Tupime uzani wa Bunge la Nane hadi la kumi na moja

Wednesday November 28 2018

 

By Luqman Maloto

Uzani wa Bunge hupimwa kwa namna mhimili huo unavyoweza kuibana Serikali au hata kuiwajibisha.

Hata hivyo, haimaanishi Serikali isipowajibishwa Bunge linakuwa halifanyi kazi sawasawa. Lakini kuna swali: “Dunia bila dhambi kipimo cha uovu kingekuwa nini?”

Bunge kama haliiwajibishi kabisa Serikali kipimo cha meno yake ni nini? Ina maana Serikali inatenda mambo yake bila presha. Wananchi wanaona kimya. Kuna wakati watajiuliza: “Je, tumechagua wawakilishi sahihi wa kuisimamia Serikali?”

Hivyo, Bunge linavyoibana waziwazi Serikali ndivyo huonekana linafanya kazi zake vizuri. Tayari Bunge la 11 chini ya Spika Job Ndugai limekuwa likidaiwa kuwa karibu na Serikali.

Kauli ya Rais John Magufuli Septemba 7, mwaka jana kuwa Ndugai alimpigia simu kumwomba mawazo yake alipotaka kuunda kamati maalumu za kuchunguza shughuli za uchimbaji na biashara ya madini ya Tanzanite na almasi nchini iliashiria jambo hilo.

Bunge la 11 limetimiza miaka mitatu. Na katika kipindi chote cha uwepo wake, Serikali imewajibika mara moja. Mazingira ya uwajibikaji ni sawa kusema Serikali yenyewe iliamua kujiwajibisha, maana hakukuwa na mjadala ndani ya Bunge wala hakukuwa na maazimio ya Bunge kuitaka iwajibike.

Tatizo lilikuja kwamba ripoti za kamati teule za Bunge zilizochunguza almasi na Tanzanite mwaka jana hazikusomwa bungeni, hivyo wabunge wote hawakupata fursa ya kujadili. Badala yake ripoti zikapelekwa juu kwa juu kwa Rais Magufuli.

Ripoti za Bunge ambazo zilisababisha Rais awaondoe kazini waziri na naibu waziri hazikujadiliwa na wabunge. Hapa bila kupepesa maneno ni kwamba Bunge halikuiwajibisha Serikali, isipokuwa Serikali ilijiwajibisha yenyewe kwa utashi wa Rais.

Ukiacha hilo, Rais Magufuli amekuwa akiwaondoa mawaziri na manaibu bila Bunge kuhusika. Idadi kubwa ya mawaziri walioanza na Serikali ya Awamu ya tano wameshawekwa kando pasipo Bunge kuchangia chochote.

Tofauti na mabunge yaliyopita Bunge la 10 lililoongozwa na Anne Makinda, Ndugai akiwa naibu spika lilikuwa imara na lilishuhudiwa likiiwajibisha Serikali mara nyingi zaidi katika historia ya nchi. Pamoja na dosari ambazo zinaweza kutajwa lilijitahidi kuthibitisha hadhi na nguvu yake.

Ni Bunge la 10 lililoendesha uchunguzi na mijadala ya kashfa za ufisadi Benki Kuu kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow na ile ya ukiukwaji wa haki za binadamu katika operesheni ya Tokomeza. Mara zote ripoti ziliposomwa na ikajadiliwa, baraza la mawaziri lilimeguka.

Mwaka 2012, Bunge la 10 lilisababisha mawaziri wanane waondolewe kazini baada ya kusoma na kuchambua ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), iliyobainisha madudu na uzembe katika maeneo yao.

Hiyo ni mifano kuonesha kuwa Bunge la 10 lilikuwa moto. Bunge la Tisa lililoongozwa na Samuel Sitta pia lilikuwa na meno, liliwezesha kung’oka kwa Waziri Mkuu Edward Lowassa na mawaziri wengine wawili kupitia kashfa ya Richmond, halafu Baraza la Mawaziri likavunjika.

Bunge la nane

Bunge la Nane, lililoongozwa na Pius Msekwa lilimsimamisha aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utawala Bora, Dk Hans Kitine. Sakata hilo maarufu kama Kashfa ya Kitine, lilionekana kabisa kuwa na harufu ya rushwa.

Katika kashfa hiyo, ilidaiwa kuwa Dk Kitine alitumia fedha za serikali, Dola za Marekani 63,000, kumtibu mke wake, Saada Mkwawa Kitine, nje ya nchi.

Uchunguzi wa baadaye ulionesha kuwa Dk Kitine alidanganya, na kwamba mke wake hakutibiwa nje ya nchi. Kashfa hiyo ilisababisha Kitine ajiuzulu uwaziri na mke wake aliamriwa kurudisha fedha hizo.

Hapo ndipo unaweza kuona namna Bunge linavyoonesha ukali kwenye fedha za wananchi, vilevile usalama wa watu.

Bunge la 11 chini ya Ndugai nalo linatakiwa kuonyesha uwezo na nguvu zake katika kuchunguza kashfa mbalimbali na kutoa mapendekezo yatakayopeleka serikali kuwajibika.

Advertisement