Ufanye nini unapochagua kazi itakayokutosheleza?

Kazi gani unayofanya, iwe ya kujiajiri au kuajiriwa, ina maana kubwa katika maisha.

Muda unaoutumia ukiwa kazini unaweza kuwa mwingi kuliko muda unaoutumia ukiwa kwingine.

Maana yake ni kwamba unapofikiri kazi ipi uifanye kimsingi unafanya uamuzi utakaoathiri mfumo mzima wa maisha yako.

Ukweli ni kwamba kazi inaweza kukufanya ukawa mtu mwenye furaha lakini pia inaweza kukuondolea amani na kukatisha tamaa na maisha.

Katika makala haya ninakuuliza maswali kadhaa yanaweza kukusaidia kutafakari zaidi unapofikiria ufanya kazi ya aina gani.

Unavutiwa na nini?

Ukimsikiliza kijana anayefikiri afanye nini baada ya masomo yake, mara nyingi sababu anayoitoa ni mapenzi aliyonayo na kitu fulani.

Hata hivyo, mambo yanayotuvutia hubadilika kulingana umri. Kila hatua ya maisha tunayopita hutengeneza mahitaji mapya ya kimaisha yanayoweza kubadili mambo yanayotuvutia.

Kuna umri, kwa mfano, unaweza kujikuta unavutiwa na vitu visivyo halisi. Mashujaa unaowasikia kwenye vyombo vya habari, masimulizi unayokutana nayo mitaani, yanaweza kukufanya ukatamani kufanya kitu fulani kwa sababu tu umesikia kitu hicho kipo.

Kutokana na ukweli kuwa mahitaji yako hubadilika kulingana na wakati, maana yake kile kinachokuvutia leo si lazima kikuvutie kesho.

Kwa kuwa ni vigumu kujua utapenda nini kesho, kufanya maamuzi ya kazi ipi ufanye kwa kuangalia unapenda nini inaweza kuwa kosa la kiufundi.

Wengine wanafanya nini?

Kwa namna fulani wapo watu wanaoathiri uamuzi yetu. Wazazi, marafiki, watu tunaowaona kwenye vyombo vya habari wana nguvu ya kujenga ushawishi fulani kwenye maisha yetu.

Kuna uwezekano mkubwa, mtoto wa mwalimu naye atakuwa mwalimu. Mtoto wa daktari anaweza kuwa daktari kama ambavyo mtoto wa mwanasiasa naye anaweza kuwa mwanasiasa.

Pia, marafiki ulionao wana nafasi kubwa ya kuathiri mitazamo yako. Unapoona wanafanikiwa kwenye eneo fulani la kimaisha, upo uwezekano na wewe ukatamani kujaribu eneo hilo.

Changamoto ni kwamba kila mtu ana upekee wake. Siyo kila kinachofanywa vizuri na wengine basi na wewe unaweza kukifanya kwa uzuri ule ule.

Uamuzi wetu wa kazi ukiathiriwa na yale tunayoyaona kwa watu wengine uwezekano wa kutokufanya vizuri ni mkubwa.

Unafikiri mshahara utakutosha?

Vijana wanaoingia kwenye soko la ajira leo hufikiri mafanikio ya kazi yanakwenda sambamba na kipato. Lakini, pamoja na ukweli kuwa tunahitaji kipato kitusaidie kuendesha maisha yetu, ni dhahiri kuwa kipato si sababu pekee.

Wapo watu wengi wanaopata kipato kikubwa lakini bado wanalalamikia kazi zao.

Wengine wanaacha kazi zenye kipato kikubwa kwenda kufanya kazi tofauti ikimaanisha kuwa kipato kikubwa si sababu inayotosha kuridhisha nafsi zao.

Unapofanya uamuzi wa kazi ukilenga kuwa tajiri pekee, unaweza kuishia kuwa mtu mwenye huzuni. Pamoja na uzuri wa kuwa na fedha, bado kuna ukweli kwamba mafanikio yako kazini ni zaidi ya hitaji la kupata fedha.

Unagusa vipi maisha ya watu?

Kulenga kugusa maisha ya watu ni kufanya kazi inayowanufaisha watu wengine.

Kwenda mbele ya mahitaji yako binafsi na kutumia ujuzi na muda wako kuangalia watu wengine wanahitaji nini kutoka kwako.

Changamoto kwa kizazi chetu, hata hivyo, mara nyingi tunajiangalia sisi wenyewe na mahitaji yetu. Tunataka kufanya kazi zitakazotufanya tuwe bora kuliko wengine na hata kuwatumia watu kwa maslahi yetu.

Ingawa ni vigumu kufikiria mahitaji ya wengine kwa asilimia mia, unapojaribu kufanya hivyo kimsingi unajiwekea akiba ya kundi la watu linalokutakia mema.

Unatatua nini katika jamii?

Jambo la kwanza ni kujidadisi. Hapa nina maana ya kujaribu kujichunguza ili kujua kitu gani unakiona kwenye jamii ambacho wewe unaweza kuwa sehemu ya ufumbuzi.

Kwa vyovyote vile, ufumbuzi wa tatizo huhitaji ujuzi. Ikiwa unataka kuwatetea watu wanaonyang’anywa haki zao, kwa mfano, pengine ukiwa na ujuzi wa sheria au uandishi wa habari, itakuwa rahisi kufikia malengo yako.

Changamoto, kama tulivyotangulia kusema, kile unachofikiri unaweza kukifanya leo, siyo lazima ukifanye kesho kwa sababu maisha yanabadilika.

Hata hivyo, tofauti na mtu anayeamua kuwa mwanasheria ili awe tajiri au basi tu kuwa maarufu, wewe utajifunza sheria ili uweze kutatua tatizo fulani unaloliona kwenye jamii inayokuzunguka.

Kutatua tatizo la mtu mwingine, ni utoshelevu usiobadilika. Katika kila hatua ya maisha yetu, sote tunatamani kuwa watu wenye manufaa kwa wengine.

Hii ndiyo siri kubwa ya uamuzi bora ya kazi yatakayokupa utoshelevu. Kutatua matatizo halisi yanayowasumbua watu wa jamii yako. Nenda katatue tatizo ambalo pengine limepuuzwa na jamii. Kadri unavyotatua tatizo hilo, ndivyo thamani yako itakavyoongezeka, na ndivyo utakavyoendelea kufurahia kile unachokifanya.

Mwandishi ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Blogu: http://bwaya.blogspot.com , 0754870815