HEKAYA ZA MLEVI : Tutumie akili zetu kuiga ya wenzetu

Saturday March 9 2019GASTON NUNDUMA

GASTON NUNDUMA 

By Gaston Nunduma

Katika karne tunayoishi ni aghalabu kwa mtu kuanzisha kitu ambacho hakijapata kuwapo. Leo hata ukianzisha mtindo mpya wa kuvalia suruali chini ya kitovu, jua kwamba hiyo ni suruali iliyobuniwa karne nyingi zilizopita.

Suruali ilishaanzishwa tangu karne hizo, sisi tukaiga na kuboresha kwa mitindo ya kikwetu. Tukapata bugaluu, pekos, tinabuu na mpaha hizi za vijana wa sasa wanazoziita modo.

Kwa mfano mtu mmoja aligundua tochi, na mwingine akagundua simu. Akatokea mbunifu aliyeziunganisha bidhaa zote mbili na kutengeneza simu ya tochi. Ubunifu kama huu ndio tunaouona kwenye kofia za migodini, fimbo za walemavu, nguo za kuzuia risasi (bullet proof jackets) na kadhalika. Pia ndio unaoonekana kwenye mitindo ya mavazi, magari, nyumba na hata vyakula.

Karibu kila tunachokiona kina historia ndefu tangu kilipogunduliwa. Kama historia kamili ya ugunduzi wa umeme ingeandikwa sidhani kama kuna maktaba ingetosha kuhifadhi maandiko yote. Unaambiwa kuna mtu aliitega radi ili apate umeme. Ilipopiga ikafuta kila kitu!

Yapo mambo mengi mazuri ya kuiga. Kwa mfano muziki; nyimbo nyingi zilizopendwa katika miaka ya sitini na sabini zilinakiliwa kutoka Ulaya, Zaire na Marekani. Kule kulipigwa muziki wa Jazz, Rock, Pachanga, Rhumba na mitindo mingine ambayo tuliiona inafaa katika utamaduni wetu.

Tukainakili na ndio maana ukisikiliza muziki wa Salum Abdallah Yazidu (SAY) utapata miondoko ya Amerika ya Kusini.

Pia mavazi kama Peckos, Boogaloo na Max ililetwa katika kipindi hicho na wasomi waliokwenda kuchukua elimu ya juu huko. Hata katika miaka ya themanini na tisini wazamiaji na mabaharia walituletea kadeti, jeans na raba mtoni. Tulikuwa na mchanganyiko wa mitindo kama mashati ya puto na ‘slim fit’. Nayo pia tuliiga.

Washoni wa hapa nyumbani nao hawakuwa nyuma. Walitumia magazeti na majarida ya mitindo ya nje kusanifu mavazi ya kikwetu. Kwa mfano gauni la Max liliweza kushonwa kwa kutumia kitenge badala ya kitambaa cha hariri.

Huko ng’ambo wapo watengeneza mavazi yenye umaalum wake. Kwa mfano shela ya harusi ina umaalumu wa kutovalika ila kwenye shughuli hiyo. Wapo washonaji wa nguo zinazovaliwa na matineja kwenye klabu za usiku na makasino. Nazo pia tumeziiga.

Kuiga si jambo baya, lakini umakini wa matumizi ya bidhaa unapaswa kuzingatiwa na watumiaji.

Hata huko nje wapo watumiaji wabaya wa bidhaa za aina hiyo. Kwa makusudi kabisa wanaweza kuzivaa hadharani nguo za faragha. Mfano mzuri ni machangudoa wanaojitangaza mitaani.

Nasema umakini uwe juu ya sisi watumiaji kwa sababu sisi kwa jina lingine ndio walaji wa bidhaa au mitindo hiyo. Kama chakula kimechanganywa na sumu bila shaka mlaji ndiye atakayekuwa mwathirika wa kwanza. Kadhalika mitindo isiyofaa inatuathiri sisi na vizazi vyetu wakati waingizaji wakiendelea kunufaika.

Ni muhimu kukumbushana jambo hili kwa sababu wapo watu wasio na nia njema, pia wapo wenye tama ya mafanikio ya haraka. Yaani ni kama ibada; kama ulijizoesha kila wakati kumkumbuka Muumba, kipindi utakachoacha ndipo utakutana na majaribu yasiyo na kipimo.

Pengine kama ikibidi basi tutafute sheria za kulinda utamaduni wetu. Niliambiwa kuwa zipo ila ni ya muda mrefu na haiwezi tena kukabili mmomonyoko wa maadili wa kizazi cha sasa.

Wamarekani wana viwango vyao ambapo kuanzia mwaka 1996 waliweka “G” (General) kwa watu wa umri, itikadi na jinsi yoyote. Watoto kwa wakubwa, wanadini, wenye matatizo ya kimwili na kiakili na wengineo.

“PG” (Parental Guidance) ni kiwango ambacho kinaweza kikawa na baadhi ya mambo yasiyowafaa watoto. “PG-13” ni Parents Strongly Cautioned yaani watoto wa miaka 13 ni marufuku kuangalia. “R” ni Restricted – kijana wa miaka 17 na chini ya umri huo haruhusiwi bila kusindikizwa na mzazi. Pamoja na kwamba wao walimchukulia mtu wa umri huo kuwa anaweza kujidhibiti, lakini kama nnavyosemaga kuwa kila mtu ni kichaa, kijana anaweza kuwehuka. Zinahitajika busara za kiutu uzima hapo.

“NC-17”: Hii sasa kijana wa miaka 17 na chini ya hapo hatii mguu kabisa. Hii ni kwa ajili ya watu wazima tu, na kwa wale wanaopenda kutoka na familia huwa hawanunui tiketi za daraja hii. Labda kama watawanunulia tiketi za picha lingine kwenye ukumbi mwingine, kisha wakutane baada ya muvi.

Lilipokuja suala la ving’amuzi kulikuwa na shida kidogo, lakini kulifanyika utaratibu wa kujisajili na kulipia chaneli zilizoonyesha filamu zisizofaa kwa watoto (X).

Kwa bahati mbaya tena waigizaji wetu wakahamisha yale waliyoyaona kwenye filamu hizo na kuyatia kwenye kazi zao. Pamoja na Bodi ya Filamu nchini kujua na kutafiti kwamba “filamu inalipa”, mbona wao ndo wanaacha maswali ya wahenga wa kizazi hiki? Kufanya kazi kubwa ya kudhibiti kazi hizo, sio kuangaliana usoni.

Mwaka 1993 Musical Youth walichenjiana pale Madison Square’s Gardens. Mtoto mdogo kwenye bendi ndiye aliyewataarifu kaka zake kwamba hili tunalikosea, kuna lijalo. Lakini si watoto wadogo ambao daima ndo watatuweka sawa. Wazee bado tunawajibika.

Advertisement