Ugonjwa wa baridi yabisi karaha kwa wazee

Dalili zinazoashiria kujitokeza kwa madhara makubwa na kuwa katika hatari ya kupata ulemavu kutokana na baridi yabisi ni maungio kubadilika na kupoteza mwonekano wake na kushindwa kufanya kazi.

Misuli huwa dhaifu, hupungua ukubwa wake na hunyauka.

Unapokuwa na ugonjwa huu ni vyema kubadili mtindo wa maisha ikiwamo ulaji wa mlo bora na ni vizuri kupendelea mboga za majani, matunda na maji mengi.

Epuka vyakula vya mafuta mengi, wanga na sukari ili kudhibiti uzito wa mwili na epuka matumizi ya tumbaku na ulevi wa pombe.

Utahitajika kupumzika walau saa sita mpaka nane kwa siku kuupa mwili utulivu. Shikamana na mazoezi utakayoshauriwa na mtaalam ambayo yataimarisha mauingio yaliyoathirika na kukakamaa.

Ingawa unaweza kufanya mazoezi mepesi binafsi ni lazima kuwa mwangalifu kwani kuna aina za mazoezi yanaweza kuchokoza tatazo.

Fanya mazoezi mepesi kama kutembea, yoga, kuendesha baiskeli na kunyoosha viungo vya mwili. Endapo utakuwa na maumivu makali kuepuka kufanya kazi ngumu. Usilazimishe kufanya mazoezi na katika hatua za awali, mazoezi yasitumie nguvu nyingi.

Hakikisha unafanya vipimo vilivyoshauriwa na daktari kwani vitamsaidia kuthibitisha ugonjwa na maradhi mengine. Vipimo vinavyofanyika mara kwa mara ni pamoja na xray, kujua hali ya chembe za damu na cha kutazama chembe za ugonjwa wa baridi yabisi katika damu.

Ukibainika ugonjwa husika, zipo dawa za kila aina za kukupa nafuu kwa sababu hakuna dawa ya kuponyesha tatizo hili hivyo epuka kununua dawa kiholela mtaani.

Dawa zilizopo ni kwa ajili ya kukata maumivu, kuimarisha maungio yaliyoharibika na kufifisha kinga inayoshambulia maungio. Tegemea kuandikiwa zaidi ya dawa moja na kubadilishiwa dozi tatizo linapopungua au kuongezeka.

Fahamu dawa unazotumia na tunza fomu ya daktari ili unapoenda kwa mwingine iwe rahisi kukupa matibabu sahihi. Upasuaji unaweza kuhitajika. Ni busara kuwahi hospitalini unapoona dalili.

Mwandishi ni daktari wa binadamu