Ujuzi huu sio wa kukosa kwa wanafunzi

Tuesday November 20 2018

 

By Elizabeth Edward, Mwanafunzi

Ni furaha kwa mwanafunzi kuhitimu kidato cha sita au cha nne na kisha kujiunga na chuo kwa ajili ya kuongeza elimu zaidi.

Hata hivyo, furaha hiyo wakati mwingine inaingia dosari pale anapojiunga na chuo na kukuta kila kitu ni kipya halafu anatakiwa kwenda na kasi hiyo bila kujali ametoka kwenye mazingira gani.

Kwa hali ilivyo sasa hata kama umetoka kijijini, ukifika chuoni lazima utaijua kompyuta na utalazimika kuitumia katika muda wako wote wa masomo.

Hakuna mwalimu anayepokea kazi iliyoandikwa kwa mkono, mazoezi yote yanatakiwa kuchapwa au wakati mwingine kutumwa kwa njia ya barua pepe, hivyo ni muhimu kuwa na ufahamu kompyuta kwa kina.

Makala haya yanakupitisha katika mambo muhimu ambayo mwanafunzi wa chuo au sekondari anayelazimika kutumia kompyuta, anapaswa kuyafahamu kwa kuanzia kabla ya kujifunza vitu vingine vingi.

Kasi ya kuandika kwa kutumia kicharazo (keypards)

Jambo la muhimu kulifahamu ukishakuwa mwanafunzi wa chuo au sekondari ambaye umepata fursa ya kuwa karibu na kompyuta, ni lazima ujue kuandika kwa kasi. Kitaalamu inaelekezwa kwamba kijana ambaye hana tatizo lolote anatakiwa kuandika maneno yasiyopungua 40 kwa dakika moja.

Ukizoea kasi hiyo itakurahisishia hata pale unapopewa muda mfupi kwa ajili ya kufanya kazi za darasani kumaliza kwa wakati. Ukiwa na kasi hii utaweza kuokoa gharama za kulipia kwa ajili ya kuchapa nyaraka zozote unazohitaji.

Stadi ya kuandika kwa programu ya ‘Word’

Ukishakuwa na kasi katika kuandika, jifunze namna ya kuandika nyaraka ambayo itaeleweka na kusomeka mbele ya macho ya mtu mwingine bila matatizo. Hapa inahusisha kupangilia maneno kama ambavyo ungeandika kwenye karatasi, inapotakiwa herufi kub

wa ikae kubwa na kwenye kituo kiwepo.

Endapo utakosea neno au kitu kompyuta inakupa uwezo ya kurekebisha na kuhifadhi ulichoandika ili kisipotee. Programu ambayo inahusika zaidi katika hili ni Microsoft Word, huu ndiyo uwanja utakaojimwaga kuandikia ‘assignments’ zako.

Kuwasilisha kwa ‘Powerpoint’

Ukiwa mwanachuo uwasilishaji wa mada uliyosoma ni jambo la kawaida na lazima itategemea mwalimu ataamua ifanyike kwa mtindo gani. Inaweza kuwa kwa makundi, wanafunzi wawili au mmoja. Ili usiwe mzigo kwenye kundi ni muhimu kujifunza programu ya ‘Microsoft Powerpoint’ na jinsi ya kuitumia.

Itakapotokea unatakiwa kuwasilisha kitu mbele ya darasa au wenzio, unapaswa kuandaa nondo zako na kuziweka kwenye program hii kisha utahifadhi kwenye flash au kompyuta na ukatumia projekta kuwasilisha.

Matumizi ya mtandao

Mtandao haiishii kwenye Facebook, Twitter, Instagram na Whatsapp. Mwanafunzi wa chuo au sekondari anatakiwa kwenda mbali zaidi ya kutumia mitandao ya kijamii. Kama una kompyuta hakikisha unajua kutumia ‘search engines’ mfano Google, Bing, yahoo, Ask.com na nyingine nyingi kwa ajili ya kutafuta vitu muhimu ambavyo unahitaji kujifunza.

Kupitia mtandao ni rahisi kupata vitabu, majarida na matini mbalimbali ambayo yanaweza kuwa msaada kwenye masomo na kujifunza vitu vingine vingi vitakavyokufanya kubobea katika eneo ulilolichagua.

Marekebisho madogo madogo

Ukitumia laptop au kompyuta ni muhimu kujifunza namna ya kufanya marekebisho madogo madogo yanapohitajika. Mfano kirusi kinapoingia haina ulazima wa kwenda kwa fundi kwa ajili ya kupambana nacho; hakikisha kifaa chako kina ulinzi wa Ant virus ambayo utakuwa unaitumia kila baada ya muda kusafisha laptop yako.

Kuweka au kuondoa ‘software’ ni miongoni mwa marekebisho hayo ambayo hayahitaji utaalam wa hali ya juu. Muhimu unapopata laptop, jaribu kila siku kuichunguza na kujua kila kitu kimekaaje ili inapotokea imeleta shida uweze kubaini kitu gani hakiko sawa.

Advertisement