Ubaya na uzuri wa vinywaji vya kuchangamsha mwili

Monday February 18 2019

 

By Dk Shita Samweli

Vinywaji nguvu ni vinywaji laini visivyo na kilevi vijulikanavyo zaidi kwa lugha ya Kiingereza kama energy drinks ambavyo ndani yake huwa na vitu mbalimbali ikiwamo vichangamsha mwili na akili.

Baadhi ya vinywaji hivyo ndani yake kuna maji, sukari, ladha, caffein, mitishamba, tauline (amino acid), protini, vitamini, madini na virutubisho.

Matangazo ya biashara ya vinywaji hivi huwa ni yakuvutia ikiwamo kuwaonyesha watumiaji wanavyochangamka kiakili, kuwa na nguvu na kasi jambo linalowavutia wanajamii ikiwamo wanamichezo kutumia.

Utafiti wa karibuni unaonyesha karibu asilimia 80 ya wanamichezo duniani wanatumia vinywaji nguvu ambavyo ndani yake huwa na kiambata cha Caffeine kinachoelezwa kikitumika kiholela huwa na madhara.

Swali ambalo huulizwa mara kwa mara je ni salama kutumiwa na watu wakawaida na wanamichezo?

Mjadala huu upo hata kwa wanasayansi wa tiba na Lishe, yapo machapisho kadhaa yakisayansi ya WHO yanayoeleza athari za kutumia vinywaji hivi vyenye caffein kupita kiasi na kila mara.

Wanamichezo, wanafunzi na wafanyakazi ngumu ndiyo wanaotajwa zaidi kutumia vinywaji nguvu wakiamini kuwaondolea usingizi, uchovu na kuwapa nguvu zaidi.

Wapo wanamichezo ambao hutumia ‘energy drink’ masaa machache kabla ya kuingia kucheza au mara baada ya kucheza wakiamini itawafanya kupata nguvu za ziada na kucheza kwa kiwango.

Ni kweli kiambata cha caffein husisimua mfumo wa fahamu hali inayomfanya mtumiaji ahisi kuchangamka asiye na uchovu.

Vile vile sukari na maji huwa na faida mwilini kwa kuupa mwili nguvu na maji.

Caffein huainishwa kisayansi kama kundi la opiod yaani dawa ya kulevya aina ya kichangamshi (stimulant) kiwango chake katika vinywaji hivi kinakubalika ni salama kwa matumizi ya binadamu.

Hata mamlaka za dawa na chakula zinakubali kuwa kiwango hicho, tatizo linakuja kwa watumiaji ambao wanatumia kiholela kupita kiasi bila kufuata maelekezo yaliyobandikwa katika chupa hizo.

Imewahi kuripotiwa madhara mbalimbali ya kiafya na vifo pale vinywaji hivi vinapotumiwa kiholela.

Watumiaji wa Energy Drink kiholela wanapata kiasi kikubwa cha caffein ambayo huambatana na madhara ya kiafya katika mfumo wa fahamu na damu na moyo.

Kiambata hiki ndicho kinahusishwa zaidi na madhara ya kiafya ukilinganisha na vitu vingine.

Madhara yanayoweza kujitokeza ni pamoja na degedege, kuumwa kichwa, kizunguzungu, kuzimia, hitilafu ya mapigo moyo, shinikizo la juu la damu, shambulizi la moyo na maumivu ya tumbo.

Pia uwepo wa kiasi kikubwa cha sukari na kiambata cha Taurine navyo vinahusishwa na madhara ya kiafya.

Kisayansi ni kweli uwepo wa caffein katika vinywaji hivyo una athari chanya katika mwili na akili.

Faida zake ni pamoja na kuchangamsha misuli, kuongeza wepesi, nguvu na uimara wa misuli lakini bado madhara ya kiafya ya caffein ni makubwa kuliko faida hizi.

Na hii ndiyo sababu wataalam wa tiba wanashauri watoto na wanao balehe wasitumie.

Pia inashauriwa mwanamichezo asitumie vinywaji hivi kama njia ya kuongeza maji mwilini kabla, wakati na baada ya mazoezi au mechi.

Kinywaji nguvu ni salama kwa mwanamichezo endapo tu hatakitumia mara kwa mara na atakitumia kwa kiasi pasipo kuzidisha chupa moja kwa siku.

Advertisement