Uganda Cubs imepania kulinda heshima

Mambo yameshaanza kupamba moto wakati huu tukielekea katika mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika(Afcon) kwa vijana chini ya miaka 17.

Mashindano hayo yataanza April 14 hadi 28 hapa nchini na tayari makundi wameshapangwa na kila timu inajua mpinzani wake.

Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Chamazi, Uhuru vimepangwa kutumika kwa mashindano hayo na tayari vimeshaanza kufanyiwa marekebisho.

Timu zitakazomaliza katika nafasi nne za juu, zitaiwakilisha Afrika katika Fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Oktoba mwaka huu nchini Peru.

Serengeti Boys imepangwa Kundi A pamoja na Uganda, Angola na Nigeria wakati Kundi B lina timu za Cameroon, Senegal, Morocco na Guinea.

Serengeti Boys ni kama imepangwa kundi la kisasi kwani ina kibarua cha kulipa kisasi kwa Uganda ambayo iliifunga mabao 3-1 katika mchezo wa nusu fainali wa mashindano ya Kanda ya Mashariki kuwania kufuzu Afcon mwaka jana.

Pia inajiandaa kukutana na upinzani kutoka kwa Angola ambayo ndani ya miaka mitatu zilikutana mara tatu.

Gazeti hili litakuwa likikuletea makala mfululizo za timu hizo shiriki ili mashabiki waweze kuzifahamu kwa undani kabla ya kuanza kwa mashindano hayo makubwa Afrika.

Leo tunaanza na wapinzani wa Serengeti Boys katika kundi A, timu ya Taifa ya vijana ya Uganda The Cubs’.

KUFUZU.

Uganda ilifuzu mashindano hayo ya Afcon baada ya kutwaa ubingwa wa mashindano ya kuwania kufuzu fainali hizo yaliyoshirikisha nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati yaliyofanyika Agosti mwaka jana hapa nchini.

Timu hiyo ilipangwa kundi B pamoja na Kenya, Ethiopia, Sudan Kusini na Djibout.

Ilianza kwa kufungwa bao 1-0 dhidi ya Ethiopia, ikaifunga mabao 5-1 Sudan Kusini, ikaichapa Kenya mabao 3-0 na kisha ikaitandika Djibouti mabao 8-0.

Timu hiyo ilitinga fainali na kuifunga Serengeti Boys mabao 3-1 katika nusu fainali na kutwaa ubingwa wa mashindano hayo kwa kuinyuka Ethiopia mabao 3-1 katika fainali Ukanda wa Cecafa.

KIKOSI

Kama hakutakuwa na mabadiliko, Uganda itakuwa ikinolewa na kocha Peter Onen ambaye pia anaifundisha klabu ya Bul inayoshiriki Ligi Kuu nchini Uganda.

Onen anasaidiwa na kocha msaidizi Hamza Lutalo huku kocha wa makipa akiwa ni Kiberu Mubarak ,meneja wa timu ni Mutyaba Bashir na daktari ni Nakabago.

Kikosi hicho kinaundwa na makipa Oluka George William, Nsubuga Farouk, Kiberu Ronald na Ssemwogerere Daniel wakati mabeki ni Rogers John, Musa Jaggwe, Ibrahim Ekellot, Kizito Garvin na Kafumbe Joseph.

Viungo wa timu hiyo ni Ivan Asaba, Kirya Gerald, Kakaire Thomas, Ssebuliba Umar, Kawooya Andrew, Ssekajja Davis, Ibrahim Juma na Sserwada Steven wakati washambuliaji ni Iddi Abdul Warid, Anthony Kent, Mpanga Sula, Bakabulindi Moses, Mugisha Rogers, Mukisa Owen na Muber Jimmy.

NYOTA WA KUCHUNGWA

Kiungo mshambuliaji Serwadda Steven ambaye anaichezea KCCA inayoshiriki Ligi Kuu ya Uganda ndiye mchezaji anayepaswa kuchungwa zaidi na Serengeti Boys katika kundi hilo.

Kucheza timu ya Ligi Kuu kumemsaidia mchezaji huyo kupata uzoefu mkubwahuku akiwa kinara wa kutengeneza mashambulizi katika timu yake.

Kiungo huyo amekuwa chachu ya ushindi katika kikosi hicho cah Uganda hivyo wapinzani kutoka kundi A hasa Serengeti Boys inatakiwa kumchunga sana.

Wachezaji wengine wanaopaswa kuchungwa ni Ssekajja Davis, Ibrahim Juma na Nijab Yiga ambao nao wamekuwa wakiibeba timu hiyo mara kwa mara.

MAFANIKIO

Hii itakuwa mara ya kwanza kwa Uganda kushiriki katika fainali hizo za vijana hivyo ni timu ambayo haina mafanikio ya kutisha.

Mafanikio pekee waliyonayo ni kutwaa ubingwa wa mashindano ya Kanda ya Afrika Mashariki ya kuwania kufuzu Afcon .

Hata hivyo, licha ya kwanza ni timu ambayo haina mafanioo makubwa lakini inapaswa kuchungwa kwani inacheza soka safi na lenye malengo.

MASTAA ILIYOWAIBUA

Wachezaji kama Steven Bengo, Emmanuel Okwi, Kiiza Hamisi, Allan Okello na Julius Poloto ni miongoni mwa mazao ya timu ya taifa ya vijana ya Uganda wenye umri chini ya miaka 17.

KAULI YA VIONGOZI

Baada ya Uganda kufuzu Afcon,Rais wa Chama cha Soka Uganda, Moses Magogo alikaririwa akisema kufuzu mashindano hayo ni ushuhuda kuwa wanafanya kazi nzuri katika eneo la kuendeleza vijana.

Alisema hiii ni mara ya kwanza kwa timu yao ya Taifa ya vijana kufuzu mashindano hayo na naaamini watashangaza kwa kuhakikisha wanafanya vizuri kutwaa ubingwa.

Pia Kocha wa kikosi hicho Peter Onen aaliswahi kusema kuwa anaaamini kikosi chake na Serengeti Boys kitafanya vizuri katika mashindano hayo na kupeperusha vema bendera ya Ukanda wa Afrika Mashariki hivyo watu wawaunge mkono.