USHAURI WA DAKTARI: Njia nne za uzazi wa mpango kwa wanaume

Utoaji wa mimba zisizopangwa na uzaaji holela usiofuata utaratibu wa uzazi mpango umepungua kwa kiasi kikubwa sana kutokana na matumizi ya njia za uzazi wa mpango.

Hata hivyo, suala la matumizi ya njia za uzazi wa mpango linaweza kuibua maswali kadha wa kadha na kuleta mdahalo kwenye jamii zetu, na maswali haya wakati mwingine huwa tuna kutana nayo sisi wahudumu wa afya; na baadhi ya maswali yanayoleta mjadala ni kama vile;Je matumizi ya njia hizi mbalimbali za uzazi wa mpango zinazingatia usawa wa kijinsia?, Njia hizi za uzazi wa mpango ni rafiki kwa afya ya mtumiaji? (hasa mwanamke kama ilivyozoeleka).

Maswali mengi yanayohusiana na matumizi ya njia za kupanga uzazi huwa yanalenga maeneo haya mawili lakini leo nitajikita kueleza kuhusiana na usawa wa kijinsia.

Suala la kujikinga au kuzuia magonjwa ya zinaa imezoeleka kuwa ni jukumu la wote wawili yaani mwanaume na mwanamke wake, lakini suala kuzuia mimba na kupanga uzazi wengi wanadhani kuwa ni jukumu la mwanamke. Na ndio maana inapofikia kwenye suala la kupanga uzazi mzigo wote wa kutumia njia mbalimbali za kupanga uzazi unabaki kwa mwanamke.

Nina imani kuwa wengi wanadhani ya kuwa, wanaume nao hawana njia zao za uzazi wa mpango, la hasha! Wanaume nao wana njia za za kupanga uzazi, na wakizitumia kwa usahihi zinaweza kuleta matokeo chanya hata kama wanawake waoau wapenzi wao wa kike wasipozitumia.

Hivyo nina imani wanaume kuanzia sasa mtaanza kuzingatia njia za uzazi wa mpango kwa lengo la kuwasaidia majukumu wanawake wenu kama nitakavyoeleza.

Kuchunga kalenda: Ni njia rahisi nay a asili ambayo mwanamke anaweza kuitumia katika kupanga uzazi, lakini haijaonekana kutumiwa na wanawake wengi kutokana na wanawake wengi kusema kuwa ni ngumu sana kuichunga kalenda na hivyo kuwasababishia kujisahau, hivyo wanawake wengi hutumia njia mbadala kama vile vidonge, vitanzi, sindano na vinginevyo.

Kisayansi, pamoja utendaji kazi wa njia hizi, lakini bado zimeonekana kuleta madhara mengine ya kiafya na madhara haya yanaweza kuwa ya muda mfupi au ya kudumu. Kuvurugika kwa mfumo wa homoni na mzunguko wa hedhi, hedhi iliyopitiliza au kukosa kabisa hedhi, maumivu ya tumbo, kiuni na mgongo wakati wa hedhi, na kupata uzito wa mwili uliopitiliza ni baadhi tu ya matatizo ya kiafya ambayo wanawake wengi huyapata kutokana na matumizi ya njia mbalimbali za uzazi wa mpango hasa kwa muda mrefu.

Matumizi ya njia za uzazi wa mpango si jukumu la mwanamke pekee hapana, ni jambo linalobeba usawa wa kijinsia. Hata wanaume nao wana njia za uzazi wa mpango wanazoweza kuzitumia na kuwapunguzia wanawake majukumu haya na ikiwezekana kuwaondolea wanawake wao adha ya kupata matatizo ya kiafya yatokanayo na matumizi ya njia za uzazi wa mpango.

Baadhi ya njia za uzazi wa mpango ambazo mwanaume anaweza kuzitumia ambazo ni rafiki kwa jinsia ya kiume ni kama pamoja na: matumizi ya kondomu, njia ya kutoa mbegu za kiume nje wakati mwanamke akiwa kwenye siku za kushika mimba, au ile inayohusisha upasuaji mdogo kwa lengo la kufunga mirija inayosafirisha mbegu za kiume kutoka kwenye korodani ili zisisafiri kwenda ukeni wakati wa tendo la ndoa. Njia hii kitaalamu inaitwa vasectomy.