Ukiona unajipunguza umri jua kuna sehemu umeshakosea

Hii mada ya leo inawahusu zaidi wadada. Nadhani kwa kuwa wanaume wanachelewa kuzeeka kuliko wanawake, umri haujawahi kuwa ishu. Mwanaume mpaka aanze kuota mvi, mwanamke wa umri wake anakuwa tayari ameshasogea sana.

Unaambiwa katika makosa ambayo mwanaume hatakiwi kuyafanya ni kumuuliza mwanamke kuhusu umri wake. Hili limekuwapo muda mrefu nami kwa utafiti wangu ambao haujapitisha na mamlaka yoyote nikagundua kwanini inakuwa hivyo.

Nimekutana na wanawake wenye umri mkubwa na wanajivunia. Yaani anataka apewe heshima yake ya udada au mama kwa lazima tofauti na wengi.

Katika kautafiti kangu nimegundua kuwa wengi wanaoficha kuhusu umri wao halisi kwa kuwa kuna mambo fulani hayajakaa sawa.

Katika kila hatua katika ukuaji wa mwanadamu unahitajika kukamilisha kufanya jambo fulani. Kwa mfano mtoto anapoanza darasa la kwanza akiwa na umri wa miaka 12 lazima kutakuwa na kautofauti. Wengi wanaanza shule wakiwa na chini ya umri wa miaka 17.

Inawezekana kabisa huyu ili kwenda sambamba na wenzake itabidi ajishushe umri ili aendane na mazingira. Vivyo hivyo katika elimu ngazi zote isipokuwa labda chuo kikuu.

Sasa hata katika maisha ya kawaida, kuna wakati itabidi uanze kujitegemea, uanzishe familia, ujenge, ununue gari na kufanya mambo mengine ya maendeleo ikiwamo kuheshimika mbele ya jamii.

Inapotokea sasa baadhi ya mambo hayaendani na umri. Yaani miaka imesonga lakini hatua za kijamii zipo nyuma hapo ndipo inapolazimika kurudisha nyuma wakati.

Hawa ndio wale ikitokea mwenzake kamzidi mwaka mmoja tu dada dada zinakuwa nyingi na shikamoo za kutosha.

Inasaidia kuidanganya jamii, lakini ukweli unabaki kuwa namba imesoma. Muhimu ni kufanya jambo kwa wakati na kukubali pale hatua fulani inaporuka.