MAKENGEZA : Tunatokwa na povu kila jambo

Sunday November 25 2018

 

By Richard Mabala

Juzi mimi na mwenzangu tuliamua kwenda sebuleni kwetu tujikumbushe enzi zetu maana bangi ya waishiwa imebanguliwa siku hizi utadhani korosho. Tangu Mwishiwa Supu akane kazi yake kuhakikisha kwamba kila mtu anaweza kufungua mdomo kuingiza supu na kutoa hoja na badala yake kujigeuza vuvuzela tu, waishiwa wamesambaratika na bado hawajaweza kutafuta njia nyingine ya kukutana.

Ingawa nasikia kwamba wapo wale vijivuzela vya mwishiwa Supu ambao wameamua kukaa naye sehemu nyingine ili mradi wapate supu ya dezo kila siku. Ubwege wa kubugia supu na kubwaga maneno ya sifa. Nashangaa kwamba hawasinzii kabla ya kumaliza minofu maana hakuna kitu kinachotia usingizi kama nyimbo za sifa tu kila siku. Mwishiwa Supu anaweza kuvimbiwa kichwa lakini sisi waishiwa wengine tutavimbiwa macho ya usingizi tu.

Basi mimi na mwenzangu tulienda kulekule kwetu kwa zamani na baada ya kufakamia supu kama kawaida yetu, yeye aliamua kupambana na chupa kama vile ni maadui zake. Baada ya kuua chupa mbili alikuwa tayari kuongea.

‘Unajua Makengeza, nimetafakari sana na nimegundua kwamba hawa wanaharakati wanapiga kelele bure.’

‘Kwa vipi?’

‘Wakati huu si wakati wa siku 16 kupinga ukatili wa kijinsia. Wanapoteza muda. Ukatili wa kijinsia ni sehemu muhimu ya mila zetu, kwa nini wapige kelele? Lazima tulinde utamaduni wetu.’

Nikashangaa.

‘Eti nini? Yaani mwenzangu, chupa mbili tu tayari umechanganyikiwa?’

‘Sijachanganyikiwa chochote. Hebu angalia watu wanavyotoa povu kuhusu mashoga, hadi hawana sababu ya kununua sabuni ili wafue nguo zao? Povu zao zinatosha.’

‘Lakini ushoga ni kinyume cha utamaduni wetu!’

‘Unaona? Hata wewe! Mbona hawatoi povu hivyo kuhusu ubakaji, au kutongoza na kuwarubuni watoto wadogo? Ina maana kwamba ni sehemu ya utamaduni wetu.’

‘Ni kinyume cha sheria.’

‘Sawa lakini kila siku wasichana wanabakwa. Wavulana wanananihiiwa lakini wapi povu? Huwezi kufua hata leso na povu lililopo. Kwa hiyo, narudia kusema ina maana kwamba ubakaji na kurubuni watoto ni sehemu ya utamaduni wetu.’

‘We Bwana, naona kweli tuondoke kabla pombe haijapanda kichwani zaidi. Mwisho utaanza kuimba nyimbo za Kinyamwezi. ‘

‘Makengeza, wewe hutaki kuona ukweli. Katika shirika letu, tunafanya kazi na vijana. Wasichana wananiambia kwamba wakitoka tu kwenda shuleni, au sokoni au wapi sijui, wanatongozwa si chini ya mara kumi kwa siku. Wasichana wenyewe ndiyo kwanza wamevunja ungo lakini wanatongozwa kama vile ni manyota ya muvi za ngono. Na watu wanaangalia tu. Mara nyingine wanawachekelea wanaume wanavyomsumbua yule dada. Haya, na msichana akibakwa, nani anapiga kelele, zaidi ya wanaharakati wachache? Kukiwa na harufu ya ushoga, mafuriko ya povu, lakini watoto wakibakwa, kavu kama jangwa la Sahara.’

‘Nimekuelewa kidogo. Yaani unasema kwamba sisi ni wanafiki. Povu kulia, kavu kushoto.’ Linatakiwa liweko kotekote.

‘Sawa kabisa.’

‘Lakini kwa sawa tuko katika hizi siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.’

‘Sawa. Na kila mwaka ni vivyohivyo. Na sisi wengine tunajaribu kupaza sauti kwamba hili ni janga la kitaifa lakini siku 16 zitapita na tutabaki palepale. Hebu nikupe mfano mwingine. Shirika letu lilienda kuangalia maoni ya vijana huko Liberia ili yaingie katika Mkukuta wao. Kwa sababu walikuwa wamemaliza vita muda si mrefu uliopita, suala la usalama lilikuwa muhimu sana. Waliposema usalama, walimaanisha je, wameng’oa mizizi ya mapigano ya wenyewe kwa wenyewe, lakini baada ya kuwasikiliza vijana wa kike, walilazimika kuingiza ukatili wa kijinsia ndani ya mpango wao wa usalama kitaifa pia maana wasichana walisema kwamba, hata kama vita vya wenyewe kwa wenyewe vimekwisha, vita yao havijaisha. Kila siku wanakuwa wahanga wa ukatili wa kijinsia. Kwani wasichana dhidi ya wakatili siyo vita vya wenyewe kwa wenyewe pia?’

‘Naona hapa unataka kulinganisha manyunyu na kimbunga. Wale ndiyo kimbunga.’

‘Hujui rafiki yangu. Hata upande wa wasichana wetu ni kimbunga pia. Kama huamini, nenda kwenye jamii na waombe wasichana wachore ramani ya jamii zao na kuonyesha sehemu ambazo hawajisikii salama. Mara nyingi ni karibu kila mahali, zikiwemo shule, zahanati na ofisi za serikali. Mara nyingine hata sehemu za ibada. Sasa iwapo hata watu wenye heshima zao wanafanya hivyo, utakataaje kwamba si sehemu ya utamaduni wetu. Wacha Bwana! Wasichana wetu wako vitani, tena ajabu ni kwamba wakijeruhiwa vitani wanalaumiwa wao tu.’

‘Hapo ninakuelewa. Msichana ambaye ndiyo kwanza amevunja ungo, hajapita unyago, wala hajapewa mafunzo ya stadi za maisha shuleni, anakutana na mtongozaji mzoefu (maana sisi wanaume tunafanya mazoezi na kupeana mbinu za kutongoza) hivyo binti wa watu hajui jinsi ya kujihami wala kujinasua kisha tunamrundikia lawama badala ya yule ambaye amemtongoza au kumlazimisha. Ajabu.

‘Kwa hiyo tukubaliane kwamba ubakaji ni mila yetu.’

Jamaa akasimama na kupaza sauti.

‘Ushoga ziiii, ubakaji juu!’

Kabla sijaweza kumpinga, alizimia. Watu wengine Bwana!

Advertisement