Tuliwapa Hasheem Thabeet, wanatupatia Nba Africa Game

Monday June 11 2018

 

Jioni moja tulivu ya Alhamisi ya Juni 25, 2009 Watanzania tuliungana kwa lugha moja kusimama na kuishi kwenye nchi ya Marekani hata kama wengi wetu hatujawahi kuigusa kwa maana ya kusafiri safari ya masaa ishirini na kutua.

Tulikuwa tumetulia tukisuri kusikia namna gani ligi kuu ya mpira wa kikapu nchini Marekani, NBA ilikuwa inampokea Mtanzania wa kwanza kucheza kwenye ligi hiyo na ambaye alikuwa anakuwa balozi wa kwanza ambaye angetambulika kimataifa katika kizazi hiki cha teknolojia na mitandao ya kijamii.

Naam akiwa amevaa suti nadhifu, kwenye eneo la kuita wachezaji wakati wa uchaguzi wa wachezaji wanaotoka vyuoni na kwenye ligi mablimbali kuingia NBA, kamishna wa NBA kwa wakati huo, David Stern alisoma jina la Hasheem Thabeet katika chaguo la pili na kwenda kwenye klabu ya Memphis Grizzlies.

Kwa Watanzania huu ulikuwa ushindi. Huu ulikuwa wakati wa furaha na huu ulikuwa wakati tulioamini kuwa tunaweza kutumia michezo mingine zaidi ya soka peke yake. Ulikuwa wakati ambao ulituma ujumbe kwa vijana wadogo kuwa tunaweza kufanya mengine nje ya soka kama ambavyo kipindi cha akina Filbert Bayi kilivyopata watu wnegi zaidi wanaopenda mchezo wa riadha.

Kuna tatizo moja pekee nyuma ya ligi hii ya NBA nalo ni muda wa michezo yake dhidi ya muda wetu huku Tanzania na Afrika kwa ujumla.

Michezo mingi inachezwa usiku wa manane au alfajiri kwa masaa yetu lakini uwepo wa Hasheem ulifanya kila mtu ajaribu kufahamu ni kitu gani kilikuwa kinatokea.

Sio kila mchezaji anayekuja na “potential” kubwa kwenye NBA basi hutokea kuwa mchezaji bora, na hili lilikuwa suala kwa Hasheem Thabeet ambaye bahati mbaya hakufanya vyema ikilinganishwa na wachezaji alioingia nao kwenye NBA kwa mwaka 2009.

Swali pekee lililobaki kwa Watanzania ni tulitumiaje nafasi hii kuweza kuwafanya watoto wafahamu umuhimu wa elimu ukihusishwa na mchezo wa mpira wa kikapu.

Katika kipindi kirefu ambacho Hasheem hakuwa gumzo NBA ni kama hata vyombo vya habari Tanzania vilimsusa, hakuna aliyetaka kumfanya balozi wa Taifa tena na tulikosa mafiga ya kuinjika chungu ambacho ni vipaji vya mpira wa kikapu Tanzania.

Miaka saba baadae yaani 2015 tangu Hasheem aanzishe safari ya Watanzania kwenda Marekani kimasomo kwa ndoto tuliyoanza kuamini kuwa inawezekana ya kuingia NBA tayari kuna jambo jema lilikuja Afrika nalo ni NBA AFRICA GAME.

Ikiwa ni sehemu ya kujitangaza na kutafuta soko la Afrika, NBA waliona kuna haja ya kutupatia fursa ambayo tumekuwa tukiikosa muda mrefu. Tayari wlaikuwa wameanzisha nyenzo za kusaka vipaji kama Basketball without boarders (mpira wa kikapu bila mipaka) program iliyozalisha wachezaji wengi wa NBA kama Joel Embiid, lakini pia Junior NBA ambayo imelenga kusimamia vijana wa miaka 14 kushuka chini na pia NBA Academy ambayo inasimamia wachezaji wenye vipaji waliokusanywa maeneo mbalimbali na kuwekwa pamoja.

