UCHAMBUZI: Ukimya wa vyama vya upinzani hauna afya

Tunapozungumzia ukimya wa vyama vya upinzani tunakuwa na maana gani? Inaelekea watu wengine na hasa wale wanachama wa vyama vya kisiasa, hawaelewi. Kuna haja ya mjadala wa hili.

Baada ya uchaguzi mkuu wa 2015, vyama vya upinzani vyote vilikaa kimya. Ukimya wa kutisha. Pamoja na ukweli wa Rais Magufuli kuzuia mikutano ya vyama vya siasa, lakini hakuzuia shughuli za vyama hivi au sauti za vyama hivi.

Mtu anaweza kuwa na mawazo kwamba vyama vingine vinaanzishwa tu ili kuvuruga uchaguzi au kuwachanganya wananchi. Vinakufa na kuibuka wakati wa uchaguzi mkuu. Hili halikuwa geni, maana chaguzi zote baada ya kuingia kwenye mfumo wa siasa za vyama vingi, daima, vyama vya upinzani vilikaa kimya baada ya uchaguzi.

Utafikiri maana ya vyama vya upinzani ni kushughulikia uchaguzi kama ilivyo Tume ya Taifa ya uchaguzi.

Hatuna maana ya Chadema na CUF tu, tuna vyama vingi vya siasa. Tunawaona viongozi wa vyama hivi hasa kwenye shughuli za kiserikali, lakini hatuoni shughuli za vyama hivi wala kusikia sauti za vyama hivi vya siasa.

Wakati wa kampeni kila chama kinaelezea vizuri sera zake, malengo yake na nia yake ya kuingia Ikulu. Baadhi ya vyama vina sera nzuri sana. Mfano Chadema, kina sera nzuri ya majimbo.

Hili alilielezea vizuri wanalielezea vizuri katika kampeni zao. Au sera ya kuwaondoa wakuu wa wilaya, ni nzuri na kufuatana na maelezo ya Freeman Mbowe, ni kweli watu hawa wanakula pesa bure. Hoja ziendelezwe hata baada ya uchaguzi, watu wajadili na kutoa maoni. Muhimu ni maoni ya watu na wala si maoni ya mtu binafsi au chama cha siasa.

Ukweli ni kwamba siku za kampeni ni chache mno. Na yale watu wanayoyasikia bila kuyasoma, wanayaacha pale. Zile zilikuwa ni kampeni. Baada ya kampeni, hata kama chama hakikufanikiwa kuingia madarakani ni lazima kiendeleze sera zake, ni lazima kifundishe sera zake kwa wananchi.

Nyuma ya sera za chama ni lazima kuwe na falsafa ya chama. Mfano sasa hivi tungekuwa tunasoma mahali mfumo wa utawala wa majimbo, aliokuwa akiuelezea Mbowe. Haya yangekuwa yameandikwa vizuri katika vitabu ili watu wajisomee. Tunasema kwamba Watanzania ni wavivu wa kusoma, lakini si wote ni wavivu. Wako watu ambao wanataka kusoma na kuelewa mambo yanavyokwenda. Viko wapi vitabu vya Chadema kuhusu majimbo? Kama havipo, basi hiyo ndoa maana ya ukimya! Kama tunaogopa kufa na kupigwa kwenye maandamano, ni lazima kubuni mbinu mpya za kisayansi na kiteknolojia.

Kwa vyovyote vile kama vyama vya siasa vinamaanisha kufanya siasa, ni lazima kazi iendelee hata baada ya kushindwa uchaguzi

Jambo hili ni lazima liendelee. Ni kazi ya vyama vya siasa kufundisha elimu ya uraia. Ni bahati mbaya hata CCM, haina programu ya kufundisha elimu ya urai. Watu wanakwenda tu gizani, hawajui haki zao za msingi, hawajui uwezo wao wa kuiweka serikali madarakani na kuitimua pale inapofanya vibaya.

Wananchi hawajui kwamba wao ndio waheshimiwa, badala ya wawakilishi wao.