Uamuzi wa Lowassa waibua kumbukizi ya Kingunge

Wednesday March 13 2019

 

By Elias Msuya, Mwananchi [email protected]

Siasa zina mengi. Wengi husema siasa ‘si hasa’. Yaani kinachoelezwa sio kinachofanyika wala kilichokusudiwa.

Hata wanasiasa wanaonekana vivyo hivyo. Juzijuzi ulisambaa msemo kwamba wanasiasa wakikwambia usiku mwema toka nje uangalie kama kuna giza. Ni kwamba wanasiasa wanafanya kinyume na wanachoeleza.

Pamoja na hali hiyo, kwa kuwa wanasiasa ndio viongozi bado miongoni mwao wapo ambao ni mifano ya kuigwa kwa mambo mema waliyoyatenda kwa umma au kwao binafsi. Pamoja na hayo wanasiasa hubadilika au kubadili kauli bila kujali walioko nyuma yao.

Kwa mfano, mchukulie Kingunge Ngombale-Mwiru. Mzee wa watu alivyojitoa mhanga kumtetea mgombea aliyeamini kuwa ameonewa akaachana na falsafa zake katika chama alichokiasisi.

Lakini mgombea huyo, Edward Lowassa hivi karibuni amerejea CCM baada ya kukaa siku 1,312 Chadema na kurudi kule alikoamini ameonewa.

Lowassa hakujali cha wafuasi wake wengine wala hayati Kingunge mwenye kadi Na.8 ya Tanu ambaye hakuficha hisia zake katika uamuzi wake. Alieleza bayana jinsi mchakato wa kumpata mgombea urais wa CCM ulivyokiukwa. Alipanda kwenye majukwaa ya kampeni ya chama hicho kumpigia debe Lowassa.

Kingunge aliendelea kushikilia msimamo wake hadi mauti yalipomkuta Februari 2, 2018 baada ya kulazwa katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili Dar es Salaam akiuguza majeraha yake ya kung’atwa na mbwa.

Wakati fulani katika siku zake za mwisho, Kingunge alisema, “CCM ni chama changu nimetoka tu nimeachana, lakini nimefanya kazi zote nimekiunda mimi kile, kwa hiyo hakiwezi kuwa kinyume changu hata kidogo.”

Ni kutokana na msimamo huo usioyumba, baadhi ya wasomi na watu wa karibu naye wanabashiri kuwa endapo angefufuka sasa na kukuta Lowassa amerudi CCM angeweza kufa tena.

Maoni ya wasomi hao wamejitokeza katika kongamano la maisha, fikra na mchango wa Kingunge lililoandaliwa na Kavazi la Mwalimu Nyerere hivi karibuni, ambalo liligongana na tukio la Lowassa kuhama Chadema kurudi CCM.

Akichangia katika mjadala huo, Profesa wa Sheria katika Shule Kuu ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Hamudi Majamba anasema Kingunge alisisitiza msimamo wake wa kuachana na CCM licha ya kutambua ukuu wa chama hicho.

Profesa Majamba anasema wakati mwanasiasa huyo anaumwa alitembelewa na Rais John Magufuli na alimwambia yeye (Kingunge) si mkubwa kuliko chama.

“Alisema ‘mimi (yeye) si mkubwa kuliko chama. Rais akasema hayo umeyasema wewe,” alisema.

Profesa Majamba alisema alipomtembelea hospitali alimuuliza Kingunge alikuwa na maana gani kuhusu kauli hiyo.

“Alisema kuna utaratibu tumejiwekea katika chama uliopitishwa katika ngazi zote. Nilijiengua kwa sababu chama ni taasisi. Walichofanya katika uteuzi wa mgombea haikuwa sawa. Kwa hiyo mimi nimejiengua ili chama kibaki,” alifafanua Profesa Majamba ambaye pia ni mkwe wa Kingunge.

Aliyekuwa msemaji mkuu katika mazungumzo hayo, Walter Bgoya ambaye pia alikuwa rafiki wa karibu wa Kingunge, anasema mwanasiasa huyo hakupenda dhuluma na ndiyo sababu ya kujitoa CCM.

