HEKAYA ZA MLEVI: Ukistaajabu ya benki, utayaona ya dalali

Saturday April 20 2019

 

Ilielezwa kuwa mkopaji alipeleka nakala ya hati ya nyumba ya rafiki yake, akachukua mzigo na kula kona. Na hilo pia halikutosha, mdaiwa ambaye ni rafiki wa huyo mama akajieleza kuwa dhamana yake ilikuwa ni kiwanda chake cha bidhaa za mbao na vitu vyake vya ndani. Ama kweli ukiyashangaa ya Musa utaona ya Firauni. Mkopo wa benki kwa fotokopi ya swahiba!?!?!

Ukipita mitaani utakutana na watu wasio na idadi walioingizwa mkengeni kwa mitindo ya matapeli wa mikopo. Wa kwanza niliyekutana naye alikuwa mfanyakazi aliyekopa akaongeze elimu. Alinipa majibu ya maswali hata nisiyouliza. Ilikuwa sawa na kunishangaa kuwa “ina maana hata wewe hujui?”

Yeye aliingia mkataba wa miaka mitatu kwa dhamana ya hati ya kiwanja. Lakini baada ya mwaka mmoja nyota njema ikawaka. Akaona bora arudishe kiasi chote cha mkopo, arudishiwe hati yake ili apate uwezo wa kuomba mkopo wa ujenzi. Lakini kwa mshangao mkuu akazungushwa kisha akakataliwa bila sababu!

Mimi naamini benki wana sababu. Huwezi kulipa deni ukakataliwa bila sababu pasi na sababu. Lakini ni zipi hasa na kwa nini zisiwe bayana? Zingatia kuwa bado kuna mamilioni ya Watanzania wanasubiri mikopo. Sasa mtu akirejesha mkopo wa mwanzo si ndio anatoa nafasi kwa mwingine kukopa?

Kwa maisha tunayoishi ni jambo gumu kuweka akiba hadi itosheleze ujenzi wa nyumba. Binafsi nilishawahi kumfanyia mtu kazi akanilipa Sh400,000. Katika miaka ya mwanzoni mwa 1990 zilikuwa hela nyingi sana, nikazificha chumbani ili kesho niwahi kuzihifadhi benki.

Waliosema hela shetani hawakukosea hata kidogo. Kokote nilipoenda nilihisi zikiniita. Nikazisikia zikinukia, nikajiuliza “pengine chumba kimeshika moto… zinaungua…” Nikatoka mbio hadi kwenye chimbo langu. Nikazikuta zipo salama usalimini.

Sasa nikatoa jamvi na kulala chini ya mwembe. Baada ya muda kausingizi kakanichukua. Nikaota sauti kama ya karatasi zinazokatwa na mikasi. Taratibu nikafumbua macho na kuona siafu wanazungukia maeneo yale… Astakafuru! Hawa watakuwa wanazigegeda hela zangu!

Nilitoka mbio hadi ndani lakini nikazikuta zimetulia tuli. Sasa niling’amua kuwa shetani wa hela anaanza kunipanda maana kila nilichokiona kilikuwa na rangi ya noti. Nilipokunywa maji nilihisi ladha ya bia barrrridd…

Nikaona usintanie: Hii hela nimeisubiri muda mrefu sana, tena nilikwisha kuiwekea malengo. Siwezi kuongopewa hata na mkubwa wa mashetani nikaifanyia anasa! Niliitoa sandukuni, nikachana godoro, nikaziingiza na kuzishonea humo. Ili kuondoa vishawishi nikaamua kulala ili kesho ifike mapema.

Lakini siku ya kufa nyani hakuna mti unaoshikika. Kila nilipokaribia kupata usingizi nilihisi zikinipapasa na kuniomba tukatembee. Kilichotokea baada ya kuridhiana nazo huwa sipendi kabisa kukikumbuka, lakini ule mchezo wa “hii sasa nachomoa ya mwisho” ulihusika sana.

Sipendi kabisa kuukumbuka mzimu ule, lakini hii tabia ya wanaojiita maofisa kuchezea kipato chetu inaniumiza sana. Vijana wa sasa waliozisoma pesa darasani wanajifanya kuzijua kuliko wenyewe wanaozisaka kwa jasho. Hata kama kuna kiza akiinusa tu anakwambia “hii elfu mbili” au “hii feki”.

Yaani benki zetu sijui zinachanganyikiwa na nini. Kwa wenzetu benki zinahifadhi hadi nyaraka muhimu kama hati za nyumba, viwanja na hata mashamba. Sasa hapa kwetu ukifanya hivyo utakuwa salama kweli?

Kapo kabenki kamoja ambako wakazi wa Kusini waliandamana wakidai kanaiba taarifa za wafanyakazi na kuwaingizia pesa bila makubaliano. Ukiona salio linasoma zaidi ya mshahara basi ndo ushakopa hivyo! Ndio kazi ya maofisa mikopo na biashara hiyo!

Mimi nina wasiwasi sana na vibenki vinavyoibuka kila kukicha. Kakifanya kazi miaka minne kanajitangaza mufilisi na kubadilishwa jina. Kama kalisajiliwa kwa jina la Soni katabadilishwa jina na kuitwa Sonic. Sasa sijui ndio kuendeleza ile misamaha ya kodi? Tena niulize: Hivi ile misamaha bado ipo?

Nakumbuka enzi zetu tulikuwa na hoteli ya kitalii, tena kwenye viwanja vikubwa (hapa nna maana ya Old Upanga Road, Gymkhan n.k.). Hii hoteli kwa wakati huo ilifananishwa na zile wanazofikia Wafalme wa Uarabuni pindi wanapotembelea Amerika. Inafanana kwa hadhi na Hoteli bingwa zilizoitwa “Hiltons”.

Basi kituko cha kwanza kilikuwa ni kusamehewa kodi kwa miaka mitano ya mwanzoni. Nadhani sababu ya umaarufu wake na kukubali kuwekeza nchini. Walishaimba tangu zamani “Mgeni siku ya kwanza mpe ugali na panza”. Lakini “Siku ya kumi” aondoke hata “kwa mateke na magumi”.

Lakini mgeni aliishi bila mateke wala magumi kwa miongo mingi tu. Badala ya kumzungumzia, mwenyeji akawa akibadili mada na kuanza kumsifu kwa majina yake mazuri. Kumbe mwenzio anajifilisi na kuiuza kwa mkewe, baadaye kwa mwanaye wa mwisho, akitoka hapo anaiuza kwa jina lake la utotoni n.k.

Wafanyakazi wa Tanzania ni masikini. Mishahara yao haikidhi mahitaji ya msingi ya mwezi mzima. Wanakosa uwezo wa kujenga, kusomesha, matibabu na kadhalika hivyo hulazimika kukopa.

Wanalazimika kukopa ili maisha yaende. Wakati wa kulipa wanasugua kweli kweli lakini potelea mbali. Watafanyeje?

Kuwadhulumu watu wa aina hii maana yake ni kuwaua.

Advertisement