VIDEO: UDSM na maktaba ya mfano nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara

Tuesday February 12 2019

Ubora wa taasisi ya elimu hasa chuo kikuu, pamoja na mengineyo hupimwa kwa kuwapo maktaba iliyosheheni kila aina ya zana ya kujifunzia.

Wanafunzi katika ngazi ya elimu ya juu, hawalishwi maarifa, bali wanayatafuta wenyewe kupitia vyanzo mbalimbali vikiwamo vitabu maktaba.

Ni kwa umuhimu huu na nafasi ya maktaba katika maendeleo ya taaluma, Serikali ilipiga chapuo ujenzi wa maktaba ya kisasa na ya kisasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Maktaba hiyo iliyojengwa katika kampasi ya Mwalimu Julius Nyerere Mlimani, inaelezwa kuwa ya kipekee katika ukanda wa nchi zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara.

Bilioni 90 zilizotumika kugharimia ujenzi wa maktaba hiyo, sio tu zimeubadilisha mwonekano wa kimandhari wa chuo hicho kikongwe nchini, lakini pia kuhanikiza mchakato wa wanafunzi kupata maarifa kupitia maktaba.

“Ukitaka kujua ubora wa chuo nenda maktaba, UDSM imefanya imefanikiwa mno katika uwanja huo. Ni maktaba kubwa zaidi katika nchi zilizopo Kusini mwa jangwa la Sahara ikiwa na uwezo wa kuchukua watu 2100 kwa wakati moja,’’ anasema Naibu Mkurugenzi wa Maktaba wa chuo hicho, Dk Paul Muleja.

Anaongeza: “Idadi hiyo ni kwa watu wanaoingia maktaba kwa ajili ya kujisomea pekee ila pia upo pia ukumbi wa mikutano wa kimataifa wenye uwezo wa kuchukua watu 600 kwa wakati mmoja”.

Anasema maktaba hiyo ina uwezo wa kuhifadhi vitabu na machapisho 800,000 vilivyopangwa kwa ustadi kwenye makabati maalum ya kuhifadhi nyaraka hizo.

Jengo zima la maktaba limeunganishwa katika mtandao wa intaneti unatoka kwenye mkongo wa taifa na kamera 88 za usalama (CCTV) zenye kazi ya kuhakikisha ulinzi kwenye kila pembe ya jengo hilo.

Jengo la maktaba hii ni la ghorofa mbili na lina lift za kisasa kwa ajili ya kuwarahishia kutembea wanaotaka kupanda juu kwa ajili ya kujisomea.

Vitabu mtandaoni

Maktaba hiyo ya kisasa inatoa fursa kwa wanafunzi kujifunza kwa kusoma vitabu vya mtandaoni. Kuna chumba maalumu chenye kompyuta 160 kwa ajili ya wanafunzi wanaosoma vitabu mtandaoni.

Utulivu unaonekana kutawala kwenye chumba hiki, huku kila mwanafunzi aliyekuwamo humo akiwa ameelekeza uso wake kwenye kompyuta au daftari akinakiri anachokisoma au kupata ufafanuzi kwenye kompyuta.

Mhudumu wa maktaba anayesimamia chumba hiki anaeleza kuwa kompyuta hizo zimeunganishwa na mtandao pamoja na kampuni mbalimbali zinazoweka vitabu vyake mtandaoni.

“Hii inarahisisha mtu ambaye wakati mwingine anaona vigumu kusoma vitabu au asivipate kwa wakati anaotaka, atafika hapa atakisoma kitabu hicho hicho kupitia mtandao,”anafafanua.

Wanachosema wanafunzi

Uwepo wa maktaba hiyo umeleta hamasa kwa wanafunzi na pia kuwa fursa kubwa kwao kwani wana uamuzi wa kusoma kwa mtindo wa kizamani (kutumia vitabu) au kwa kwa njia ya mtandao.

Mwanafunzi wa mwaka wa tatu, Msolah Pilu anasema kwake imempa hamasa ya kutamani kusoma zaidi na kuifanya maktaba hiyo kuwa sehemu ya maisha yake ya kila siku awapo chuoni hapo.

“Naweza kusema ni kama imenifungulia dunia, badala ya kutumia muda kupiga soga naona ni heri nije maktaba nisome vitabu, nikiona nimechoka nakaa pale kwenye mtandao napumzisha akili kwa kuchati kisha narudi tena,”

Pili hatofautiani Patricia Patrick anayeeleza kuwa anajivunia kuwa mwanafunzi wa chuo hicho jambo linalompa sifa za muda wote kuwa huru kuitumia maktaba hiyo.

“Najisikia fahari, hii ni maktaba kubwa ina vitabu vingi tofauti na ile ya zamani, hivyo kuwa mwanafunzi wa UDSM nafurahia muda wote ninaojisikia kutembelea viunga vya jengo la maktaba,” anasema.

Advertisement