NDANI YA BOKSI: Ukiyaishi maisha ya King Kiba, joto la corona litapita hivi...

2016... ‘Ostabei’ jijini Dar es Salaam. Ilikuwa ni mida mibovu. Kichwani nimetanguliza ‘sanitaiza’ kadhaa. Si zile za kutakatisha mikono kukwepa ‘korona’. Hapana! Ni za kulainisha akili ifanye kazi haraka. Jambo la kujishauri mara mbili sikuhitaji muda huo.

Mjivuni mimi. Nimeweka pozi la kimadaha utadhani ndiye mzalishaji wa ‘corona’. Najidaidai bila sababu za msingi. Ndo uzuri wa ‘sanitaiza’ ya akilini. Ikikolea inafanya uwe mtu wa kujiamini hata pasipostahili. Ndo maana ajali zinakuwa nyingi, sehemu ya kuhofia, ‘sanitaiza’ ya akilini inakupa jibu: “Acha woga pita na spidi 120.”

Nimevimba. Ni kwenye baa moja maarufu. Siwezi kuitaja, haipo ilipitiwa na ‘corona’ yake, mmiliki aliishiwa ‘sanitaiza’ ya kulinda mtaji.

Yes! Kila mtu ana uso wenye nuru, utembeaji wa uhakika na maongezi ya kijivuni. Kiswahili kilichozidiwa na sentensi za Kiingereza. Sasa mtu anasema: “Imejini covidi naintini, imesambaa olo ova ze woldi ini tuu manthi. Hiyo ni veri denjarazi kwa kweli. Na amshoku kuona pipozi araundi mii zei teki iti simpo laiki taarifa za nzige vile.”

Kuna maeneo Daslama mjini, Mji aliokulia Bibi Titi, Kiswahili kinatengwa na kuwekwa karantini ya kinywani. Ndo eneo nililokuwepo usiku huo. Kuhusu idara ya totozi usiseme. Kwanza picha linaanza ni ubora wa warembo wale. Ilikuwa vigumu kujua hata utaifa wao.

Nilikuwa na mrembo ambaye kufika kwake pale kula na kunywa ni juu yangu lakini hali hiyo haikusaidia mimi kuumiza shingo kutazama warembo wengine. Naikumbuka siku hii maana ni ya mwisho kuongozana na totozi sehemu. Wakati niko njiani nilijiona nimeongozana na malkia. Nilipofika baa na kukaa nikaona nipo na jinsia nyingine tu. Sasa ile ‘sanitaiza’ ilipokolea na kuona totozi zingine. Nikajiona mimi na msela mwenzangu tu.

Nadhani hata yeye hakuona ajabu mimi kumpuuza. Kuna wakati warembo wanawajua zaidi yao. Anachagua kuvumilia au kujivua pendo. Alichagua uvumilivu. Kama kuna wanaotazama wataona namnyanyasa kijinsia. Huwezi kuwa na dem hapo hapo ukawa bize kutazama wengine. Ni zaidi ya dharau.

Ikibidi nibadilike, nikawa bize naye, namtazama huku nikimsemesha kwa maongezi flani ili kama alikasirika apoe. Lakini kadiri nilivyoendelea nikagundua siko naye pale kiakili wala kimasikio, macho yake yalikuwa yakitazama kitu kilicho nyuma yangu. Nikapiga pafu moja kuzuga, nikageuka kuangalia anachotazama. Nikaona kundi la vijana wa kike wachache na wa kiume kadhaa. Sikuwatazama sana nikageuka kuendelea na ‘bebe’ wangu. Yeye bado macho yako kwao, haikunitisha lakini kabla sijanyanyua glasi tena nikashituka. Kuna kitu kichwani ‘kilikliki’ kuwa katika wale vijana kuna mmoja, tena machachari.

Kumbe nikiwa bize kutazama ubora wa uumbaji wa muumba, naye akapata nafasi kutazama kilichomvutia.

Nami sikushangaa anachoshangaa. Dem yeyote nchi hii akikutana na Kiba atakosa utulivu wa macho na akili. Anapendwa mchizi. Kumshangaa dem anayemshangaa Kiba baada ya kukutana naye ni kulazimisha kuukataa ukweli wenye ukweli. Asipomshangaa King Kiba unataka amshangae mbunge wako au balozi wako wa nyumba kumi huko kwenu Kimara?

