UFUGAJI KUKU KISASA: Yajue magonjwa ya kuku, dalili na tiba zake

Magonjwa ya kuku ni maradhi yanayoathiri afya ya kuku na kusumbua wafugaji wengi hasa wale wadogo.

Kuku, kama walivyo viumbehai wengine, hupatwa na magonjwa mbalimbali.

Kwa kuwa kuku ni mifugo ya binadamu, hivyo ni jukumu la mfugaji kutatua tatizo linapotokea ambalo hujumuisha afya yake.

Makala haya yanaelezea baadhi ya magonjwa ya kuku yanayowakabili wafugaji wengi na baadhi ya njia za kupunguza au kujilinda.

Kila ugonjwa huwa na dalili zake kuu ambazo hujitofautisha na magonjwa mengine, ingawa zipo zile za kufanana kama vile kutokula vizuri, kushusha mabawa, kuzubaa/kusinzia na joto kuwa juu. Magonjwa tunayojadili ni haya yafuatayo:

Kideri / mdondo

Ugonjwa wa kuharisha unaowapata kuku ambao huwafanya wanakufa bila mpangilio.

Dalili: Kupindia shingo juu au chini, mwendo wa kuzungukazunguka, kutembea mwendo wa kurudi nyuma huku kichwa kikiwa kimepindia chini au juu. Dalili isiyo kuu ni mharo rangi ya kijani.

Kinga/chanjo: Kuku wapewe kinga wakiwa na umri wa siku 5-7

Tiba: Ugonjwa huu husababishwa na virusi kwa hiyo hauna tiba. kinachotibika ni hizo dalili tu ila ugonjwa hubaki kwenye damu hivyo tumia Trimazine 30% na mult vitamin.

Gumboro

Dalili: Kuharisha rangi nyeupe kama chokaa. Ukimpasua baada ya kufa kunakuwa na kama matone ya damu kifuani na kwenye firigisi sehemu ya mbele.

Kinga/Chanjo: Wakinge kuku kwa kuwapa chanjo ya gumboro.

Tiba: Ugonjwa huu husababishwa na virusi kwa hiyo hauna tiba.

Mahepe

Dalili: kukakamaa kwa miguu na mabawa, hapa mguu mmoja mara nyingi huwa mbele na mwingine nyuma, kuvimba kwa kihifadhia chakula (crop), kwa kuku wa mayai huathiriwa wakiwa wadogo ila madhara hutokea wakifikisha miezi 5 wakianza kutaga.

Kinga/chanjo: Chanjo hutolewa kwa vifaranga wenye umri wa siku moja, vifaranga hupewa chanjo ya mahepe.

Tiba: Ugonjwa huu husababishwa na virusi kwa hiyo hauna tiba.

Ndui ya kuku

Dalili: Vipele sehemu zisizokuwa na manyoya kama vile vilemba vya kichwani (comb na wattle), puani na miguuni.

Kinga/chanjo: wapewe chanjo wakiwa na umri wa miezi 2 mpaka 3.

Tiba: Ugonjwa huu husababishwa na virusi kwa hiyo hauna tiba., kupunguza madhara waoshe kwa maji ya uvugu vugu yenye chumvi ya mawe hadi Vipele viishe au vipake mafuta na mpe antibiotic kama Otc 20%.

Homa ya matumbo

Husababishwa na bakteria Dalili: Mharo rangi ya njano. Tiba: Esb3, Trimazine 30%, Tylodox.

Mharo damu

Ugonjwa huu husababishwa na vimelea aina ya Protozoa na hushambulia kuku wote wakubwa na wadogo ila huathiri zaidi kuku wadogo.

Jinsi unavyoambukiza: Kula chakula chenye kinyesi au maji yenye vimelea vya ugonjwa huu.

Dalili: Kuharisha kinyesi kilichochanganyika na damu, kuku kudhoofu na kupungua uzito, Kuku kuzubaa na kushusha mabawa kamakavaa koti, Kuku kujitenga na wengine na Kupoteza hamu ya kula.

Kinga: Vifaranga wakifikia umri wa siku saba wapewe Amprolium kwa siku tatu mfululizo, hata kama dalili za ugonjwa hazijajitokeza.

Tenganisha vifaranga na kuku wakubwa; zingatia usafi wa banda na vyombo vya chakula na maji; kuku wagonjwa watengwe na kupewa tiba mara moja

Tiba: Dawa aina ya Amprolium, Oxytetracycline au Salfa ambayo huchanganywa kwenye maji na kupewa kuku kwa siku 5 hadi 7.

Kipindupindu cha kuku

Dalili: kinyesi mharo wa kijani, Kuku huhara mharo wa njano, Husinzia na kulegea, Hulala kichwa kikining’inia kwenye mabawa, Magoya husimama, Hushindwa kusimama hatimaye hufa.

Tiba: Huweza kutibika kwa dawa aina ya sulfa, Trimazine 30 % au Esb3,

Mafua makali

Dalili: Chafya, kusinzia, kuvimba sehemu za uso, kichwa na macho, ute mzito mweupe jichoni hupelekea jicho kuziba, udenda puani na mdomoni.

Tiba: Fluban, au Tylodox au OTC 20 %, Tylosan, changanya na mult vitamin.

Minyoo

Ni wa wadudu wanaoleta madhara kwa kuku na hata kwa wanyama wengine. Kuku hupata minyoo kwa kula vyakula vyenye kinyesi chenye wadudu.

Dalili: Kuku hudumaa, manyoya huwa hafifu, damu hupungua, kupungua uzito na kukonda, utagaji wa mayai hupungua, minyoo huweza kuonekana kwenye kinyesi

Kinga kuu: Kuku wapewe dawa za kuzuia minyoo kila baada ya miezi mitatu . Safisha banda kwa dawa ya kuua wadudu, badilisha matandazo, safisha vyombo vya chakula na maji,tenganisha kuku wakubwa na wadogo

Magonjwa yanayotokana na lishe duni

Kuvimba macho, miguu kukosa nguvu na kashindwa kusimama au kutembea, kutaga mayai tepetepe, kula mayai, kudonoana.

Tiba na kinga: Chakula kiwe na mchanganyiko mzuri wa vitamini na protini. Kwa kuku wanaodonoana kata au choma midomo yao na uwape mboga za majani ukiwa umezining’iniza juu kidogo.