UCHAMBUZI: Ujumbe maalumu kwa waheshimiwa wabunge

Waheshimiwa wabunge wa Bunge la Tanzania, huu ni ujumbe wa haraka kwenu kwa sababu taifa letu linaelekea pabaya. Ni wa haraka kwa kuwa kuna dalili za nyinyi kusahau kwamba mbunge ni wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, anawajibika kwa wananchi wote na wala si wa chama au wa mtu binafsi.

Taifa letu hivi sasa lina changamoto nyingi. Mfano, kuna kazi ya kufafanua maana ya ‘Hapa Kazi tu’. Majambazi yakiiba yanaimba kwa furaha ‘Hapa kazi tu’, wahujumu uchumi wakifanikiwa katika harakati zao, wanaimba kwa furaha ‘Hapa Kazi tu’. hata kama ni kimoyomoyo. Viongozi wote, wabovu na wazuri wanaimba kwa sauti kubwa hivyo hivyo. Ni lazima wabunge walijadili hili na kulitafutia ufumbuzi.

Tunawaomba wabunge wetu, ambao ni sauti yetu, wamuombe Rais John Magufuli atufafanulie maana ya kaulimbiu yake ya ‘Hapa Kazi tu’. Wasaidizi wake waandike vitabu na kuvisambaza, ili tusome na kuelewa. Vinginevyo itapotoshwa na jambo hili si zuri hata kidogo.

Changamoto nyingine ni ile ya kuelekea kwenye mfumo wa chama kimoja cha siasa. Hili linajionyesha wazi. Unasikika kama wito wa kumtaka kila mwananchi kuwa mwana CCM. Mtanzania yeyote anayeunga mkono mfumo huu, haitakii mema nchi yetu. Inawezekana sisi tukaishi kwa amani na utulivu, lakini watoto wetu na wajukuu wetu watachinjana. Mfumo wa utawala wa chama kimoja, hauna historia ya kuleta amani popote duniani. Kujipenda sisi bila kuangalia amani na utulivu wa vizazi vijavyo ni dhambi kubwa. Ni kazi ya wabunge kuliona hili la mfumo wa chama kimoja na kulikemea kwenye vikao vya Bunge.

Changamoto nyingine ambayo iko wazi kabisa kwa kila Mtanzania ni ile ya Katiba mpya na Tume huru ya uchaguzi. Haiwezekani wabunge wetu kukwepa hili, halafu wakatwambia wanatuwakilisha na wanaipenda Tanzania.

Tunawategemea kulijadili hili kama wabunge wetu na wala si makada wa vyama vya siasa. Ni lazima na ni muhimu wabunge wetu wakapambanua vizuri tofauti kati ya mahaba na ushabiki wa vyama vyao vya siasa na mapenzi ya taifa .

Changamoto nyingine ambazo ni kazi ya wabunge kuziangalia, kuzijadili na kuzitafutia ufumbuzi ni hali ya uchumi wa taifa letu. Shilingi inaendelea kuzama, wakati nchi yetu ina utajiri wa kila aina.

Tunataka kusikia Bunge letu likijadilia masuala ya kitaifa na kimataifa. Tunataka kusikia mijadala juu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Biashara kati ya watu wa nchi hizi na ustawi wao.

Mbunge, anapochaguliwa au kuteuliwa, anakuwa wa taifa zima, aangalie masilahi ya Watanzania wote.

Ujumbe wangu, taifa linapita katika kipindi kigumu. Wabunge ndiyo macho na mdomo wa taifa. Wabunge, wakikaa kimya, wahujumu uchumi na watu wasio wazalendo wataendelea kuila nchi na kuibakiza mifupa mitupu.

Waheshimiwa wabunge, fanyeni kazi yenu bila ya wasiwasi, tetea na kulinda masilahi ya kila Mtanzania. Mkishindwa kufanya hivyo, basi heshima mnayoipata kama wabunge, itayeyuka.