mfumo wetu haufai. Bila shaka kuna nchi nyingi ambazo zinafuata mfumo mabunge ya jumuiya ya madola.

Lakini, kama kuna yale ambayo tunaweza kujifunza kwa wengine ambao si jumuiya ya madola, na tukaweza kupunguza gharama za kuendesha bunge na kuongeza ufanisi wake haitakuwa jambo baya.