HEKAYA ZA MLEVI: Ukistaajabu ya benki, utaona ya dalali

Abunuwasi alikwenda kwa jirani kuazima sufuria kubwa. Alipewa, akapikia pilau na kuisherehesha sikukuu yake. Baada ya siku chache aliirudisha ikiwa na sufuria ndogo ndani yake. Jirani akashangaa na kumkumbusha kuwa aliazima ile kubwa tu. Akajibu kuwa ile kubwa ilizaa. Jirani alifurahi sana na kuiona nyumba ya Abunuwasi kuwa ya baraka.

Mara ya pili alikwenda tena kuazima sufuria ileile. Inaeleweka kuwa wazoefu wa shughuli ndio wanaomiliki masufuria makubwa, majamvi na maturubai. Jirani alipoazimwa sufuria kwa mara ingine alifurahi zaidi. Aliwaza kuwa pengine safari hii inaweza kurudi na mapacha.

Lakini baada ya siku chache Abunuwasi alimjia akiwa na huzuni tele. Kiunyonge akampa mkono jirani yake: “Pole sana, yote ni mapenzi ya Mungu…” Jirani alishangaa maana hakuwahi kupokea taarifa ya msiba kwa wakati ule. Akauliza sababu ya hiyo pole, Abunuwasi akamjibu kuwa sufuria yake imekufa!

Kwa sababu hakuna ambaye hakumjua Abunuwasi kwa vituko vyake, jirani aling’amua janja ya huyu jamaa na akamchimbia biti kuwa kama hatairudisha siku hiyo atampeleka kwa Kadhi. Wakati huo shughuli za mahakama zilisimamiwa na Kadhi ambaye alikuwa ndiye Sultani mwenyewe, Harun bin Rashid.

Asubuhi iliyofuata jirani alikwenda kufungua shtaka. Maelezo yake yalimfanya Kadhi na wasaidizi wake kucheka mpaka kugalagala. “Sufuria imekufa? Ebu kamlete huyo mjinga tuvunje kabisa mbavu zetu hapa,” walimwambia na mbio jirani alichukua askari na kumfuata.

Abunuwasi akafikishwa mbele ya baraza akiwa kavalia nguo za msiba. Alieleza vizuri jinsi alivyoazima sufuria bila kujua kuwa ilikuwa na ujauzito. Alipomaliza tu kuitumia ikajifungua salama mtoto wa kiume. Akairudisha na kichanga chake.

Alipokuja kuichukua kwa mara ya pili hakujua kuwa ilikuwa inaugua. Alipoiweka jikoni pengine kwa sababu ya joto kali ikafa. Na siri ya sufuria, ikifa huyeyuka na kutoweka.

Mwanzoni wazee wa baraza walicheka mpaka wakalia. Lakini kadiri simulizi ilivyokuwa ikishuka walibaki midomo wazi kwa mshangao.

Walipomuuliza jirani alikiri kuziweka pamoja sufuria zake bila kujua jinsia zake na bila kujua kuwa zilikuwa na mahusiano. Pia alikiri kupokea kichanga cha sufuria kutoka kwa Abunuwasi. Wazee walikuna vichwa hadi vikatoa unga!

Kwa kawaida maswali tata hujibiwa na vitabu vya dini. Wazee wakazama humo, wakapekua lakini hawakupata jibu la sufuria kuzaa. Lakini Abunuwasi aliwaongoza kuwa wasiutafute upepo wangali wakiupunga. Sufuria kuzaa au kutozaa si hoja; ishu ni je, kuna kinachozaa ambacho hakifi?

Mwongozo wake ulisababisha waitwe wanazuoni. Baada ya kupitia maandiko na kuyatafakari walitoka na jibu kuwa hakuna ushahidi wa sufuria kuzaa, lakini kulikuwa na ushahidi kuwa hakuna kilichozaa kikakosa kufa. Abunuwasi akatoka kifua mbele.

Hesabu zake zilienda sawa. Ili kuiiba sufuria alianza na mipango; kwanza aliitia uhai (ujauzito, uzazi na maradhi) kisha akaiua. Kumbuka wakoloni walianza kuleta wapelelezi, wakafuata wavamizi, halafu Wamishenari kisha watawala. Ni sawa na kuleta mikataba mitamu na mwisho wake ukawa mchungu.

Siku moja nilisikia tangazo kuwa ndani ya dakika chache tu unaweza kupata mkopo mkubwa wa kuweza kujenga nyumba kubwa. Nikaanza kujiuliza maswali ya kilevi: Fomu inajazwa saa ngapi? Afisa mikopo anakagua dhamana saa ngapi? Meneja anaidhinisha saa ngapi na mkopo unatoka saa ngapi?

Nilijiuliza haya kwa sababu hakuna anayekupa kitu bila sababu pasipo na sababu. Ukimwona mtu “anakasaidia” kabinti kako fedha bila sababu yoyote, ujue ana sababu. Hakuna binadamu aliyeweza kufikia viwango hivyo isipokuwa manabii, ambao karibu wote waliuawa.

Inanikumbusha mtu aliyekopa kwa rehani ya shamba la familia. Siku hiyo jamaa alipewa gari na hela za mfukoni ili kufuatilia hati na mambo yake mengine. Meneja wa benki, ofisa mikopo na mawakili walipatikana katika muda muafaka, fomu zikajazwa. Ofisa akahakiki, meneja akaidhinisha na jamaa akachukua mzigo.

Miezi michache baadaye mkopaji alifanikiwa kupata fedha mahali, akataka kulipa deni lote kwa pamoja ili arudishe hati ya watu… Ah wapi! Kila akiongelea mawio wenzake wanamjibu ya machweo. Aliambiwa njoo kesho; meneja kasafiri; ofisa mikopo anauguliwa na kadhalika.

Siku ya kulipa ilipowadia wadai wakazima simu. Jamaa alikwenda ofisini akakuta shughuli nyingine kabisa zikiendelea. Kila akiuliza mawakala wa benki watu wanamwangalia kwa jicho baya na kunong’onezana “au dishi limeyumba?”

Asubuhi na mapema alipigiwa simu na mwangalizi wa shamba. Alimwambia kuwa ameagizwa na kampuni ya madalali kutoa nafasi ili shamba lipigwe mnada.

Mwanzoni nilidhani ni vibenki vidogo vidogo tu ndio vinavyoleta machachari haya, lakini nilipomsikia mkuu wa mkoa mmoja akimtemea cheche meneja wa benki kubwa sana nchini, ndipo nikaelewa. Alichefuliwa aliposikia kwamba nyumba ya mama mmoja ilipigwa mnada ati kwa mkopo wa rafiki. Itaendelea...

kuwa rafiki wa mama huyo alipeleka nakala ya hati ya nyumba ya mama, akachukua mzigo na kula kona. Na hilo pia halikutosha, mdaiwa ambaye ni rafiki wa huyo mama akajieleza kuwa dhamana yake ilikuwa ni kiwanda chake cha bidhaa za mbao na vitu vyake vya ndani. Ama kweli ukishangaa ya Musa utaona ya Firauni. Mkopo wa Benki kwa fotokopi ya swahiba!?!?!

Inaendelea toleo lijalo