Uchaguzi na umuhimu wa elimu ya mpigakura

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Semistocles Kaijage (kushoto) akijadiliana jambo na Mkurugenzi wa tume hiyo, Athuman Kihamia (katikati) na mjumbe wa NEC, Jaji Thomas Mihayo wakati wa mkutano na wadau wa vyama vya siasa uliofanyika jijini Dar es Salaam. Picha na Maktaba

Miongoni mwa majukumu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ni pamoja na kutoa elimu ya mpigakura pia kuratibu na kusimamia watu wanaotoa elimu hiyo.

Haya ni mafunzo yanayotolewa kwa raia na mamlaka zinazosimamia chaguzi kuhusu ushiriki wao katika uchaguzi.

Kwa Tanzania, zipo taasisi zinazojihusisha na uimarishaji wa demokrasia kwa kutoa elimu ya mpigakura. Elimu hii, tofauti na ile ya uraia, inalenga kuelimisha kuhusu namna ya kupiga kura na si nani wa kupigiwa kura.

Elimu ya mpigakura ni sehemu tu katika elimu ya uraia ambayo kwa kawaida inapaswa kutolewa wakati wote.

Wakati elimu ya uraia inaweza kutolewa kupitia mitaala ya shule na vyuo na kuhusisha taasisi za kiraia na zile za kitaifa na si lazima kuzihusisha mamlaka zinazosimamia uchaguzi.

Elimu inayotolewa na mamlaka zinazosimamia uchaguzi inakwenda mbali zaidi kwa kuwa na taarifa za kina kuhusu uchaguzi.

Taarifa hizo ambazo zinajulikana kama taarifa za uchaguzi au tangazo la uchaguzi ni pamoja na aina ya uchaguzi, tarehe na muda wa kupiga kura, eneo atakalopigia kura mtu aliyejiandikisha pamoja na vielelezo anavyopaswa kuwa navyo ili aweze kushiriki uchaguzi.

Asasi za Kiraia

Nchini Tanzania NEC ndiyo taasisi iliyopewa mamlaka kisheria ya kutoa elimu ya mpigakura. Hata hivyo chini ya uratibu na mwongozo wa Tume, Asasi za kiraia zinaweza kutekeleza jukumu hilo.

Elimu hii inapaswa kulenga katika kuhamasisha wapiga kura kushiriki katika chaguzi zinazozingatia uimarishaji wa demokrasia na uhusiano kati ya uchaguzi na haki za binadamu.

Hii ni tofauti na elimu ya uraia ambayo ina taarifa zinazohusu muundo wa serikali husika, mamlaka zinazochaguliwa kushika madaraka, masuala ya msingi ya kiuchumi, kijamii na kisiasa yanayolikabili taifa.

Vilevile inahusika na haki sawa kwa wanaume na kwa wanawake pamoja na umuhimu wa amani na umoja wa kitaifa.

Kuna usemi usemao ‘Hakuna elimu isiyo na maana. Kufundisha kwa elimu ya uraia au ya mpigakura katika shule na vyuo mbalimbali kunaweza kusaidia kujenga ujasiri na kuhamasisha ushiriki wa raia katika masuala yanayohusu demokrasia.

Elimu ya mpigakura imeendelea kuwa muhimu katika masuala ya upigaji kura na uchaguzi. Inawezesha wapigakura kutambua umuhimu wa kujiandikisha, kuifahamu orodha ya wapigakura na namna ya kushiriki na kupiga kura kwa usahihi.

Kwa kutambua umuhimu wa elimu hii, NEC imeendelea kutekeleza jukumu hilo kwa kuzishirikisha asasi mbalimbali za kiraia. Katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 Asasi za kiraia zipatazo 400 ziliomba kushiriki kutoa elimu hiyo.

Kuelekea 2020

Tayari NEC imeanza mchakato kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2020 na shughuli zilizoanza kufanyika kuwa ni pamoja na kuboresha kanuni za uboreshaji Daftari la kudumu la wapigakura.

Katika mkutano wake na viongozi wa vyama vya siasa, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage alieleza kuwa moja ya shughuli zilizofanyika ni uandikishaji wa wapigakura kwa majaribio katika kata mbili za Kibuta, Kisarawe na Kihonda ya Morogoro.

Mwenyekiti huyo anasema lengo la zoezi hilo ni kuvifanyia majaribio vifaa vitakavyotumika katika uandikishaji na uboreshaji wa daftari hilo utakaofuatia wakati wowote kuanzia sasa.

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la utafiti wa mitandao ya Kijamii la Ujerumani la Statista, idadi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii duniani itafikia bilioni 2.77 mwaka 2019.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi nayo imejikita katika kutumia mitandao yake ya kijamii ili kusambaza elimu ya mpigakura kwa urahisi.