“Kwa maelezo yake Ngombare aliamini kwamba CCM haikumtendea haki Lowassa kwa kutopitisha jina lake kuwa mgombea wa urais,” alisema Bgoya.

Anasema Kingunge alimtetea Lowassa hata kwenye kashfa ya Richmond iliyosababisha ajiuzulu uwaziri mkuu akisisitiza kuwa kujiuzulu kwake hakukumaanisha kuwa yeye binafsi alikuwa na hatia.

Bgoya anasema Kingunge “alijiuzulu ili kuepusha serikali yote kuanguka na kulazimisha kufanyika kwa uchaguzi. Aliongeza (Kingunge) kuwa ilikuwa imekubaliwa katika ngazi zote za chama, kwamba baada ya kujiuzulu mazingira yangeandaliwa ya kumsafisha na kurejesha heshima yake na stahili zake za kisiasa.”

Anaongeza kuwa “hayo mazingira ya kumsafisha Kingunge alisema hayakuandaliwa. Na hilo nalo la uongozi wa chama kutotekeleza ahadi yake, likaongeza uzito wa uonevu huo.”

Hata hivyo, Bgoya anasema aliendelea kumdodosa Kingunge sababu ya kumng’ang’ania Lowassa ilhali wagombea wengi waliwahi kuenguliwa CCM lakini hakuwahi kuwapigania.

“Nilimuuliza, ‘unasahau kwamba hii si mara ya kwanza kwa CCM kuwatema wale ambao kamati kuu iliona hawafai? Ni wanachama wangapi wa ajabuajabu ambao wamepitishwa katika uongozi ambao katika Kiswahili cha leo wangeitwa feki, na wangapi ambao walionekana wanafaa wakatemwa?’” anahoji na kuongeza;

“Baada ya Lowassa kurejea CCM na kupokewa kwa vifijo, alhamdulillah, Ngombare sijui kama angefurahi au la. Lakini nadhani angefurahi lakini sidhani kama angerejea naye kwenye chama.”

Wachambuzi wengine waliomwelezea Kingunge ni mwandishi wa habari mkongwe, Jenerali Ulimwengu akisema Kingunge alikuwa mwanasiasa jasiri asiyekubali mambo kirahisi.

“Alikuwa mwenye utashi mkubwa na alikuwa na uwezo wa kujieleza hata kama aliona watu hawakubaliani naye.

Watu wengi wanajiita wanasiasa lakini wanafanya mipangilio tu. Wewe kaa hapa tusiingiliane.

Kingunge alikuwa akikosoa muundo wa chama. Wanasema hakukosana na Nyerere, si kweli, walishakosana mara nyingi tu,” alisema Ulimwengu.

Anaongeza, “Siku za mwisho aliachana na CCM mpaka mwisho alifariki akiwa nje ya CCM. Kuna mambo ambayo aliona hayashughulikiwi na utawala uliopo.”

Katika kongamano hilo, alikuwapo pia Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba aliyesema walifahamiana na Kingunge tangu mwaka 1966.

Huku kila mmoja akimkumbuka kivyake katika kongamano lililohudhuriwa na ndugu za Kingunge, Profesa Martha Qorro wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anaeleza jinsi alivyomwona miaka ya 1980, wakati Kingunge akiwa na Bgoya walipokuwa wanawatembelea ndugu zake maeneo ya Kinondoni na kupiga soga hadi usiku wa manane.

Lakini hilo halikumwondoa katika mstari Tina Mfanga wa Jukwaa la Wajamaa Tanzania anayemtazama Kingunge kama mtu jasiri na hivyo akawataka vijana kushikilia misimamo yao bila kuyumbishwa na matakwa ya wanasiasa.

Mjadala juu ya Kingunge unaibua hisia kuwa, je, Kingunge angefufuka leo angejisikiaje kumwona Lowassa amerudi kwenye chama kilekile alichokipinga kwa kumwonea? Je, angemfuata tena kama Khamis Mgeja? Na angekuwapo Kingunge, Lowassa bado angetekeleza uamuzi huo? Na mwaswali mengine kibao.

Advertisement