Ukijibu maswali yafuatayo hutadharau kazi yako

Muktasari:

  • Hauko peke yako. Tafiti zinaonesha kuwa takribani asilimia 80 ya watu wanaofanya kazi za kuajiriwa au kujiajiri hawapendi kazi zao.

Huenda wewe ni miongoni mwa watu wanaofanya kazi wasizozipenda. Unaona aibu na pengine unajisikia kufedheheka watu wakijua unafanya kazi gani.

Hauko peke yako. Tafiti zinaonesha kuwa takribani asilimia 80 ya watu wanaofanya kazi za kuajiriwa au kujiajiri hawapendi kazi zao.

Kwa hakika mambo mengi yanachangia watu kutokujisikia fahari na kazi wanazozifanya. Kuna migororo kazini, mazingira mabaya ya kazi, mtu kutokuona namna gani kazi anayofanya inakidhi makusudi mapana ya maisha yake na wakati mwingine kufanya kazi isiyokidhi matarajio ya jamii.

Jambo moja la hakika ni kwamba, kutokupenda kazi yako kunaweza kukugharimu.

Kwanza, uwezekano ni mkubwa hutakuwa na furaha hata kwenye maisha yako ya nje ya kazi, hutakuwa na bidii kazini, hutakuwa mbunifu, na matokeo yake unaweza kuharibu kazi.

Katika makala haya naomba nikupitishe kwenye maeneo matano yanayoweza kukusaidia kutathmini thamani ya kazi unayoifanya hata kama unafikiri ni kazi isiyo na maana.

Jiulize maswali matano yafuatayo:

Unafahamu wewe ni nani?

Swali hili linaonekana jepesi lakini si kila mtu anaweza kulijibu. Kwa wengi wetu, tunapoulizwa sisi ni nani, mawazo yetu yanakwenda kwenye majina yetu. Tunafikiri sisi ni majina yetu.

Lakini ukweli ni kwamba tungeweza kubadili majina yetu na bado tukabaki kuwa sisi. Maana yake sisi ni zaidi ya majina yetu.

Usipojua kwa hakika wewe ni nani itakuwa vigumu kujua unachopaswa kukifanya. Utajaribu kujifunza kila kitu, utafanya mambo mengi kwa wakati mmoja, matokeo yake hutajipambanua kwa jambo mahsusi litakalokufikisha kwenye kilele cha mafanikio.

Hatua ya kwanza ya kujitambua ni kujua vitu maalum ambavyo Mwenyezi Mungu ameviweka ndani yako.

Hapa tunazungumzia vipaji, ujuzi, maarifa na uzoefu ulionao. Vitu hivi kimsingi ndivyo vinavyobeba utambulisho wako.

Unapojiulizwa wewe ni nani, maana yake unaulizwa kuubaini uwezo wa kipekee unaoishi ndani yako. Uwezo huu ndio uliobeba thamani yako.

Unajua kitu maalum unachokifanya?

Tumezungukwa na mashinikizo ya kila aina yanayojaribu kutushawishi kuchukua uelekeo fulani katika maisha.

Mashinikizo haya, mara nyingi yanatufinyanga kufuata mkumbo unaotulazimisha kukidhi matarajio yasiyokidhi thamani zetu.

Kutokujua kitu kinachobeba thamani ya kazi tunazozifanya, hutufanya tukate tamaa na yale tunayoyafanya, hali inayochangia kutukosesha furaha ya kazi.

Hata hivyo, ukizungumza na watu wanaojivunia kazi zao unagundua hawa ni watu wanaojua kwa hakika kitu gani hasa wanachokifanya.

Hawapati shida kujua eneo lipi la maisha wanaliweza zaidi kuliko maeneo mengine. Wanajua kitu gani wanachokifanya kinachobeba thamani zao.

Hebu jiulize unazo sifa zipi maalum unazodhani zinakuweka kwenye nafasi nzuri zaidi ya watu wengine kujifunza kwako? Je, kazi unayofanya inatumia uwezo na sifa hizo unazoamini unazo?

Kazi yako inamnufaisha nani?

