UCHAMBUZI: Tuwekeze katika upendo kuondoa tofauti za kisiasa

Karne ya saba baada ya uongozi wa Mtume Muhammad (SAW) katika umma wa Waislam, alifuata Khalifa Aboubaqar Swadiq kisha Omar Khattab. Wakati wa uongozi wa Omar kulitokea kisa cha mauaji.

Kijana alimuua baba mtu mzima mwenye watoto wakubwa. Wale watoto ambao baba yao aliuawa, walimkamata yule kijana na kumpeleka kwa Omar. Walimuomba kiongozi huyo apitishe hukumu ya kisasi, kwamba anayeua auawe.

Omar akataka yule kijana ajitetee. Kijana akasema yule baba aliyemuua, alimpiga jiwe ngamia wake akafa, kwa hiyo naye alimpiga jiwe ambalo lilikuwa sababu ya kifo chake. Omar akatoa hukumu kuwa kwa utetezi huo yule kijana alipaswa kuuawa.

Kijana yule baada ya kusomewa hukumu, aliomba kuahirishwa utekelezaji wa hukumu mpaka siku iliyofuata ili arejee nyumbani kuonana na mdogo wake. Alisema, anaishi na mdogo wake tu, na waliachiwa mali nyingi na baba yao, kwa hivyo alikusudia kumkabidhi zote ndipo arejee kupokea adhabu ya kifo.

Omar akamuuliza yule kijana ni nani angemdhamini ili aruhusiwe kuondoka? Kijana aliwatazama wasaidizi wa Omar, akamnyooshea kidole mmoja wao kwamba ndiye angemdhamini. Omar alimuuliza msaidizi wake aliyetajwa kama yupo tayari kumdhani kijana. Yule msaidizi wa Omar alikubali.

Watu wote walishangaa kuona msaidizi wa Omar anamdhamini mtu asiyemfahamu na akiondoka hajui angempataje. Kijana aliondoka.

Siku ya ahadi ikafika. Muda ukawa unayoyoma pasipo kijana kuonekana. Na sheria ikawa, unayemdhamini akikimbia basi adhabu yake inakuangukia wewe. Jua likazama, watu wakawa wanamhurumia msaidizi wa Omar kuwa anaelekea kuuawa kwa kumwamini mtu asiyemfahamu.

Giza la jioni kabisa, kwa mbali akaonekana mtu anakimbia. Kumbe ni kijana aliyedhaminiwa. Mara akawa amefika. Akamwambia Omar, “Nimefika kutimiza ahadi ya kupokea adhabu ya kifo.” Omar akamuuliza, aliweza vipi kurudi ili auawe wakati alikuwa na fursa ya kukimbia?

Kijana akamjibu: “Naam, nimeogopa isije kuonekana uaminifu umetoweka.” Omar akamuuliza msaidizi wake ni kwa nini alimdhamini asiyemjua? Akajibu: “Niliogopa isije kuonekana huruma imetoweka.” Hapohapo wale ambao baba yao aliuawa walitangaza kumsamehe kijana.

Omar akawauliza kwa nini wameamua kumsamehe mtu aliyemuua baba yao? Wakamjibu: “Tunaogopa isije kuonekana kusameheana kumetoweka.” Omar akamwachia huru kijana.

Mambo matatu huonekana katika upendo – uaminifu, huruma na msamaha. Mwandishi wa Marekani, Janet Morris amepata kusema: “Love see all, hate is blind.” Kwamba upendo huona vyote, chuki ni upofu.

Muhimu zaidi ni kwamba palipo na upendo, ukweli huwa na nguvu zaidi. Palipo na chuki ukweli hupata wakati mgumu. Mwalimu Nyerere aliandika kwenye kitabu cha Tujisasahishe kuwa ukweli huwa haupendi kupuuzwa na una kawaida ya kulipa kisasi.

Hata hivyo, palipo na chuki hata hayo maneno ya Nyerere hupuuzwa. Ni kama sasa, siasa zinafanya yenye kuonekana, watu wanafumba macho ili wasione, halafu wanataka wengine wote wasione.

Upendo ukidhihirika, wapinzani wataona mambo mengi yenye kufanywa na Serikali ya Rais John Magufuli. Upendo ukitamalaki, hakutakuwa na shida kwa mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu kumsifu Magufuli kwa ujenzi wa reli ya kisasa ya Standard Gauge.

Upendo ukishamiri, Taifa zima litapata baridi na huruma kwa maumivu anayopitia Lissu tangu aliposhambuliwa kwa risasi Septemba 7, 2017. Kila mtu angepaza sauti kuwataka polisi wachunguze na kutoa majibu, ikiwa ni pamoja na kuwafikisha watuhumiwa mahakamani.

Kejeli za mitandaoni zinaonesha wapo watu ama wanafurahia au wanaona sawa Lissu kupigwa risasi.

Naamini upendo ukitamalaki, hoja ya kuzuia mshahara na masilahi ya Lissu ingekuwa haramu. Unamnyimaje mshahara mtu ambaye miezi 17 iliyopita chupuchupu auawe baada ya kupigwa risasi nyingi na mpaka leo anatembelea magongo na bado hajakamilisha matibabu?