Kuwa na vitu hivi peke yake haikuwa inatosha kwa sababu bado wahenga walisema kuona ni kuamini.

Badala ya kusafirisha hawa vijana wote kuwapeleka Marekani kushuhudia michezo ya NBA, ilitakiwa ifanywe kuwa rahisi zaidi na ndipo wazo la NBA AFRICA GAME lilipozaliwa.

Huu ni mchezo unaohusisha wachezaji wenye asili ya Afrika waliopo kwenye NBA dhidi ya wachezaji wa mataifa mengine. Kuanzia mwaka 2015 ulianza kufanyika pale Afrika Kusini na vijana kutoka kwenye Basketball without Boarders, JR NBA na NBA Academy hupata nafasi ya kufundishwa na makocha na wachezaji wa NBA kwa muda wa wiki moja.

Hii huwajenga vijana na kuwapa ndoto kubwa zaidi. Baada ya Hasheem Thabeet hatuna kisingizio kuwa hatuwezi kupata balozi wa kuliongoza taifa na kulifikisha mbali. Kwenye uwanja wa Jakaya Kikwete Youth Park kuna kituo mahususi ambapo vijana wa mashuleni wana nafasi ya kushiriki mashindano ya JR NBA.

Binti wa Kitanzania, Jessica Ngisayise naye alipata kuwepo kwenye Basketball Without Boarders na kushuhudia mchezo wa NBA AFRICA 2017, kitu ambacho naamini kilibadilisha fikra zake na hata wenzie waliamini kila jambo linawezekana.

Kwenye mboni zangu nilimwona Jessica akipata mafunzo kutoka kwa wachezaji kama CJ McCollum, Joel Embiid, Kristaps Porzingis na makocha Eric Spoelstra ambaye ni bingwa wa NBA mara mbili. Sio jambo dogo hata kidogo.

Bahati mbaya nyingine ni kuwa, hata vyombo vya habari navyo havijapata nguvu ya kusukuma matukio makubwa kama haya na kuna fursa nyingi wanazoweza kupata kuhakikisha kuwa wanaweza kuwa sehemu ya matuko kama haya.

Wizara zinaweza kushirikiana nasi na kuwapa nafasi ya kuwatumia hawa nasi pia tunatakiwa kuwa jirani kusaidia serikali.

Wakati tukiwa tumeanza kusahau umuhimu wa Hasheem Thabeet katika kuhamaisha vijana wetu, wao NBA wala hawajivungi naye, na wanamtumia kweli. Mapema mwezi huu Juni wamemtumia kutangaza kurejea kwa mchezo wa NBA AFRICA tena. Akiwa na Didier Mbenga, Mkongo aliyewahi kuchezea Los Angeles Lakers walitangaza kila ambacho NBA watafanya wakati huo.

NBA wala hawajajisahaulisha, wametangaza tayari kuwa NBA AFRICA GAME 2018 inarejea tena Afrika katika jiji la Pretoria nchini Afrika Kusini Agosti 4, 2018, wachezaji kama Joel Embiid na DeMar Derozan wakiwa manahodha. Hata mheshimiwa Kigwangala anaweza kutumia nafasi hii kuwafikia pasipo kwenda Marekani.

Ni wakati wa kufikiria namna ya kutumia hizi fursa bila kutupa lawama sehemu moja. Hata Hasheem ni rafiki wa moja kwa moja wa nyota kama Russell Westbrook, Kevin Durant na Stephen Curry, kwa bajeti nzuri anaweza kuwaleta.

Sio lazima tufanye ya VISIT RWANDA kwenye jezi za Arsenal. Tuitumie Agosti 4, 2018 vyema kwani wachezaji wa NBA watakuwa hapo Afrika Kusini tu. Hasheem Thabeet atakuwa balozi wao, tumtumie pia.

Advertisement