Nilichogundua ni kuwa Kiba alikuwa kikazi. Alialikwa na mmiliki wa eneo lile kwa malengo ya kibiashara. Pamoja na mtungi kichwani. Haikunizuia kuwaza kuwa Kiba ni vigumu kukutana naye maeneo ya batani.

Ni staa anayeishi kiustaadh, kiinjiisti kama si kilokole. Aina ya maisha yake hayafananii na afanyacho (muziki). Kuna wasanii wana vibweka, fujo, na matukio kibao mchana na usiku. Lakini hawafikii robo ya umaarufu wa King Kiba. Unajiuliza huyu angekuwa Kiba ingekuwaje? Lakini hii haina maana kuwa muziki unahitaji mwanamuziki mwenye tabia za Kiba. Ukweli ili uwe staa mkubwa kama Kiba kimuziki, usiishi aina ya maisha anayoishi. Utachelewa sana.

Aina ya maisha ya Kiba hayaendani na fujo za soko la muziki duniani. Kifupi muziki hauna urafiki na tabia za Kiba. Unapoona yeye anapasua anga na tabia zake zile. Hapo ndipo unapokuja upekee wa kipekee wa King Kiba. Inashangaza kidogo. Yaani Kiba anasimama juu ya kilele cha ustaa kwenye sanaa ya muziki, huku akiishi kwenye uzio wa tabia za Kiinjilisti. Anaweza kuwa na kiburi cha ubinadamu. Ndiyo! Lakini kiburi chake kinafunikwa na tabia zake za kujitofautisha na ujinga wa wenzake.

Anaweza kuwa na dharau, lakini akawa anajitofautisha sana na dharau za wenzake. Na wakati mwingine mapambano yake ya kutaka kuwa tofauti na tabia mbovu za wenzake yanazalisha dharau na kiburi ndani yake. Mtu anayeweza kumuita sehemu kwa lengo la mtu huyo kutafuta kiki. Kiba akashitukia na kukataa. Kwa huyo ataonekana kiburi na huyo mtu kugeuka dalali wa kutangaza kiburi cha Kiba.

Kiba unaweza kutomsikia kimuziki, wala kwenye matukio makubwa kama haya ya corona. Lakini anabaki kuwa msanii mkubwa kati ya wakubwa waliopo. Wapo ambao wametumia vipaji na umaarufu wao kuelimisha jamii juu ya corona. Lakini wapo ambao walitaka au wameitumia corona kama kiki kutaka ‘kutrendi’ kama kawaida yao. Lakini Kiba ni kama hayupo vile.

Kiba ni mtoto wa Kariakoo. Mtoto wa mjini kweli kweli. Kariakoo ndo tafsiri rahisi na sahihi ya utoto wa mjini. Lakini tabia zake haziakisi makuzi ya Kariakoo. Kitu kinachoakisi makuzi yake ya Kariakoo ni kupenda na kucheza soka basi. Maeneo aliyozaliwa na kukulia yamezungukwa na klabu kubwa zaidi Afrika Mashariki za Simba na Yanga.

Kiba huwezi kumuona maeneo ya starehe kama hana kazi la kufanya. Huwezi kumkuta mitaani wala kwenye kurasa za mitandao huko akiposti hovyo au kubishana na watu. Ukubwa na uzito wa jina lake hauendani na tabia zake. Uliza tabia za mastaa wakubwa wa aina yake wa kale na sasa kwenye muziki. Kuwa na tabia zake ni kipaji kigumu kuliko kipaji chake cha muziki.

Corona inatulazimisha wote tuwe kama King Kiba. Tusiende mitaani kama hatuna jambo la msingi huko. Mitungi tugongee ndani badala ya kubishana katika kaunta za baa na kurushiana mate hovyo. Ukifuatilia maisha ya Kiba na kuyaishi, itakuwa rahisi kuepukana na maambukizi ya corona. Uchune geto tu kama huna mchongo wowote mtaani. Corona ni miyeyusho kuliko mnavyodhani. Waambie wana corona ni noma.