Kwa asili binadamu ni mbinafsi anayejifikiria yeye na mahitaji yake. Ndio maana tunapofikiri kazi gani tufanye, mara nyingi tunafikiria namna gani kazi hiyo itakavyotusaidia kuwazidi wengine.

Hakuna ubaya kimsingi kuwa mbinafsi kwa sehemu. Hata hivyo, watu wanaofurahia kazi zao wanafanya tofauti. Watu hawa, wanakwenda mbele ya mahitaji yao binafsi. Badala ya kujifikiria wenyewe, wanakuwa na aina fulani ya kundi la watu wanaolenga kulifikia kupitia kazi zao.

Kwa lugha nyingine, watu hawa wanajua kwa hakika nani ananufaika na kile wanachokifanya na hivyo wanatumia ujuzi na uzoefu walionao katika kuhakikisha watu hawa wananufaika.

Nikuulize, unalijua kundi mahsusi la watu wanaonufaika na kazi yako? Akina nani ni walengwa wa kazi yako? Ukiwatambua vizuri watu unaowatumikia, uwezekano ni kubwa utaanza kuona thamani ya kazi yako.

Kazi yako inatatua tatizo gani?

Furaha ya kazi yako inategemea pia namna gani unaamini kazi hiyo inakufanya kuwa jibu la matatizo yanayowakabili watu wengine. Usipokuwa na uhakika kazi yako inakuwezesha kutatua tatizo gani kwa watu, kwa hakika, itakuwa vigumu kuifurahia.

Unaweza kuwa na madaraka, kipato, heshima na umaarufu, lakini kama huna hakika kazi yako inakusaidia kutatua shida gani za watu wanaokuzunguka, unaweza kuendelea kujisikia utupu ndani yako.

Je, kazi yako inakuwezesha kutatua tatizo gani? Je, watu unaowalenga wanakabiliwa na changamoto gani ambazo kwa uwezo, vipaji, ujuzi ulionao unaamini unaweza kuwasaidia kuzitatua?

Ukweli ni kwamba kila kazi inaweza kukupa utoshelevu. Muhimu ni kujua aina ya matatizo unayoyatatua kwa kupitia kazi yako. Utoshelevu wa polisi, kwa mfano, unategemea namna gani anajua vile anavyowezesha watu kuishi bila hofu ya uhalifu. Polisi huyu, akiweza kuelewa tatizo analolitatua katika jamii, bila shaka anaweza kuipenda zaidi kazi yake kuliko anapojifikiria kama ‘mie polisi tu.’

Unaleta tofauti gani kwa watu?

Tunaweza kupima mafanikio yetu kwa kipato, mamlaka tulivyonayo, umaarufu lakini kama vyote hivyo haviwasaidii watu wengine kuwa bora zaidi, itakuwa vigumu kujisikia utoshelevu.

Njia rahisi ya kujua nafasi uliyonayo katika jamii ni mchango unaoutoa kuboresha maisha ya watu unaowalenga. Unapoona maisha ya watu yanabadilika kama matokeo ya kile unachokifanya kupitia kazi yako, ni wazi utapata utoshelevu zaidi.

Ukitaka kujua tofauti unayoileta kupitia kazi yako, jifunze kwenda mbele ya jina la kazi yako. Fikiria matokeo ya kazi unayoifanya katika jamii.

Kwa mfano, kama wewe ni mwalimu wa shule ya msingi, kazi yako ni kuwasaidia watoto kujitambua na kufikia ndoto zao. Kazi yako ni zaidi ya ualimu. Ukianza kuitazama kazi yako kwa mtazamo huo, unaweza kushangaa namna utakavyokuwa na utoshelevu kuliko mtu anayesema, ‘Mimi ni mwalimu tu.’

Kama wewe ni muuguzi, badala kujibana kwenye jina la kazi yako, jione kama mtu anayefanya kazi ya kuwasaidia wagonjwa kuwa na furaha zaidi wanapopata huduma za daktari.

Kwa kifupi, tukiweza kuzitathimini kazi zetu kwa kuangalia nani tunayejaribu kumsaidia, uwezekano ni mkubwa tutazipenda kazi zetu zaidi.

Christian Bwaya ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Blogu: http://sw.globalvoices.org , 0754870815