HOJA ZA KARUGENDO : Tusikubali kushinikizwa, tusikubali kupigishwa magoti

Aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa akihutubia  kwenye mkutano wa kampeni mwaka 2015.Lowassa amerejea CCM.Picha ya Maktaba

Muktasari:

  • Watanzania walijua nguvu za CCM, walijua kiu ya madaraka waliyokuwa nayo viongozi wa CCM, nguvu ya pesa na kuwa upinzani wa kweli ulikuwa bado haujazaliwa. Walijua jinsi wale wote waliojiita wapinzani walikuwa wamenyimwa nafasi ya kula ndani ya chama.

Tunaweza kukwepa kushinikizwa na Jumuiya ya Kimataifa? Tunaweza kuziba masikio yetu tusisikilize hoja za mashirika hayo yanayotoa misaada hapa kwetu? Au ni lazima kuendelea kukubali shinikizo na kufuata matakwa yao?

Historia inaonyesha Tanzania, tulikubali mfumo wa vyama vingi kwa kushinikizwa ndiyo maana hadi leo hii hatukubali kupokea mfumo huu kama sehemu ya maisha yetu.

Dunia ya leo inaimba siasa ya vyama vingi vya siasa, demokrasia, usawa wa kijinsia, haki za binadamu. Tunaweza kutenda kinyume? Tunaweza kukataa mfumo wa vyama vingi vya siasa na kushabikia siasa ya chama kimoja?

Hata kama chaguo la watu wetu ni chama kimoja cha siasa? Tunaweza kukataa kushinikizwa na kupigishwa magoti?

Kura za maoni zilizofanyika wakati Tanzania inajiandaa kuipokea siasa ya vyama vingi vya siasa, zilionyesha kwamba asilimia 20 ya Watanzania walitaka siasa ya vyama vingi na asilimia 80 walikataa.

Watanzania walijua nguvu za CCM, walijua kiu ya madaraka waliyokuwa nayo viongozi wa CCM, nguvu ya pesa na kuwa upinzani wa kweli ulikuwa bado haujazaliwa. Walijua jinsi wale wote waliojiita wapinzani walikuwa wamenyimwa nafasi ya kula ndani ya chama.

Kwa kuyapima yote hayo, waliona ni bora kubaki na utawala wa chama kimoja, maana haikuwa na maana kuudanganya ulimwengu kwamba tunafuata siasa ya vyama vingi na huku ukweli ni chama kimoja tu ndicho kinachoshika utamu wote.

Uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi uliofanyika 1995, ulikuwa wa motomoto kweli. Baadhi ya watu waliokuwa wamechoka na ukiritimba wa chama kimoja waliihama CCM na kujiunga na vyama vya upinzani.

Watu kama Augustine Mrema, walivuma na kuleta matumaini kwamba hatimaye Tanzania inaweza kutawaliwa na chama kingeni.

Uchaguzi mkuu wa pili wa vyama vingi vya siasa uliofanyika 2000, ulishuhudia wimbi kubwa la watu waliokuwa wamekihama chama hicho cha mapinduzi mwaka 1995, wakirudi tena ndani ya chama hicho. Walio wengi hawakurudi kwa kutaka au kwa kukipenda chama. Walirudi kuyasalimisha maisha yao, kusalimisha shughuli zao na biashara zao kwa wale waliokuwa na biashara.

Ni vigumu nchi kuendelea bila kuwa na vyama vya upinzani vyenye nguvu kutoa changamoto kwa chama tawala. Ni kazi ya Watanzania wote kushirikiana kujenga nguvu za upinzani vinginevyo tutabaki kuimba wimbo wa umasikini hadi mwisho wa dunia!

Ni vyema na Rais John Magufuli, akasikia hoja hii. Ili afanikiwe katika jitihada zake alizozianzisha kwa kasi kubwa, ni muhimu afikirie kubadilisha mfumo na mtizamo wa chama chake. Huu mfumo wa sasa hivi wa Rais kuwa mwenyekiti wa chama, hauwezi kumsaidia! Mtizamo wa kuwaona wapinzani kama “Adui”, hauwezi kumsaidia. Lakini pia mfumo wa sasa hivi wa kukitanguliza chama cha siasa badala ya kulitanguliza taifa hauwezi kumsaidia katika jitihada zake. Tunahitaji kutembea pamoja kama taifa! Na kamwe tusikubali kushinikizwa na kupigishwa magoti!